NA MARTIN MAZUGWA
MOJA kati ya michezo inayozidi kupoteza mwelekeo kila kukicha hapa nchini ni mchezo wa ngumi hasa za kulipwa, ambapo mabondia wengi wamekuwa wakitupia lawama mapromota wa mchezo huo kuwa hawawatendei haki.
Miaka inavyozidi kwenda, ndivyo mchezo wa ngumi unavyoendelea kupungua thamani sababu kubwa ni ubabaishaji wa viongozi waliopewa dhamana ya kuuongoza mchezo huo hapa nchini.
Imekuwa kawaida kusikia malumbano, mara baada ya mapambano kuisha kati ya mabondia na mapromota wa mchezo huo hapa nchini, jambo ambalo linajenga taswira mbaya katika ulimwengu wa ngumi.
Mchezo huu umeanza kupotea mwelekeo kutokana na usimamizi mbovu uliopo katika vyama vinavyousimamia, kukosekana kwa umakini wa kuusimamia imepelekea kuwa kawaida kusikia kilio cha mabondia kudhulumiwa.
Ngumi zimepoteza mvuto tofauti na enzi za wakongwe kama Rashid Matumla, Maneno Osward ‘Mtambo wa Gongo’ na wengine wengi ambao wameliletea Taifa sifa kubwa katika mapambano ya ndani na nje ya nchi.
Wakali hawa waliipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika mataifa mbalimbali duniani kutokana na ubora wao.
Mabondia wamekuwa wakilalamika kila siku kuhusu kunyonywa na mapromota ambao wamekuwa wakiangalia faida zaidi kwa upande wao na kuwafanya mabondia kukosa haki zao.
Mwaka jana moja kati ya pambano lililokuwa likisubiriwa kwa hamu kubwa na wapenzi wa ngumi hapa nchini, ilikuwa baina ya Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’ dhidi ya Francis Cheka, lililotakiwa kufanyika katika ukumbi wa PTA usiku wa Krismasi, lakini ilishindikana kutokana na kutokamilika kwa malipo kati ya Cheka na promota, Siraji Kaike.
Jambo hilo liliibua hisia kwa wapenzi wa ngumi, huku wapenzi wa mchezo wa masumbwi wakitoa malalamiko juu ya pambano hilo kushindwa kufanyika.
Wengi walimlaumu Cheka kwa kitendo cha kuonyesha msimamo wake, huku wengine wakimpongeza kwa kuonyesha kujali masilahi yake.
Jambo ambalo lilitoa taswira mbili, moja ikiwa mbaya kwa upande wa promota na nzuri kwa mabondia jambo lililoibua mzozo uliopo katika mchezo huo unaopendwa ulimwenguni.
Kwa hali hii mabondia wa hapa nchini wanapaswa kujitambua na kuwa makini kuangalia watu wa kufanya nao kazi, inatakiwa waache kuishi kwa mazoea kama miaka ya nyuma.
Mabondia hasa wa ngumi za kulipwa, wanapaswa kuipitia vizuri mikataba wanayoingia na mapromota wa mchezo huo ambao wengi wao ni wajanja.
Bado safari yetu ni ndefu ya kuhakikisha mabondia wetu hapa nchini wanafika mbali, ambapo licha ya mchezo huo kutopewa nafasi kubwa lakini wamekuwa wakijitahidi kuipeperusha vyema bendera ya taifa katika mapambano mbalimbali.
Ifike wakati mapromota wa mchezo wa ngumi za kulipwa hapa nchini, kuacha ubabaishaji, mchezo huu unakoelekea si kuzuri kwani kadiri siku zinavyokwenda, ndivyo unavyozidi kuporomoka na kupoteza hadhi.