Khamis Sharif -Zanzibar
MAKARANI wa uandikishaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura katika wametakiwa kufuata kanuni, sheria na miongozo ya uchaguzi ili kutoa huduma bora wakati uandikishaji na uhakiki wa taarifa za wapigakura katika majimbo mbalimbali ya mikoa ya Unguja.
Akifungua mafunzo ya siku moja kwa makarani hao mjini Unguja, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Thabit Idarous Faina, alisema matarajio ya tume ni kuandikisha idadi kubwa ya wananchi waliokosa fursa hiyo awali hivyo ni vyema makarani wakawa makini pale wanapotekeleza majukumu yao.
Alisema kwa kuwa tume inadhamira ya kuandikisha kila mwenye sifa atakayefika kituoni ni vyema makarani hao wakanyakazi kwa bidi ili kufikia dhamira hiyo ili Wazanzibari waliwengi washiriki katika hatua zote za mchakato wa uchaguzi.
Faina alisema tume imekamilisha kazi ya uandikishaji na uhakiki wa taarifa za wapiga kwa mikoa yote ya Pemba.
Alisema kukamilika kwa kazi ya uandikishaji na uhakiki wa taarifa za wapiga kura ni hatua muhimu ambayo itaiwezesha tume kuweka wazi daftari, kugawa vitambulisho vya kupigia kura na kukamilisha kazi ya Uchaguzi Mkuu 2020.
Akiwasilisha mada juu ya utaratibu na miongozo ya kazi ya uandikishaji, Mkuu wa Kurugenzi ya Mifumo ya Uchaguzi wa ZEC, Mwanakombo Machano Abuu, alisema kazi ya uandikishaji itafanyika kwa siku mbili kwa kila kituo cha uandikishaji na kuwataka kuzifanyia kazi changamoto zilizojitokeza katika zoezi la awali.
Baadhi ya makarani wa uandikishaji waliahidi kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi zaidi sambamba na kuwataka wananchi wenye sifa za kuwemo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kutodharau fursa hiyo ambayo itawapa haki ya kushiriki katika Uchaguzi Mkuu 2020.