VICHEKESHO vya makomediani maarufu Bongo, Mussa Yusuph ‘Kitale’ maarufu zaidi kama Mkude Simba na Stan Bakora ni tishio kwa sasa Bongo.
Pengine kinachowabeba zaidi ni staili yao ya kuchekesha ya kujibizana. Kabla ya kujulikana kuwa Mkude Simba ndiye Kitale, komediani wa muda mrefu ambaye amepaishwa na staili yake ya uteja, watu walijua ni ujio wa wasanii wapya kwenye vichekesho.
Ukweli ni kwamba, ulikuwa ujio wa staili mpya ya msanii Kitale, lakini pia ujio wa kipaji kipya kwenye komedi, Stan Bakora.
Ni vichekesho vya kwenye redio, ambapo Radio E-FM ndiyo waliowatambulisha. Sioni haya kusema kuwa, wasanii hawa ni kati ya vionjo vilivyoipaisha redio hiyo na kuwa na mashabiki wengi.
Hakuna aliyemjua Stan Bakora kabla ya E-FM, hata Kitale mwenyewe kama asingejiweka wazi mapema, angebaki na umaarufu mara mbili – angekuwa Mkude Simba na wakati huohuo Kitale.
Angeendelea kutesa kwenye filamu za vichekesho kama Kitale, lakini wakati huohuo akitengeneza maisha kwenye vichekesho vya redio na mitandaoni.
Sanaa ya ucheshi siyo kazi ndogo. Isingekuwa rahisi mtu kumpiku au kumfikia Mzee Majuto au Joti kwenye uigizaji wake. Kama Stan Bakora angekuja na staili ya akina Masanja, asingepata mafanikio aliyonayo leo hii.
Unaweza kuona kwamba staili yao ya tofauti ndiyo iliyowabeba na ni kweli kwamba hawafanani na wasanii wengine hapa Bongo kwenye vichekesho vyao.
Achana na Stan Bakora, yupo komediani mwingine anayekwenda kwa jina la Shaphii Omary maarufu JK. Msanii huyu mwenye uwezo wa kuigiza sauti za watu maarufu wakiwemo viongozi, amepata umaarufu zaidi baada ya kuweza kuiga kwa ustadi sauti ya Rais Mstaafu wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete.
Shaphii aliona mbali. Kabla yake, wapo wakali wa kuiga sauti; kuna Steven Nyerere ambaye anapatia zaidi sauti ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, nyuma yake yupo Mc Babu Ayoub, wote hawa ni wakali wa kupatia sauti za watu maarufu.
SHAPHII ALIVYOJIONGEZA
Alichofanya Shaphii ni kushughulisha ubongo wake kidogo tu; hakuona njia ya kutokea kama angeigiza kilekile kwa staili ileile.
Alichofanya Shaphii ni kuangalia kiongozi mwenye kukubalika zaidi kwa wakati huo, kisha akamchagua kama ‘pacha wake’. JK ni kiongozi mwenye ushawishi mkubwa, anapendwa na watu na ana mvuto.
Komediani huyo, akapitia humohumo. Na kwa kweli JK ana lafudhi fulani nzuri, tamu kusikiliza. Shaphii alivyoamua kumuiga, ikawa ndiyo njia yake ya kutoka kisanii. Asingekuwa na jipya kama angeigiza zaidi kama Hayati Nyerere.
UPENDO, USHIRIKIANO
Wapo baadhi ya wasanii huogopa kuwasaidia wengine wakidhani labda watafunikwa. Ugonjwa huu upo zaidi kwenye Bongo Fleva na Bongo Muvi. Msanii akiona mwenzake ana kipaji, anaogopa kumsapoti akidhani huenda akawa juu zaidi yake.
Hayo ni mawazo ya kimasikini. Waliowaza kimasikini, wamekufa kisanii na hawana jipya. Angalia Kitale alitazama atoke na nani katika staili yake mpya, akamuona Stan Bakora. Wote wamekuwa maarufu. Kila mmoja akila usawa wa kamba yake.
Tunaona mfano mzuri sana kwa msanii Vincent Kigosi ‘Ray’. Huyu ni miongoni mwa wasanii wasiogopa vipaji vipya. Ni Ray ndiye aliyemnoa marehemu Steven Kanumba na hadi anafariki, alikuwa akisema hilo waziwazi.
Ray ni mwalimu wa Kanumba. Wapo wasanii wengi waliopitia mikononi mwa Ray pale Kaole Sanaa Group. Mastaa wengi waliotokea Kaole wanakiri hilo.
Irene Uwoya, hawezi kukataa kuwa kipaji chake kimevumbuliwa na mkongwe Lucy Komba katika filamu yake ya Diversion of Love iliyotoka mwaka 2010.
Kadhalika Wema Sepetu hawezi kusema kwamba hajui mchango wa marehemu Kanumba kwenye uigizaji wake. Kanumba ndiye prodyuza wa kwanza kuona kipaji cha Wema, akamwigiza kambini pale Lamada Hotel, Ilala na kazi nzuri ikazaliwa – A Point of No Return ambayo iliingia mitaani mwaka 2009.
WASANII KAZI KWENU
Kama ambavyo E-FM walikubali vipaji vya Mkude Simba na Stan Bakora, wote wakanufaika kwa kuinuana, ndivyo ambavyo Kitale alikubali kushirikiana na Stan Bakora ambaye alikuwa hajulikani kwenye ulimwengu wa sanaa na wote wapo juu kwa sasa.
Kusaidiana ni kati ya kanuni za mafanikio. Usiogope ushindani. Huwezi kuwa bingwa peke yako, zaidi unapokuwa na mtu wa kukuchallenge.
Zaidi ya kusaidiana wasanii kwa wasanii pia ni vizuri kukumbuka jamii inayoshabikia kazi zenu kwa kushiriki kwenye harambee mbalimbali. Baadhi ya wasanii wanafanya. Najua wapo ambao wanafanya lakini hawajitangazi.
Kwa haraka haraka, nawaona Diamond na hasimu wake mkubwa Ali Kiba wakijitahidi kushiriki kwenye mambo ya kijamii kwa sehemu kubwa. Inaweza miongoni mwa sababu zinazowaweka juu. Kama hujaanza, anza utaona. Hakuna mchawi, ni kujiongeza tu!