30.3 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

UCHAGUZI TLS: TATIZO SIASA AU LISSU?

NA EVANS MAGEGE,

NI uchaguzi wa aina yake. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kutokana na shauku kubwa waliyonayo wataalamu wa sheria na baadhi ya wananchi wanaofuatilia mwenendo wa masuala ya kisheria nchini.

Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kinatarajia kufanya uchaguzi wa kumpata rais na makamu wa chama hicho Machi 18, mwaka huu.

Kuitishwa kwa uchaguzi huo kunatokana na uongozi uliopo madarakani kumaliza muda wake wa mwaka mmoja kwa mujibu wa taratibu za chama hicho.

Tayari mwenendo wa kuelekea kwenye uchaguzi huo umeanza kugusa hisia za wafuatiliaji wa mambo nchini. Maswali ya nani anayefaa kuiongoza TLS kwa sasa ndiyo yanaonekana kuwa chachu ya hisia hizo.

Majina matano ambayo yamepitishwa kuingia katika nafasi ya kuwania urais wa TLS nayo yanatazamwa kama sehemu ya kuchochea zaidi wafuatiliaji wa mambo ya kisheria kuwa karibu na mwenendo wa uchaguzi huo.

Majina hayo ni Tundu Lissu, Francis Stola, Lawrance Masha, Victoria Mandali na Godwin Mwapongo.

Kimantiki, aina ya wagombea waliojitokeza kuwania nafasi ya urais wa TLS katika uchaguzi wa mwaka huu  nayo inaweza kuwa sehemu ya mvuto unaowahamasisha watu wengi kufuatilia mwenendo wa uchaguzi huyo.

Duru za mambo kutoka ndani ya chama hicho zinabashiri kuwa uchaguzi wa mwaka huu huenda ukawa mgumu ukilinganisha na ule wa mwaka jana.

Mtazamo huo unajengwa na hoja ya aina ya majina ya wagombea wa nafasi ya urais ambapo baadhi yamejijenga katika muktadha wa siasa hususani vyama vya upinzani nchini.

Hata hivyo, mtazamo huo bado unaponzwa kwa uzoefu wa mambo pindi joto la uchaguzi linapozidi kufukuta  kwamba mara nyingi mawakili wanapokutana kwenye uchaguzi huacha kando itikadi za kisiasa, badala yake husimamia masilahi ya taaluma yao.

Yapo mazingira ambayo kwa namna moja ama nyingine yanajipambanua kwamba nyuma ya uchaguzi huo hususani nafasi ya rais na makamu wake kuna ushindani wa kisiasa ambao upo chini kwa chini.

Lissu na Masha ambao ni miongoni mwa wagombea urais, mbali na uwakili ambao unawabeba kuwania nafasi hiyo, pia ni washirika wazuri wa siasa za upinzani na wanaonekana kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa na wajumbe wenye mitazamo ya kisiasa kwa upande wa upinzani.

Kwa upande wa Stola na Mandali, wagombea hao hawavumi au kusikika katika medani za siasa nchini, lakini wanahusishwa kuungwa mkono na kundi la wajumbe wenye mwelekeo wa siasa upande wa chama tawala (CCM).

Ingawa hoja ya siasa haina afya sana katika misingi ya uchaguzi huo, lakini mazingira ya kuhusisha siasa katika uchaguzi huo yanatajwa kumsababisha Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, kutoa kauli nzito yenye mwelekeo wa kutishia kukifuta TLS.

Katika taarifa iliyorushwa na kituo cha televisheni cha Azam two katikati ya wiki hii, ilimkariri Dk. Mwakyembe akisema TLS kimegubikwa na siasa  hivyo atakifuta chama hicho na kupeleka muswada bungeni ili kisajiliwe kuwa chama cha siasa ambacho kitakuwa chini ya msajili wa vyama vya siasa.

Inawezekana Dk. Mwakyembe alitoa kauli hiyo kwa kutambua kinachoendelea nyuma ya pazia hasa joto la kampeni za kuupata uongozi mpya wa TLS.

Kwanini TLS ifutwe?

Kauli ya Dk. Mwakyembe ya kutishia kuifungia TLS kwa sababu ya kugubikwa kisiasa, imeibua maswali mengi miongoni mwa wafuatiliaji wa mambo hususani wasomi na mawakili nchini.

Baadhi wametumia mwanya wa  kuichambua hoja hiyo ya Dk. Mwakyembe kama fursa ya kupigia debe mmoja wa wagombea wa nafasi ya urais wa TLS.

Duru zaidi kutoka ndani ya TLS zinadai kuwa Mwakyembe hana mamlaka ya kukifuta chama hicho kwa sababu kinatambulika kisheria (The Tanganyika Law Society Act).

Kwamba chama hicho kinaweza kufutwa kama Bunge litaridhia muswada wa sheria hiyo ifutwe. Hata hivyo, kama chama hicho kitafutwa mahakama itakuwa imeondolewa sehemu ya nguvu yake.

“The Tanganyika Law Society Act ni sheria mama ya chama chetu, ikitokea ikafutwa, mahakama itafanya kazi na nani? Kwa sababu wakili ni ofisa wa mahakama kama sheria ikafutwa mahakama itakosa mawakili,” anasema wakili mmoja ambaye hakutaka jina lake kuandikwa kwenye makala haya.

Kwa upande mwingine Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo, aliandika ujumbe kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter wenye msingi wa kujibu kauli ya Dk. Mwakyembe.

Ujumbe huo ulisomeka: “ Dk. Mwakyembe amewasaidia sana wajumbe wa TLS kujua kwanini wanapaswa kumchagua @Tundulissu. Nawatakia uchaguzi mwema na TLS imara.”

Nini kimemshtua Dk. Mwakyembe?

Rais wa TLS anayemaliza muda wake alikaririwa na gazeti moja la kila siku (si MTANZANIA) akisema amesikia kauli aliyoitoa Dk. Mwakyembe na wanaendelea kuitafakari kabla ya kuitolea tamko ingawa alitanabaisha kuwa mpaka sasa hakuna dalili au mtu mwenye uhakika kuwa chama hicho kina mwelekeo wa kisiasa.

Akijibu swali iwapo kutatokea madhara yoyote kama Serikali itaamua kukifuta chama hicho alisema: “Sauti ya chama na kazi kubwa tunayoifanya katika jamii haitakuwapo na hatutajua nani ataifanya.

“Tatizo kubwa ambalo limejitokeza naona ni wanachama kutoka vyama vya siasa wenye kadi kugombea, lakini mpaka sasa, TLS hakuna mtu mwenye uhakika kwamba ina mtazamo wa kisiasa,” anasema. 

Kwa upande wake Wakili Peter Kibatala, amekuwa akihoji sababu ya Dk. Mwakyembe, kutishia kukifuta TLS.

Ujumbe aliouandika kupitia mtandao wa kijamii wa What’sApp anasema kauli ya Waziri Mwakyembe inajibiwa kwa hoja nyepesi ya kwamba nini kimemshtua.

Katika maelezo yake, anahoji sababu ya Dk. Mwakyembe kutokuongea wakati Jaji Mkuu mstaafu alipochukuwa fomu za kugombea urais kupitia CCM?

“Ni lini Jaji Agustino Ramadhani alichukuwa kadi ya uanachama wa CCM? Au ni sawa kwa marais wa zamani wa TLS kugombea ubunge kupitia CCM muda mfupi baada ya kuachia nafasi; na ku-create kila impression kwamba alikuwa CCM card –carrying  member?” anaandika Kibatala.

Kibatala anaendelea kuhoji kwamba, Waziri Mwakyembe anafikiri mawakili hawana utashi wa kutofautisha kati ya itikadi za siasa na msingi wa TLS?

Akatanabaisha kuwa mawakili zaidi ya 5,000 wanaweza kuwa wajinga kiasi cha kurubuniwa na itikadi au harakati za kisiasa za vyama?

“Alikuwa wapi yeye kama wakili kutetea tulipotishiwa kuunganishwa katika kesi iwapo tutatetea wateja wetu? Alikuwa wapi kukemea polisi walipokamata mawakili wenzake wakiwa kazini? Waziri Mwakyembe anafikiri ni rahisi kiasi hicho kuifuta TLS kwa kuwa yeye ni waziri? Hafahamu kuna mahakama ambazo yeye hawezi- control na kuna tools kama Judicial Review etc?” anaandika Kibatala.

Anaendelea kuhoji kwamba, Mwakyembe alikuwa wapi kuzungumzia maofisa wa polisi waliostaafu na punde tu wakagombea ubunge kupitia CCM? Tena walikuwa ni mawakili na wanachama wa TLS.

“Mbona hazungumzii neutrality ya Jeshi la Polisi? Vipi kuhusu mwanajeshi aliyeteuliwa nafasi ya juu ya CCM? Watuache TLS tuchague viongozi wetu ili tutimize majukumu yetu ya kisheria,” ameandika Kibatala.

 Wakili, Aidan Katare, naye hoja yake haikuwa tofauti sana na zile alizozitoa wakili Kibatala, katika ujumbe wake aliuandika kwenye mitandao ya kijamii alijipambanua wazi kuwa atampigia kura Tundu Lissu.

Katika maelezo yake juu ya kauli ya Dk. Mwakyembe, wakili Aidan anaandika kuwa kiongozi huyo hana mamlaka ya kufuta Chama cha Wanasheria Tanzania  (TLS).

Naye Wakili Tundu Lissu ambaye ni mmoja wa wagombea wa nafasi ya rais wa chama hicho, aliandika ujumbe usemao kwamba kauli ya Dk. Mwakyembe si ya mara ya kwanza kwa viongozi wa Serikali kutishia kukifuta chama hicho.

“Hii si mara ya kwanza kwa viongozi wa Serikali kutoa vitisho vya kuifuta TLS. Waziri Mkuu hayati Edward Moringe Sokoine, aliwahi kutishia hivyo katika kilele cha vita dhidi ya wahujumu uchumi miaka ya mwanzo ya ‘80. Na hata kabla ya hapo katika miaka ya ‘60 na ’70 watangulizi wake walijaribu kufanya hivyo,” anaandika Lissu.

Anachambua andiko hilo kwa kusema vitisho hivyo vimekuwa vikitolewa kila wakati TLS na private  bar wanapo-assert their independence na wanapoanza kutetea utawala wa sheria na kupinga state lawlessness and impunity of the rulers.

 Lissu anakwenda mbali zaidi katika andiko lake hilo kwa kusema mawakili wakiwa kimya na TLS ikiwa mfukoni mwa Serikali watakuwa darlings wa Serikali.

Aidha, baadhi ya wadadisi wa mambo wanaitazama kauli hiyo ya Dk. Mwakyembe sawa na mtu aliyejificha gizani na akarusha jiwe kwa watu walio kwenye eneo lenye mwanga.

Kwamba kuingia kwa Lissu ndani ya kinyang’anyiro hicho kunatazamwa kama mwanzo wa kusogezwa shuka la siasa za upinzani kwenye chama hicho nyeti kwa utetezi wa haki za raia.

Pamoja na kauli mbalimbali za mawakili hao, swali linabaki kuwa lengo la Dk. Mwakyembe kukifuta chama hicho ni nini hasa? Je, ni hofu ya chama hicho kuongozwa na Lissu kama atachaguliwa au kutokuwa na imani na wanachama wote wa TLS?

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles