PARIS,Ufaransa
SERIKALI ya hapa imesema kwamba inatathmini kurejesha kodi kwa wenye kipato kikubwa, ambayo ilifutwa na Rais Emmanuel Macron baada ya kuingia madarakani.
Uwezekano wa kurejeshwa kwa kodi hiyo maarufu kama ISF iliyokuwa ikitozwa kwa wenye kipato kikubwa nchini umetajwa na Msemaji wa Serikali, Benjamin Griveaux katika mahojiano na kituo cha redio cha RTL.
Hata hivyo msemaji huyo alisema kwamba uamuzi kuhusu hatua hiyo haujawekwa kwenye meza ya mazungumzo na akasema kuwa ikiwa sera fulani haileti ufanisi, serikali sio kiziwi, italibadilisha.
Kufuta kodi hiyo ilikuwa ahadi muhimu ya kampeni ya Rais Macron anayependelea biashara, kama njia ya kurahisisha uwekezaji na kuundwa kwa nafasi za ajira.
Lakini wakosoaji wake, wakiwemo wengi walioshiriki katika maandamano yenye fujo yaliyoandaliwa siku za hivi karibuni na vuguvugu la ‘vizibao vya njano’ katika maeneo mengi ya nchi, wamekuwa wakichukizwa na mtazamo wa Rais Macron, wakimshutumu kuwapuuza wanyonge.
”Ninavyodhani mimi, chanzo cha matatizo yote ni kwamba Macron anawapenda matajiri, anawapenda wenye nguvu, anawahusudu mabosi wakubwa katika taasisi za kifedha. Anapenda matajiri kama alivyosema Hollande, na hawajali watu wa kawaida. Na sio kwamba hawajali tu, bali pia anawadharau, na sababu hiyo ndio imetufikisha hapa.” alisema mwandamanaji mmoja.
Vuguvugu la Vizibao vya njano ambalo lilianzia kwenye jukwaa la kupinga kodi kwenye mafuta ya dizeli iliyopandisha bei ya bidhaa hiyo inayotegemewa na wengi, lilikua na kugeuka malalamiko mapana dhidi ya kupanda kwa gharama ya maisha, na hasira dhidi ya sera za Rais Macron alichukuliwa na wengi kuyafumbia macho masaibu ya watu wa vijijini na miji midogo nchini hapa.
Hapo juzi Waziri Mkuu, Edouard Philippe aliahirisha kwa miezi sita kodi hiyo kwa mafuta ya dizeli, muda ambao alisema utatumiwa kushauriana na wote wanaoathiriwa na kodi hiyo.