26.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 8, 2024

Contact us: [email protected]

UBINAFSHAJI WA KUSHINIKIZWA ULIPORA WAZAWA RASILIMALI

Na, ALOYCE NDELEIO


VIJANA  katika maeneo ya nchi zilizo na kipato cha chini wamekuwa na aibu ya kufanya kazi za kilimo kutokana na taswira iliyojengeka kuwa shughuli hiyo ina tija ndogo.

Hali hiyo inamaanisha kuwa vijana wanakuwa wamekosa fursa za kazi nzuri na wanashindwa kuzifikia  huduma na ulinzi wa kijamii hatua  inayowafanya kuungana na uhamiaji wa ndani na  hata kuzamia katika nchi nyingine na kuwa wahamiaji wa kimataifa.

Hali hiyo inayafanya baadhi ya maeneo kubakiwa na wanawake  na wazee wakiwa wanajishughulisha na kilimo wakiwa wanakabiliwa na vikwazo vikubwa katika kuzifikia rasilimali za kuboresha uzalishaji wao. Hali ya aina hiyo imekuwa ni moja ya changamoto  za kuleta mabadiliko vijijini  na hata kuunganisha  vijiji  na miji.

Hali hiyo ndio imekuwa  ikielezwa na wanasiasa kuwa  ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana  kuwa ni bomu linalosubiriwa kulipuka, lakini kiuhalisia ni kwamba  bomu hilo linaweza  kuzuiwa  lisilipuke kwa kulitengua.

Kufanikiwa katika hali ya aina hiyo kuliwahi kuwekwa wazi na Rais wa Ivory Coast, Allasane Ouattara katika Mkutano wa Magavana wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB).

Alisema, “Lazima (vijana) wasaidiwe na wawekewe mazingira bora ya kupata fursa za ajira na kujiajiri, bila kufanya hivyo ni kukaribisha matatizo na machafuko yanayotokana na ongezeko la mahitaji na kukata tamaa katika miji yetu inayokua kila kukicha kutokana na ongezeko la vijana wanaosaka ajira na maisha bora.”

Ukweli unabakia kuwa viwanda ndio nyenzo ya ajira kwa makundi yote ya jamii na rejea nzuri ni wakati  wa uongozi wa Awamu ya Kwanza ambapo ajira nyingi  zilikuwa zinapatikana kwenye viwanda  ambavyo vilikuwa vingi na vikitumia malighafi za ndani  ambazo ni pamoja na mazao yaliyokuwa yanazalishwa ndani ya nchi.

Aidha viwanda vingi vilijengwa na Serikali kwa msaada wa nchi marafiki miongoni mwa nchi hizo ni pamoja na China ambayo ilijenga Kiwanda cha Nguo cha Urafiki na vingine vilitaifishwa  kutoka mikononi mwa wageni walikuwa na mrengo wa kunyonya wananchi.

Hatua hiyo ilifanyika enzi za ujamaa na hata hivyo kutokana na mageuzi yaliyoikumba dunia viwanda vingi vilibinafsishwa baadaye katika mazingira ambayo hadi sasa yanazua ulalamishi na hivyo watu walio wengi kukosa ajira.

Tofauti na Tanzania viwanda vingi vya China vilivyokuwa vinamilikiwa na dola ya kijamaa enzi za Mwenyekiti  Mao Tse Tung hivi sasa vinamilikiwa na wafanyabiashara binafsi wa Kichina wakishirikiana na wabia toka nchi zilizoendelea hususani Japan, Korea ya Kusini, Ulaya na Marekani.

Wachina wao wamebadili sera za kijamaa lakini kabla ya kufanya hivyo walihakikisha ubinafsishaji unarudisha rasilimali za Taifa (umma) toka kwenye umiliki wa dola na kwenda katika umiliki wa Wachina binafsi na sio umiliki wa wawekezaji wa kigeni.

Wawekezaji wa nje waliuziwa sehemu ya hisa tu za mali za umma ili wavutiwe kuleta mitaji na maarifa mapya katika uzalishaji viwandani.

Hali kadhalika Wachina hawakufanya ubinafsishaji kutokana na shinikizo la wafadhili wa nje bali kutokana na utashi wao wenyewe baada  ya kubaini kwamba sera za kijamaa hazitaweza tena kuleta maendeleo ya kiuchumi kwa kasi kubwa katika mfumo wa sasa wa uchumi wa dunia.

Kwa bahati mbaya Tanzania haikuweza kubinafsisha rasilimali za Taifa kwa Watanzania binafsi kwa sababu Serikali ilikuwa inashinikizwa kutekeleza masharti ya wafadhili wa nje haraka kabla ya kutafakari kwa kina. Wafadhili hao ndio wanataka wawekezaji wa kigeni wamiliki uchumi.

Hata hivyo walipotokeza baadhi ya Watanzania kutaka kununua baadhi ya mali hizo  wengi walipigwa danadana na hivyo uwekezaji ukawa umejaa taswira ya kuwa ni shughuli inayoweza kufanywa na watu kutoka nje na wazawa kutupwa pembezoni.

Hilo limekuwa linashamirishwa na viongozi walio wengi kwa kuwaalika wawekezaji wa nje zaidi na kuwasahau wazawa.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Ahsante kwa kutufunza, Je viongozi wetu wanakuelewa. Bado wanawaleta na kuwaomba wawekezaji. Je kwa nini Watanzania toka vijijini wakawa huru kujipangia nini wanataka kifanyike badala ya mawaziri kuja kuwalazimisha wananchi wakubali mipango yao ya kutoka Dodoma . Wakijua wazi ni mali za Watanzania huko waliko na si ya Wakuu toka Dodoma. na kwa upande wa uwekezajiWajichagulie wenyewe na waende ubia na wawekezaji. Serikali kazi yake kusaidia kutoa elimu ili Wananchi wanufaike, na itanufaika kwa kukusanya kodi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles