25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Ubishani mkali wa sheria kesi ya Nassari

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

MVUTANO mkali wa zaidi ya saa nne umeibuka katika Mahakama Kuu ya Dodoma kati ya mawakili wa pande mbili kuhusu kanuni ya Kudumu ya Bunge kifungu namba 146 (3) kilichomvua ubunge, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari(Chadema).


Shauri hilo lilikuwa kwenye usikilizwaji wa ombi la mbunge huyo juu ya kufungua kesi ya msingi ya kutengua uamuzi wa Spika wa Bunge, Job Ndugai wa kumvua ubunge wake.


Ombi hilo linasikilizwa na Jaji , Latifa Mansour ambako upande wa Jamuhuri uliwakilishwa na mawakili Alesia Mbuya na Masunga Kawahanga kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Pius Mboya kutoka Ofisi ya Bunge.


Upande wa utetezi ulikuwa na mawakili, Hekima Mwasipu na Fred Kalonga.
Shauri hilo namba 22/2019 lilianza kusikilizwa saa 3:15 asubuhi hadi saa 7:15 mchana ambako kesi hiyo iliahirishwa hadi Machi 29 kwa ajili ya kutoa uamuzi wa ombi la mbunge huyo.


Hata hivyo, kabla ya kuahirishwa kesi hiyo kulikuwa na mvutano huo ambao ulitokana na kanuni iliyomvua ubunge ambako upande wa Jamhuri ulidai kuwa Spika Ndugai yupo sahihi huku upande wa utetezi ukidai kuwa kanuni hiyo imekiukwa.


Mawakili wa pande zote walifanya rejea ya kesi mbalimbali za aina hiyo.
Wakili Mbuya wa upande wa Jamhuri alidai Spika yupo sahihi katika uamuzi wake kwa kuwa kanuni inasema mbunge atakoma ubunge asipohudhuria mikutano mitatu ya bunge mfululizo bila taarifa.


Upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Kalonga alisema kabla ya kufikia uamuzi huo, Spika alipaswa kutoa onyo kama kanuni inavyoelekeza lakini hakufanya hivyo na kudai kuwa amekiuka kanuni kwenye uamuzi wake.


Baada ya mvutano wa huo, Jaji Mansour alisema Mahakama hiyo imesikiliza pande zote hivyo uamuzi mdogo wa kesi hiyo utatolewa Machi 29 mwaka huu baada ya kupitia mapingamizi matatu yaliyowasilishwa na upande wa Jamhuri.


Uamuzi huo wa Machi 29, mwaka huu utaamua kama Mbunge huyo wa upinzani ataruhusiswa kufungua kesi ya msingi ama la.


Machi 20, mwaka huu, Mahakama hiyo ilizuia kutofanyika uchaguzi wa Ubunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki hadi shauri la kutoridhishwa na uamuzi wa Spika wa kumvua ubunge Nassari litakapoamuriwa.


Pia Mahakama ilitoa siku saba kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwasilisha majibu ya madai ya Mbunge huyo.


Katika kesi hiyo, Nassari aliomba kibali cha kufungua kesi ya msingi kwa ajili ya kutengua uamuzi wa Spika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles