29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Ufumbuzi wa kidijitali, kichocheo cha maendeleo ya kilimo Tanzania

Mwandishi Wetu

Kilimo ni sekta kubwa inayochangia uchumi wa nchi nyingi barani Afrika. Kwa mujibu wa takwimu ya kilimo Afrika ya mwaka 2017 (Africa Agriculture Status Report 2017), sekta hii inachangia zaidi ya asilimia 30 ya pato la bara hilo na kuajiri zaidi ya asilimia 60 ya nguvu kazi.

Katika nchi za Afrika, kilimo ni njia ya kuleta maendeleo, kuondoa umasikini, kutengeneza ajira, kupanua biashara na uwekezaji baina ya nchi za Afrika na viwanda na maendeleo ya kiuchumi.

Nchini Tanzania, kilimo kinaajiri asilimia 70 ya wananchi na huchangia hadi asilimia 30 ya pato la taifa. Pamoja na mchango wake kwenye uchumi, sekta hiyo bado inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na miundombinu duni, upatikanaji mdogo wa fedha na ukosefu wa njia za kuaminika za taarifa kama vile utabiri wa hali ya hewa na bei za masoko.

Kwa miongo kadhaa, Serikali ya Tanzania imekuwa ikibuni na kutekeleza sera za kukabiliana na changamoto hizo, hata hivyo, kilimo cha kujikimu bado kinategemewa zaidi.

Hadi sasa wakulima wengi wanategemea zana za kilimo za jadi kama vile majembe ya mkono, kwani vifaa vya kisasa ni gharama sana.

Zaidi ya hayo, katika baadhi ya jamii wakulima hulima kulingana na msimu wa mvua ambao husababisha mavuno yasiyolingana na nguvu iliyotumika kwa sababu mvua hizi hunyesha kwa kusuasua.

Lakini hivi sasa tunashuhudia jinsi teknolojia inavyochochea ukuaji wa sekta ya kilimo katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara.

Uwepo wa simu bora na za bei nafuu umeongeza upatikanaji wa mifumo ya kidijitali, ambayo imesababisha uvumbuzi wa huduma za kilimo kama vile, zana (app) za utabiri wa hali ya hewa, na vipima udongo zinazosaidia katika kusimamia ukuaji wa mazao kwa wakati halisi, pamoja na programu ya usimamizi wa kilimo na ndege za umwagiliaji zisizo na rubani (drones).

Pia kuna mifumo ambayo hutoa onyo mapema pale kunapokua na tofauti katika ukuaji wa mazao.

Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania Plc ambayo ni miongoni mwa wavumbuzi wanaoleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo ilizindua zana (App) iitwayo ‘Connected Farmer’ ambayo inaunganisha wakulima na wanunuzi na pia inatoa taarifa kuhusu bei za mazao sokoni, utabiri wa hali ya hewa na vidokezo kupitia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (SMS) ambazo huwasaidia wakulima wasiotumia simu janja (smart phones) kupata taarifa kupitia simu zao za analojia.

Mkurugenzi wa idara ya biashara Vodacom, Arjun Dhillon anasema nguvu ya teknolojia katika kubadilisha jamii haiwezi kupingwa na ndiyo maana Vodacom Tanzania inawekeza sana katika ubunifu hasa katika sekta muhimu ya kilimo.

Anasema Tanzania ina zaidi ya wakulima wadogo milioni nne na maofisa kilimo zaidi ya 3,000, pia asilimia 70 ya uzalishaji wa Kilimo Afrika Mashariki hutokana na Wakulima wadogo wadogo, na kwa kawaida wakulima hawa wana maeneo ya ukubwa usiozidi heka mbili, hivyo kufanya mahusiano ya wakulima, shughuli na usimamizi wa taarifa kuwa kazi kubwa au isiyowezekana.

“Kampuni ya Vodacom kwa sasa inatoa suluhisho kwa wakulima wa pamba na wakulima wa alizeti ambao wana shauku kubwa na fursa hii mpya kutoka Vodacom.

“Teknolojia hizi za kidijitali zinafungua fursa kubwa kwa wakulima wadogo, wawekezaji, na wajasiriamali kuboresha ufanisi wa kilimo cha biashara nchini,” anasema.

‘Connected farmer’ na zana nyingine za kidijitali ni njia za kubadilisha na kuleta maendeleo ya kiuchumi, kijamii na mazingira katika nchi.

Kupitia matumizi ya teknolojia ya simu Vodacom Tanzania inategemea kuchochea zaidi uzalishaji katika sekta ya kilimo ambayo itasaidia Tanzania kufikia malengo yake ya kuwa nchi yenye uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles