24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

UBINGWA YANGA VPL Hiki ndicho kilichoibeba

6NA SELEMAN SHINENI

YANGA wamefanikiwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), wakiwa wamelala nyumbani kama walivyofanya Leicester City katika Ligi Kuu England.

Katika msimu ambao ulitabiriwa kuwa na upinzani mkali katika hatua ya lala salama, mambo yamebadilika ghafla na Yanga wametwaa ubingwa wakiwa na mechi tatu mkononi.

Pointi tatu walizoporwa Azam kutokana na kumchezesha Erasto Nyoni wakati akiwa na kadi tatu za njano dhidi ya Mbeya City na kichapo cha bao 1-0, ambacho Simba ilikipata kutoka kwa Mwadui juzi, viliihakikishia Yanga ubingwa wakati wakiwa wamelala ndani.

Upinzani wa Simba na Azam haukutosha kuwazuia vijana wa Hans van der Pluijm kutetea ubingwa wa VPL kiulaini, katika msimu ambao ulitabiriwa kuwa na ushindani wa hali ya juu kati ya timu hizo tatu.

Inawezekana hili ni swali ambalo wanajiuliza watu wengi, imekuaje Yanga imetwaa ubingwa mapema hivyo licha ya upinzani mkubwa wa Simba na Azam? Makala haya yatakupa jibu la swali hili!

Ukubwa wa kikosi

Yanga imeingia msimu huu ikiwa inajivunia kuwa na kikosi kikubwa kitu ambacho kimeisaidia timu hiyo kuendelea kufanya vizuri hata pale ambapo wachezaji wake wa kutumainiwa wanapokosekana.

Ndio maana hata timu hiyo ilipokuwa na mechi mfululizo (Kombe la Shirikisho, Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika), bado iliweza kuendelea kufanya vizuri kwa sababu ilikuwa ikiwachezesha wachezaji wake kwa zamu na kuwapa muda wa kupumzika.

Ukiangalia benchi la Yanga wachezaji kama akina Malimi Busungu, Paul Nonga, Geofrey Mwashiuya, Matheo Anthony, Pato Ngonyani wana uwezo wa kucheza kikosi cha kwanza kwenye klabu yoyote ya VPL.

Imeonekana msimu huu hata pale Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alipokuwa majeruhi bado ukuta wa Yanga ulikuwa imara kutokana na uwepo wa Vincent Bossou, wakati golini Deogratius Munishi ‘Dida’ na Ally Mustapha ‘Barthez’ wote wana uwezo mkubwa na yeyote anayekosekana kumekuwa hakuna pengo golini.

Majanga Msimbazi

Licha ya Simba kujaribu kupambana msimu huu, lakini bado majanga yaliendelea kuiandama klabu hiyo ya Msimbazi ambayo ilianza msimu ikiwa chini ya Dylan Kerr ambaye alitimuliwa na nafasi yake kuchukuliwa na Jackson Mayanja.

Chini ya Mayanja, mara kwa mara Simba imejikuta kwenye mgogoro mzito kati ya kocha huyo na wachezaji wake, kitu ambacho kwa kiasi kikubwa kimechangia kupoteza morali ya timu kufanya vizuri, huku taarifa za Mohamed Dewji ‘Mo’ kutaka kuinunua timu hiyo zikitengeneza makundi ndani ya klabu na kuifanya ishindwe kupambana katika mbio za ubingwa.

Kushinda viporo

Kama kuna mtihani Yanga walikuwa nao ni ule wa mechi za viporo, kutokana na kushiriki michuano ya kimataifa vijana wa Pluijm walijikuta wakiandamwa na viporo kadhaa, ambavyo kama wangetetereka kidogo vingewaharibia kwenye mbio za ubingwa.

Wakati Azam wakipoteza pointi kadhaa za viporo, Yanga ilifanikiwa kushinda mechi zake zote na kuitoa Simba kileleni, licha ya kukabiliwa na mechi mfululizo na ushindi huu wa viporo ndiyo uliongeza morali ya miamba hiyo ya Jangwani kuwania taji la Ligi Kuu.

Ubora wa benchi la ufundi

Ubora wa benchi la ufundi la Yanga chini ya kocha Hans van der Pluijm, umechangia kwa kiasi kikubwa timu hiyo kutwaa taji mapema msimu huu, kutokana na kuweza kutengeneza kikosi imara huku wachezaji wote wakiwa na furaha hata wale wanaokaa benchi.

Mbali na Pluijm, benchi la ufundi la Yanga lina mtu kama Juma Mwambusi ambaye ubora wake ulionekana wazi wakati akiwa Mbeya City, sambamba na kocha wa makipa, Juma Pondamali ambaye ni mmoja wa makocha bora zaidi wa makipa nchini.

Usajili bora

Ukiacha usajili wa Mniger, Issoufou Boubacar Garba ambaye ni wazi kuwa Yanga walilishwa ‘tango pori’, usajili wa Yanga msimu huu umekuwa bora sana na umesaidia kuimarisha kikosi hicho kutoka kile ambacho kilitwaa taji la Ligi Kuu msimu uliopita.

Wazimbabwe, Donald Ngoma na Thabani Kamusoko, wamekuwa wachezaji muhimu zaidi kwenye kikosi cha Yanga tangu watue Jangwani kutoka FC Platinum, huku staa mwingine wa kimataifa kutoka Togo, Vincent Bossou, naye akigeuka kuwa kiongozi kwenye kikosi cha Yanga.

Donald Ngoma

Kama kuna mchezaji ambaye amekuwa mwiba sana kwenye beki za timu pinzani kwenye kikosi cha Yanga msimu huu basi ni Ngoma, ambaye mara kwa mara amewasababishia kadi nyekundu wapinzani kutokana na soka lake la upambanaji akiwa uwanjani.

Katika mechi ambazo Yanga imeshindwa kucheza kabisa msimu huu, Ngoma peke yake amekuwa akiibeba timu hiyo na kubadili matokeo sehemu ambayo wenzake wanaonekana kukata tamaa na uwepo wake kwenye kikosi umechangia kwa kiasi kikubwa timu hiyo kutwaa taji mapema msimu huu.

Amani klabuni

Licha ya sakata la kujiuzulu kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Yanga, Dk. Jonas Tiboroha na figisu figisu za uchaguzi kwa ujumla, klabu hiyo ya Jangwani imekuwa na amani ya hali ya juu ambayo imesababisha umoja klabuni na kuifanya timu hiyo itwae taji mapema sana.

Kutetereka kwa Azam

Azam ni moja kati ya timu ambazo zilitarajiwa kutoa upinzani mkubwa kwa Yanga msimu huu, lakini kitendo cha kutetereka kwake wakati ilipokuwa inakabiliwa na mechi za viporo, kulitoa mwanya kwa vijana wa Pluijm kuongeza pengo la pointi kati yake na vijana hao wa Stewart Hall.

Na pigo kubwa zaidi kwa Azam kwenye mbio za ubingwa lilikuja baada ya timu hiyo kuporwa pointi kwa kumchezesha Nyoni wakati akiwa na adhabu na hiyo ndiyo sababu kubwa Yanga imefanikiwa kutangaza ubingwa ikiwa imelala nyumbani kama Leicester City.

Ushindi nje ndani dhidi ya Simba

Inawezekana ikiwa ni mechi nyingine tu kwenye ligi, lakini siku zote matokeo kwenye mechi ya Yanga na Simba huwa yana mchango mkubwa sana kwenye mbio za ubingwa kutokana na ukweli kuwa wakati mwingine matokeo ya mechi hii husababisha migogoro klabuni.

Hivyo kitendo cha Yanga kushinda mechi zote mbili dhidi ya Simba, kiliongeza kujiamini na amani kwenye klabu hiyo ya Jangwani na pia kilitengeneza pengo la pointi sita kati yao, hii ni kutokana na kushinda mechi zote nyumbani na ugenini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles