27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

UCHAGUZI WA MARUDIO KENYA SHAKANI, UHASAMA UKIONGEZEKA

JOSEPH HIZA, DAR ES SALAAM


WASIWASI na mashaka umezidi kukua iwapo Kenya itaweza kweli kuendesha uchaguzi mpya wa marudio kwa mwezi mmoja uliobakia.

Inatokana na wadau wakuu wa uchaguzi huo kuendelea kuvutana na kushikilia misimamo migumu ya kutokububaliana juu ya namna ya kuuendesha kwa namna inavyotakiwa.

Mbaya zaidi iwapo ikatokea uchaguzi ukafanyika bila utatuzi wa kasoro zinazolalamikiwa iwe wagombea wote wawili kushiriki au kuwa wa upande mmoja utakaposusiwa na mmojawapo hatari ya mustakabali wa baadaye wa taifa hilo au uhalali wa uchaguzi kuhojiwa.

Na iwapo uchaguzi utashindwa kufanyika ndani ya muda unaokubalika, kuna hatari ya kuzuka mgogoro wa kikatiba, ambao utaliweka taifa hili njia panda kisiasa na hata kiusalama.

Hilo likatokea moja ya suluhu pekee itakuwa kuundwa kwa serikali ya kitaifa.

Mkanganyiko iliyotokea tangu Mahakama ya Juu ya Kenya ilipotangaza kufuta matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti 8 yaliyompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta, imezidi kuongezeka badala ya kupungua.

Akitangaza uamuzi huo kufuatia kile Mahakama ya Juu ilichoita kasoro nyingi kinyume na Katiba, Jaji Mkuu David Maraga aliitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutangaza uchaguzi mwingine ndani ya siku 60.

Tume ikatangaza Jumanne ya Oktoba 17 kuwa siku ya uchaguzi huo ukishirikisha wagombea wawili tu wakuu Kenyatta wa Jubilee na Raila Odinga wa muungano wa National Super Alliance (NASA).

Lakini Raila ameapa kuwa atasusia uchaguzi huo iwapo malalamiko yao hayatashughulikiwa na Jumapili iliyopita alisisitiza hilo.

Alizinduan kampeni ya nchi nzima dhidi ya uchaguzi kuendeshwa na timu ya sasa ya IEBC, ambayo anaituhumu ilivuruga uchaguzi wa Agosti 8 kwa kumpendelea Kenyatta.

Hata hivyo, moja ya changamoto kubwa ni kwamba Mahakama ya Juu bado haijatoa hukumu yake yote kamili, ambayo inapaswa kueleza kwa kina sababu za kuamua kufuta ushindi wa Rais Kenyatta.

Ripoti hiyo kamili pamoja na mambo mengine ingeipa picha Tume juu ya namna ya kufanya na kupunguza ugumu unaoikabili sasa kuifanyia mageuzi.

Jaji Maraga alieleza tu ‘kasoro na uharamu’ hasa katika mchakato wa kusambaza na kujumuisha matokeo ya uchaguzi, kitu ambacho kinawapa baadhi ya walioboronga ‘kichwa ngumu’ kutokuwa tayari kung’atuka.

Mahakama ya Juu ina hadi Septemba 22 mwaka huu kutoa hukumu yote, ambayo hata hivyo itaipatia IEBC muda finyu wa kufanyia kazi kasoro tajwa ikiwamo mabadiliko ya lazima ya makamishina.

Haijaeleweka iwapo Mahakama ya Juu itagusia chochote kuhusu mfumo wa teknohama au iwapo watawanyooshea kidole moja kwa moja watu waliohusika kuchakachua matokeo ya kura katika mfumo wa kielektroniki wa IEBC.

Utatoa majibu iwapo kuna kuna uhalali wa kuwaondoa baadhi ya maofisa wa juu au la na iwapo jibu ni ndiyo waondolewe, je muda uliobakia unatosha kuchukua hatua hiyo?”

Kukiwa na ukosefu wa hukumu kamili, ambayo ingetoa mwongozo, IEBC imeendelea na mipango yake ya kuandaa uchaguzi mpya ikipuuza mwito wa upinzani wa kuwafukuza maofisa wa juu wa tume.

Kinachoonekana ndani ya Tume hiyo chini ya uenyekiti wa Wafula Chebukati ni kuogopana, kulindana na kugawanyika kwa misingi siasa za vyama  viwili vinayoidhibiti Kenya.

Awali Chebukati alitangaza mabadiliko ndani ya timu ya kusimamia uchaguzi akiwaondoa maofisa kadhaa akiwamo anayelalamikiwa zaidi na upinzani, Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO), Ezra Chiloba.

Si hivyo, Chebukati aliteua bosi mpya wa kusimamia teknohama, mfumo, ambao ndio chanzo cha kufutwa kwa uchaguzi huo, akimtaka aripoti kwake moja kwa moja badala ya awali kwa CEO.

Hata hivyo, uamuzi wake huo ulipingwa vikali si tu na chama cha Jubilee kilichodai maofisa wapya aliowateua wanafahamika kuipendelea NASA bali pia ulizua mpasuko mkubwa ndani ya tume hiyo yenyewe.

Baadhi ya makamishina waliopinga mabadililo hayo walidai, Chebukati alichukua uamuzi wa kufanya mabadiliko mapya peke yake bila kushauriana nao huku wakimtetea Chiloba.

Hilo likamfanya Chebukati asalimu amri kwa kutengua uamuzi wake huo, kitu kinachoonesha Tume kupasuka baina ya ‘Team Chebukati’ na ‘Team Chiloba’, ambazo pia ni kama vile zimegawanyika baina ya NASA na Jubilee.

Wachambuzi wengi wa mambo wanasema IEBC ilipaswa kuchukua hatua kufanya mabadiliko kwa vile timu iliyopo ilishapoteza uhalali wa kusimamia uchaguzi mpya kufuatia madudu yaliyofanywa nayo.

Aidha wanaulaani mpasuko ndani ya timu na sintofahamu kuelekea Oktoba 17, ambao umeikanganya umma.

Aidha mpasuko ndani ya IEBC ulionekana mara nyingine wakati memo ilipovuja ikionesha Chebukati akimweka kiti moto Chiloba ajieleze juu ya kasoro zilizotokea katika uchaguzi wa Agosti.

Kasoro hizo ni pamoja na kutofanya kazi kwa simu maalumu zenye thamani ya zaidi Sh milioni 800 za Kenya, kudukuliwa kwa mfumo wa teknohama, uwepo wa akaunti ya siri ya Chebukati na kadhalika.

Licha ya hayo, Kenyatta alisisitiza hakuna ulazima wa mabadiliko ya tume na kuwa uchaguzi uendelee kama ulivyopangwa, akimtuhumu Odinga kuwa amelenga kuhakikisha uchaguzi haufanyiki, kama mbinu ya kulazimisha serikali ya mseto.

Lakini NASA imesimamia msimamo wake wa kutoshiriki uchaguzi huo hadi pale  matakwa yake yatakapoafikiwa.

Nasa imekuwa ikitaka baadhi ya makamishna wa tume wakiongozwa na Chiloba wang’atuke kwa tuhuma za kusababisha uchaguzi uliopita kutokuwa wa huru na wa haki.

“Yale masharti tumeweka ili tushiriki uchaguzi sharti yatimizwe. Lazima ufanyike kwa mujibu wa masharti tuliyoweka,” alisema Raila Jumapili iliyopita wakati akiendesha kampeni za muungano wake wa NASA katika viwanja vya Jacaranda, Donholm, Jijini Nairobi.

NASA imemuonya Chiloba kuwa kung’ang’ania kwake ofisini kutamfanya akumbane na kile kilichompata, aliyekuwa mwenyekiti wa Tume hiyo, Isaack Hassan.

Isaack aliyeiongoza IEBC katika Uchaguzi Mkuu wa 2013, aligoma kuondoka ofisini hatua iliyomfanya Raila atumie nguvu ya umma kumuondoa mwenyekiti huyo kutosimamia uchaguzi huu wa 2017.

“Haturudi uwanjani iwapo hatujang’oa visiki, miba na handaki. Tuko tayari kabisa kwa shughuli hiyo pale tutakaposawazisha uwanja na tutamuambia Uhuru Kenyatta aje sasa,” alisema Raila.

Mbali ya makamishina, uchapishaji wa karatasi za kupiga kura pia unaleta utata ambapo Nasa haitaki kampuni ilizozichapisha ya Al-Gurair iliyoko Dubai, ambayo inadai kuwa na uhusiano wa kibiashara na Kenyatta.

Wachambuzi wa mambo wanakubaliana kuwa imani dhidi ya timu ya IEBC imeathirika vibaya na kupoteza uhalali wa kusimamia uchaguzi huo na suluhu ni vyama pinzani kukaa pamoja na kukubaliana njia mwafaka kwa wote.

Hata hivyo, ongezeko la misimamo mikali, kukashifiana na kukebehiana  kumezidisha mpasuko na kufanya ugumu wa kuwakutanisha mafahari hao pamoja.

Mbaya zaidi ni Mahakama ya Juu wakati ikisubiriwa itoe hukumu yote kamili, Jaji wake mkuu Maraga ameitwa ‘mkora’ akitishiwa kushughulikiwa iwapo Kenyatta atashinda.

Aidha Kenyatta ametishia kumng’oa Odinga kupitia wingi wa wabunge wa chama chake iwapo mpinzani wake huyo atashinda uchaguzi wa mwezi ujao.

Kwa mujibu wa Katiba ya Kenya, IEBC ina hadi Oktoba 31 kufanya chaguzi mpya na iwapo itashindwa baada ya tarehe hiyo kuna hatari wa mgogoro wa kikatiba utakauweka nchi njia panda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles