24 C
Dar es Salaam
Sunday, May 19, 2024

Contact us: [email protected]

Ufisadi wagubika Shirika la posta

 Luteni Kanali mstaafu, Dk. Haroun Kondo
Luteni Kanali mstaafu, Dk. Haroun Kondo

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Posta Tanzania (TPC), Luteni Kanali mstaafu, Dk. Haroun Kondo ameamuru mikataba yote iliyoingiwa na shirika hilo ipitiwe upya, baada ya kubaini baadhi ni mibovu.

Mbali na hayo, watumishi wote wa shirika hilo watahakikiwa upya ili kubaini wafanyakazi hewa na waliofanya udanganyifu katika uhakiki wa kwanza.

Dk. Kondo, alisema hayo jana alipokutana na bodi ya wakurugenzi kupitia majukumu waliyopewa baada ya bodi hiyo kuzinduliwa Oktoba, mwaka huu.

“Mashirika ya umma yamejiingiza katika mambo ambayo huwezi kuamini, yamesababisha mashirika kukwama, wazawa wanafanya mambo kama nchi si yao, yanayofanywa na Watanzania yanaogopesha.

“Kitu cha Sh milioni 25 watu wanaandika bilioni, kuna watu wezi Posta, wabadhirifu wanakula fedha, wakubwa waliopewa dhamana ndio tatizo wameifikisha nchi pabaya kazi kulalamika tu.

“Watanzania hawana uoga wanaingia mikataba ya ovyo kila sehemu wanaingiza siasa, waliozoea kufanya mambo ya ovyo, sasa tunasema basi, mashirika yamejaa rushwa na watumishi hewa.

“Ninazo taarifa za Posta tukae tujiangalie tuko wasafi kiasi gani, mashirika yameathiriwa zaidi na watendaji,wengine baada ya kufanya kazi wanazungumza tu hawajulikani wanafanya kazi gani,”alisema.

Dk. Kondo, aliitaka bodi kushirikiana kila mmoja kwa sehemu yake kuhakikisha wako wasafi, yasiwapo mazingira ya kulindana.

“Kuna mikataba mingi mibovu, watu hawana aibu wanasaini, kuna mkataba uliingiwa na TPC Plot namba 416, jengo la ghorofa tatu lililopo jirani na jengo la mawasiliano, kuna kipengele kinaeleza mkataba huo ni wa milele.

“Mikataba mingi wanayoingia hawana uchungu na nchi, mikataba mibovu ipo mingi, naagiza mikataba yote mipya na ya zamani iangaliwe upya, tukibaini ina upungufu tunaikataa,”alisema.

Alisema jengo hilo la ghorofa tatu lina vyumba sita, mpangaji analipa pango kwa mwezi Sh 1,800,000 ambapo kila ghorofa kwa mwezi Sh 600,000.

Alisema pango hilo kwa miaka mitatu mpangaji atakuwa kalipa Sh milioni 64.8, lakini yeye kawasilisha taarifa ukarabati aliofanya katika jengo hilo umegharimu Sh milioni 398.7.

“Kodi ya Sh milioni 1.8 kwa mwaka katika gharama hizo za ukarabati, mteja atakaa miaka 20 bila kulipa kodi ya pango,” alisema na kuongeza kwamba lazima mikataba iangaliwe upya.

Akizungumzia wafanyakazi hewa, alisema katika uhakiki wa awamu wale wenye vyeti feki inadaiwa waliviondoa ili wanusurike.

“Tutaanza kuwafanyia uhakiki upya wafanyakazi wa Posta, Hazina inatoa fedha wafanyakazi hawapo,”alisema.

Alisema kutokana na kukua kwa teknolojia lazima wajifunze kutoka kwa wenzao ambapo wao walikwenda nchini Kenya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles