30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mahakama ya mafisadi yatupa watatu jela miaka miaka mitatu

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imewahukumu kwenda jela miaka mitatu wafanyakazi watatu wa Bandari Kavu ya Azam (ICD) kwa kupatikana na hatia ya kughushi na kusababisha hasara kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

 Watu hao wanadaiwa kuisababishia TRA hasara ya zaidi ya Sh bilioni 12 kwa kutoa makontena 329 bila ya kulipiwa ushuru na malipo mengine

Mahakama hiyo pia imewaachia huru wafanyakazi wawili wa TRA kwa tuhuma zote 110 walizokuwa wameshtakiwa nazo.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jaji Winfrida Korosso baada ya kusikiliza ushahidi wa mashahidi 34 wa upande wa mashtaka na washtakiwa kujitetea wenyewe.

Washtakiwa walioachiwa huru ni aliyekuwa Mchambuzi Mwandamizi wa Masuala ya Biashara TRA, Hamis Omary na Haroun Mpande wa Kitengo cha Mawasiliano ya Kompyuta TRA

Waliotiwa hatiani ni aliyekuwa Meneja wa Operesheni za Usalama na Ulinzi ICD, Raymond Adolf Louis (39) na wenzake Khalid Hassan, mfanyakazi wa Azam na Benson Malembo ambaye ni mfanyakazi wa Region Cargo Services.

Akisoma hukumu hiyo baada ya kuwaachia huru washtakiwa hao wawili, Jaji Korosso alisema mshtakiwa Adolf na Khalid anatiwa hatiani kwa mashtaka ya kughushi kuanzia shtaka la pili hadi 106.

Mshtakiwa Adolf, Khalid na Malembo wanatiwa hatiani kwa   kuisababishia TRA hasara ya Sh 12,618,970,229 iliyotokana na kodi ya makontena 329.

Hata hivyo mahakama hiyo iliwaachia huru washtakiwa wote kwa   kutakatisha fedha baada ya Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka hayo bila kuacha shaka.

“Mahakama ilisikiliza maelezo ya Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka kuhusu washtakiwa kupewa adhabu kali.

“Mahakama pia imesikiliza hoja za mawakili wa washtakiwa kuomba wateja wao wapunguziwe adhabu kwa sababu ni wakosaji wa mara ya kwanza.

“Waliomba wapunguziwe adhabu kwa sababu wateja wao wana familia zinawategemea wakiwamo wazazi wao, wake zao hawana kazi wanawategemea wao, pia mahakama ilizingatia miaka waliyokaa gerezani tangu walipokamatwa.

“Mahakama imezingatia kwamba washtakiwa wamejutia makosa waliyofanya, imezingatia kwamba katika kipindi walichofanya kazi Azam haijaiwahi kutokea tatizo lolote, imezingatia kwamba muda wote wa kesi walikuwa wapole, wanyenyekevu na wamekaa gerezani muda mrefu.

“Mshtakiwa wa kwanza amekaa gerezani miaka mitatu na miezi minne, aliingia Novemba 29 mwaka 2015, mshtakiwa wa pili amekaa akatoka kwa dhamana na mshtakiwa watano alikaa gerezani miaka mitatu na miezi miwili, aliingia gerezani Januari 2016,”alisema Jaji Korosso.

Alisema kwa makosa ya kughushi kuanzia shtaka la pili hadi 106 washtakiwa wa kwanza Adolf na Khalid  atakwenda jela kwa kila kosa miaka mitatu na kwa kosa la kusababisha hasara ya zaidi ya Sh bilioni 12, washtakiwa wote watatu, kila mmoja atatumikia kifungo cha miaka miwili jela.

“Adhabu zote zitakwenda kwa pamoja, kwa mujibu wa sheria ya uhujumu uchumi, washtakiwa wanapotiwa hatiani lazima walipe fidia ya kiasi walichosababisha hasara.

“Mahakama hii inatoa amri kwa washtakiwa wote, watakamaliza kutumikia adhabu zao wailipe TRA nusu ya zaidi ya Sh bilioni 12 ambazo ni Sh 6,309,485,114.5.

Mawakili wa Utetezi, Kung’e Wabeya, Amir Mshana na Gabrieli Kunju waliifahamisha mahakama kwamba wana nia ya kukata rufaa, hawakuridhishwa na hukumu hiyo.

Awali washtakiwa walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kufuta taarifa kwenye kanzi data (data base) kinyume cha sheria ya mtandao, kughushi, kutakatisha fedha, kusababisha hasara ya Sh 12,618,970,229 na kusaidia ukwepaji wa kodi wa kiasi hicho cha fedha.

Matukio hayo yanadaiwa kutokea Julai 11 na Oktoba 28,2015 Dar es Salaam ambako kwa makusudi zilifutwa taarifa katika kanzidata zinazohusu makontena 329 yaliyoingizwa nchini na kupelekwa katika Bandari kavu ya Azam ICD.

Washtakiwa walikuwa wanakabiliwa na mashtaka ya kughushi hati 105 za kutoa makontena kwenye Bandari Kavu ya Azam ICD iliyopo maeneo Sokota na kujaribu kuonyesha yalitolewa kwa halali na TRA Dar es Salaam wakati si kweli.

Wanadaiwa kuwa kati ya Julai 11 na Oktoba 28, 2015 kwa vitendo vyao walisababisha hasara ya Sh 12, 618,970,229 kwa kutoa makontena 329 bila ya kulipia ushuru na malipo mengine.

Kesi hiyo wakati inafunguliwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilikuwa ikimuhusisha pia aliyekuwa Kamishna wa Forodha na Ushuru wa TRA, Tiagi Masamaki ambaye aliachiwa huru Julai 13 mwaka 2017 katika mahakama hiyo ya chini na kuwa miongoni mwa mashahidi 34 walitoa ushahidi katika kesi hiyo Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles