26.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 27, 2023

Contact us: [email protected]

Kesi ya ubunge wa Lissu kesho

Kulwa Mzee -Dar es salaam

KESI ya kupinga kuvuliwa ubunge iliyofunguliwa na aliyekuwa mbunge wa zamani wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, inatarajiwa kuanza kusikilizwa kesho.

Hati ya kuwaita pande mbili imetolewa jana na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ikiwaita wahusika kufika katika shauri hilo linalosikilizwa mbele ya Jaji Sirilius Matupa.

Lissu ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), yuko nchini Ubelgiji kwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu ambao hadi sasa hawajajulikana, Septemba 7 mwaka juzi.

Amefungua shauri hilo chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Wakili Alute Mughwai, ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo.

Lissu alifungua shauri la maombi  Mahakama Kuu, Masjala Kuu, Dar es Salaam, dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), akiomba kibali cha kufungua shauri la kupinga uamuzi huo.

Kwa mujibu wa maombi namba 18 ya mwaka 2019, Lissu anaiomba mahakama hiyo impe kibali cha kufungua kesi ili itoe amri ya kumtaka Spika Ndugai ampe (Lissu) taarifa yake ya kumvua ubunge.

Anaiomba mahakama hiyo impe kibali cha kufungua kesi ili iite taarifa ya uamuzi wa Spika wa kumvua ubunge na kisha itengue na kutupilia mbali uamuzi huo.

Mwombaji huyo anaomba mahakama impe kibali afungue shauri ili mahakama itoe amri ya kusimamisha kuapishwa kwa mbunge mteule wa jimbo hilo, Miraji Mtaturu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katika hati ya dharura, Lissu anaiomba mahakama hiyo isikilize na kutoa uamuzi wa maombi yake haraka kwani vinginevyo, Mtaturu ambaye Julai 19, mwaka huu  alitangazwa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, ataapishwa kushika wadhifa huo.

Hivyo anadai atakuwa ameathirika kwa kuwa atapoteza haki zake zote, kinga na masilahi yake yote yanayoambatana na wadhifa wake huo wa ubunge.

Uamuzi wa kumvua ubunge ulitangazwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, Juni 28, mwaka huu wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, huku akitaja sababu mbili.

Spika Ndugai alizitaja sababu hizo kuwa ni kushindwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa muda mrefu bila kumjulisha kwa maandishi mahali aliko na sababu ya pili ikiwa ni kutokuja taarifa za mali na madeni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Hata hivyo, Spika Ndugai alijitetea kuwa si yeye aliyemvua ubunge bali ni katiba ya nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,206FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles