23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

SAMORA MACHAEL: SHUJAA WA MSUMBIJI ANAYEAMINIKA KUUAWA NA MAKABURU

 Joseph Hiza, Dar es Salaam


ILIKUWA Oktoba 20, 1986 siku ambayo haitasahaulika katika nyoyo za raia wengi wa Msumbiji na Afrika hasa katika nchi zilizokuwa mstali wa mbele katika ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika, Tanzania ikiwamo.

Ni siku, ambayo Samora Machel, Rais wa Kwanza wa Msumbiji na maofisa wengine 33 walikuwa angani wakitokea Zambia kurudi Msumbiji wakati ndege yao ya Kisovieti aina ya Tupolev ilipoanguka nchini Afrika Kusini.

Utawala wa Afrika Kusini wa wakati huo wa Wazungu wachache na washirika wao wa Magharibi ulidai kuwa ajali hiyo ilitokana na uzembe wa wafanyakazi wa ndege hiyo.

Lakini Msumbiji, Urusi na mataifa mengine mengi ya Afrika, yaliamini kabisa ilikuwa ya kupangwa na uchunguzi ulibainisha hilo.

Msumbiji pia ilikumbushia vitisho vya utawala huo kandamizi dhidi ya maisha ya Machel, vilivyotolewa na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Makaburu Magnus Malan, mapema Oktoba 1986.

Maudhui ya vitisho hivyo kiasi cha kuunganishwa na kifo cha Machel yanatokana na hatua za kidiplomasia zilizokuwa zikifanywa na nchi za mstali wa mbele kujaribu kuitenga Afrika Kusini na washirika wake waliobakia katika eneo hilo hasa madikteta Kamuzu Banda wa Malawi, na Mobuto Sese Seko wa Zaire (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Oktoba 19, 1986, kama sehemu ya harakati hizo, Machel alisafiri kwenda kuhudhuria mkutano katika mji wa Mbala nchini Zambia.

Machel, na marais wa Zambia, Kenneth Kaunda, na Angola, Jose Eduardo dos Santos, wiki moja kabla katika mkutano uliofanyika mjini Maputo, viongozi hao walikuwa wamepewa jukumu na viongozi wenzao wa Mstari wa Mbele, akiwamo Baba wa Taifa la Tanzania, Marehemu Mwalimu Julius Kambarage  Nyerere.

Katika jukumu hilo walitakiwa kuzungumza moja kwa moja na kujaribu kumshawishi Mobutu aachane na utawala wa Makaburu pamoja na kuwasaidia waasi.

Ikumbukwe kipindi hicho, Zaire ilikuwa ikitoa misaada kwa waasi wa UNITA nchini Angola, ambao walikuwa wakishirikiana na utawala wa kikoloni.

Lakini wakati ndege hiyo ya Urusi ikirudi kutoka Mbala, iliachia njia yake na hivyo kuanguka vibaya katika vilima vya Mbuzini, nchini Afrika Kusini mpakani na Msumbiji.

Uchunguzi uliofanywa na wataalamu wa Urusi wakishirikiana na Msumbiji ulibainisha kuwa hiyo haikuwa ajali bali ndege ilihadaiwa na kituo cha uongozaji ndege mpakani cha Makaburu na hivyo kuifanya iachie njia na kuanguka.

Baada ya Afrika Kusini kuachana na sera za kibaguzi zilizoshuhudia utawala wa walio wengi mwaka 1994 chini ya Kiongozi wa Kwanza Mweusi Nelson Mandela ambaye amemuoa Graca Machel, mjane wa Samora, iliundwa tume ya usuluhishi na maridhiano ambayo pia ilichunguza suala hilo.

Kabla ya uchunguzi kukamilika, nyaraka zilionesha kuwapo ushahidi unaohusisha ajali hiyo na uliokuwa utawala huo wa makaburu.

Na hilo lilimfanya hivi karibuni Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma kuamuru kufanyika upya kwa  uchunguzi kuhusu ajali hiyo utakaoendeshwa na kikosi maalumu cha polisi kijulikanacho kama Mwewe.

Hata hivyo, tangu Zuma aamuru uchunguzi huo mwaka 2012, hakuna dalili za chanzo kamili cha ajali hiyo wakati huu ambao Samora anaelekea kutimiza miaka 32 tangu kifo hicho hapo Oktoba 26, 2018.

 

Samora alizaliwa katika Kijiji cha Madragoa sasa Chilembene, katika Jimbo la Gaza, katika iliyokuwa Ureno ya Afrika Mashariki (Msumbiji), akitokea katika familia ya wakulima wa kabila la Shangana.

 

Chini ya utawala wa Ureno, babu yake, alilazimishwa kukubali kuuza mazao yake kwa bei ya chee kuliko ile wanayolipa wakulima wa Kizungu.

 

Aidha alilazimishwa kulima zao la pamba, ambalo lilimpotezea muda kulinganisha na mazao ya chakula yaliyohitajika na familia yake na alipigwa marufuku kuwawekea alama ng’ombe wake kuzuia wezi.

 

Hata hivyo, baba wa Machel alikuwa mkulima mwenye mafanikio: alimiliki majembe manne ya kukokotwa na ng’ombe na ng’ombe 400 kufikia mwaka 1940.

 

Machel alikulia katika kijiji hicho na alihudhuria katika shule ya misheni na mwaka 1942, alipelekwa katika shule ya mji wa Zonguene katika jimbo hilo hilo la Gaza.

 

Shule hiyo iliendeshwa na Wamisheni wa Kikatoliki ambao waliwafundisha watoto lugha ya Kireno na utamaduni wake.

 

Ijapokuwa alihitimu darasa la nne, Machel kamwe hakuweza kukamilisha elimu yake ya sekondari.

 

Hata hivyo, alikuwa na cheti kilichomwezesha kusomea uuguzi popote pale nchini Ureno, kwa sababu shule za uuguzi hazikuwa zikitoa shahada.

 

Machel alianza kusomea uuguzi moja ya kazi chache ambazo weusi waliruhusiwa kuzifanya katika jiji la Lourenço Marques (sasa Maputo), kuanzia mwaka 1954.

Kama ilivyo kwa weusi wengi, katika miaka ya 1950, katika eneo la jamii yao ya wakulima katika mto Limpopo, alishuhudia unyonyaji wa wazungu, akiona jinsi ardhi yote yenye rutuba ikiwa chini ya serikali ya kikoloni ya jimbo na walowezi wa kizungu ambao walitengeneza miundo mbinu mipya eneo hilo.

 

Na kama ilivyokuwa kwa wengi wao, baadhi ya ndugu na jamaa zake walienda kufanya kazi katika migodi ya Afrika Kusini ambako fursa ya kazi zilipatikana.

 

Muda mfupi baadaye, mmoja wa kaka zake aliuawa katika ajali mgodini.

 

Akiwa ameshindwa kukamilisha mafunzo rasmi ya uuguzi katika Hospitali ya Miguel Bombarda mjini Lourenço Marques, alipata kazi kama msaidizi katika hospitali hiyo hiyo ili apate kiasi cha kutosha kujilipia masomo ya usiku.

 

Alifanya kazi katika hospitali hiyo hadi alipoondoka nchini humo kwenda kujiunga na wazalendo wa Msumbiji walioendesha harakati za ukombozi katika nchi jirani ya Tanzania.

 

Kabla ya hapo aliendesha migomo kupinga kitendo cha hospitali hiyo kubagua weusi ikiwamo mishahara midogo kulinganisha na wazungu.

 

Awali kabla ya kutimkia Tanzania ziara ya msomi Eduardo Mondlane katika miji ya Lourenco Marques na Gaza mwaka 1961 ilileta mabadiliko mapya kwa Mondlane na wengine wengi.

 

Samora Machel, akiwa miongoni mwao alimtaka Mondlane kujikita katika harakati za ukombozi wa nchi yao.

Tangu mwishoni mwa miaka ya 1950 raia wengi wa Msumbiji waliondoka nchini humo kwenda nje  kuendesha harakati hizo.

 

Mondlane alikubali changamoto za kuwaunganisha wenzake.

Juni 1962 Mondlane alikubali mwaliko wa Nyerere kukusanya na kuunganisha makundi ya wapigania uhuru wa Msumbiji  yaliyotapakaa mjini Dar es Salaam.

 

Viongozi wa makundi hayo walikubaliana kuunda vuguvugu la Front for the Liberation of Mozambique (Frelimo) chini ya uongozi wa Mondlane.

 

Baada ya hapo mlolongo wa raia wa Msumbiji wanaovuka mpaka kuingia Tanzania kwa ajili ya kubeba silaha ukashamiri.

 

Kufikia Agosti 1963 Samora Machel akaelekea Tanzania kuungana na harakati hizo za msituni.

 

Machel alikuwa miongoni mwa kundi la kwanza la wapiganaji wa Frelimo waliopelekwa Algeria kwa mafunzo ya kivita.

Baada ya kukamilisha mafunzo Machel alirudi  Tanzania akiwa kama mkufunzi katika kambi ya mafunzo ya kijeshi ya Frelimo huko Kongwa.

 

Kufikia Septemba 25, 1964, wakati Frelimo ilipoanzisha harakati za ukombozi wapiganaji 250 walikuwa wamefunzu vyema. Machel aliratibu mkakati wa msitu katika kampeni za Niassa.

 

Miaka miwili baadaye baada ya kifo cha Waziri wa Ulinzi wa Frelimo Filipe Magaia, Machel akachukua nafasi hiyo kisha akawa mnadhimu mkuu wa jeshi, nafasi aliyoishika kipindo chote cha vita.

 

Sifa zake za kimikakati, kisiasa na kijamii na uwezo wake kama askari mkakamavu na mwenye uwezo wa kushawishi na uuunganisha wenzake ulimpatia sifa nyingi na kukubalika miongoni mwa makada wenzake.

Pia aliaminiwa na kuheshimiwa na Rais wa Frelimo Mondlane.

Februari 3, 1969, Mondlane akauawa kwa bomu lililoweka katika kifurushi.

Aprili 1969 baraza la kirais likachaguliwa likihusisha Uria Simango (makamu wa zamani wa rais), Samora Machel, na Marcelino dos Santos (aliyekuwa waziri wa mambo ya nje).

Novemba 1969 Simango alisimamishwa na baraza hilo  na Februari 1970 akatimuliwa kutoka Tanzania. Machel akawa kaimu rais huku dos Santos makamu wake.

Katika kikao kilichofuata cha kamati kuu ya chama, nyadhifa zao hizo zikathibitishwa rasmi na Simango alitimuliwa moja kwa moja kutoka chama hicho.

 

Machel, aliendelea na harakati za kupigania uhuru huku akiwa bega kwa bega na Josina Abiatar Muthemba Machel.

Wawili hao walioana Mei 1969.

Awali Josina Muthemba Machel alijaribu kukimbilia Tanzania kuungana na Frelimo Machi 1964, lakini alikamatwa na kufungwa na Wareno kabla ya kufanikiwa na kutokomea Tanzania Agosti 1965.

Shujaa huyo anayekumbukwa hadi leo nchini humo alikuwa akiongoza vikosi mbalimbali vya wanawake.

 

Hata hivyo, akiwa msituni afya yake ilianza kuzorota na akahamishiwa katika hospitali mjini Dar es Salaam ambako alifariki dunia Aprili 7, 1971.

 

Mwaka 1975, Samora akamwoa Graca Simbine, pia mpiganaji wa Frelimo ambaye baada ya uhuru aliteuliwa kuwa waziri wa elimu na ambaye sasa ni mke Mandela.

Chini ya uongozi wa Machel na Frelimo, Msumbiji  ikapata uhuru wake kutoka kwa Wareno Juni 25, 1975.

Machel akiwa madarakani alichukua maamuzi mbalimbali yakiwamo yaliyouchukiza utawala wa makaburu na aliiwekea nchi hiyo vikwazo bila kujali kama viliathiri uchumi wa Msumbiji huku akisaidia wazalendo wa Afrika Kusini waliokuwa katika harakati mbalimbali za kupambana na ukandamizi wa Makaburu.

Akiwa bado anahitajika na wananchi wake na Afrika kwa ujumla akafariki katika ajali ya ndege Oktoba 20, 1986, nafasi yake ikachukuliwa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje Joaquin Chissano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles