Na RENATHA KIPAKA-BUKOBA
SERIKALI imetakiwa kuchukua uamuzi wa kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka yaliyosababisha Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kagera (KCU 1990 LTD) kuvunjwa kwa kile kilichoelezwa kuendesha chama hicho kinyume na taratibu za ushirika.
Kauli hiyo ilitolewa juzi mjini hapa na waliokuwa wajumbe wa bodi iliyovunjwa na kuondolewa madarakani na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, mnamo Julai 21, mwaka huu, ambapo wajumbe hao waliongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Frank Muganyizi, nakueleza kutotendewa haki maamuzi hayo.
Walisema pamoja na kuendelea kufanya jitihada za kutakiwa kueleza ukweli kwa Waziri mwenye dhamana, wameonekana dhahiri kutokubaliwa kupewa nafasi ya kujieleza ingawa wahusika moja kwa moja wanaopaswa kuwajibika juu ya shutuma husika wapo na ofisi ya Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini inalitambua hilo.
Akizungumzia suala hilo mwenyekiti huyo wa zamani wa bodi hiyo, alisema uamuzi wa bodi yake kuvunjwa haukuwa wa haki kwani hoja zote zilizoainishwa na Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini, Dk. Audax Rutabanzibwa, zilipaswa kujibiwa na bodi iliyomaliza muda wake.
Alitoa mfano wa moja ya hoja iliyotajwa na Mrajisi ni kushindwa kulipa deni la Benki ya CRDB ambalo bodi iliyomaliza muda wake ilikabidhi bodi mpya deni la Sh bilioni 7.5 lililokuwa likidaiwa na benki hiyo ambapo hadi bodi yake inamaliza kipindi cha mwaka tayari kiasi cha Sh bilioni 4.7 zilikuwa zimelipwa na kubaki na deni la bilioni 2.8 tu.
“Tunatuhumiwa kulipa malipo ya mashaka. Kuingia mikataba isiyozingatia bei ya soko, mradi wa maharage kwa msimu wa 2012/13, zote hizo hoja haziwahusu wajumbe wa bodi yangu, ni hoja zilizokuwepo ambazo ni kutotutendea haki sisi wajumbe wa bodi mpya kutuhoji jambo ambalo hatulijui na waliopaswa kuhojiwa wapo,” alisema.
Pia Mwenyekiti huyo alimtaka Waziri kama anataka kunusuru ushirika awe tayari kuchunguza mambo ya ushirika kwani moja ya wahusika wanaohusika kujibu hoja husika ni Mrajisi wa Vyama vya Ushirika kwa kuwa hata yeye amehusika kulipwa kiasi cha Sh milioni 25 akifanya biashara na KCU huku akitambua kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha maadili ya utumishi wa umma.