24.3 C
Dar es Salaam
Monday, September 16, 2024

Contact us: [email protected]

Udom kufanya tafiti zaidi kutatua changamoto kwenye jamii

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimesema kitaendelea kufanya tafiti zaidi na kuzigeuza kuwa bidhaa zitakazoingia sokoni kwa lengo la kutatua changamoto zilizoko kwenye jamii.

Akizungumza na Waandishi wa habari Mkurugenzi wa Shahada za Awali Udom, Dk. Victor Marealle, amesema wanaamini tafiti hizo zitaifikisha mbali nchi na chuo hicho.

Alikuwa akizungumza baada ya kupokea tuzo ya washindi wa kwanza kwa upande wa taasisi za elimu ya juu nchini kwenye Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba).

Dk. Marealle ambaye alikuwa msimamizi wa banda la chuo hicho kwenye maonesho hayo amesema hawataki kazi za watafiti wao ziishie katika makabati bali wanataka ziende kutatua matatizo halisi ambayo yapo kwenye jamii.

“Udom tunakuja tofauti kidogo, kwanza tunatafiti mahitaji ya ndani na mahitaji ya nje halafu tunatengeneza programu ambazo zinakidhi mazingira yanayotuzunguka, kwahiyo hata tafiti tunazozifanya zinakuwa na matokeo chanya kwenye jamii,” amesema Dk. Marealle.

Aidha amesema tuzo hiyo ni ishara ya kutambulika kwa kazi wanazozifanya kwani walikuja na bunifu za kiteknolojia na baadhi ya bidhaa zilizotokana na tafiti ambazo wanafunzi wanazifanya kwa kushirikiana na walimu.

“Tunapokuwa tunawafundisha wanafunzi wetu hatuishii tu katika nadharia, tunakwenda katika vitendo ambavyo ndiyo vinaweza vikazalisha vitu. Tuzo tuliyopata inathibitisha mambo makubwa tuliyoweza kuyafanya, ni chachu ya sisi kuzidi kupambana zaidi na kutatua matatizo yanayozunguka nchi yetu na kuendeleza tafiti mbalimbali,” amesema Dk. Marealle.

Mkurugenzi huyo amewakaribisha wahitimu wa kidato cha sita na watu wengine wenye sifa kujiunga na chuo hicho kusoma programu mbalimbali kuanzia ngazi ya shahada za awali mpaka uzamivu.

Miongoni mwa tafiti zilizoonyeshwa na chuo hicho katika maonesho hayo zinahusu mchakato wa kurusha satellite itakayosaidia katika masuala ya mawasiliano, vyombo vinavyoweza kusaidia kupunguza ajali, bunifu zinazoweza kusaidia ulishaji wa samaki na kutoa huduma za tiba lishe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles