NYOTA wa ngumi duniani, Tyson Fury, inawezekana akapoteza leseni yake ya ngumi kutokana na kukubali kuwa alikuwa anatumia dawa aina ya cocaine.
Bondia huyo kwa sasa anasumbuliwa na matatizo ya akili ambapo inadaiwa kuwa matatizo hayo yanatokana na matumizi ya madawa hayo.
Hata hivyo, Fury amekiri kuwa alikuwa anatumia dawa hizo kwa ajili ya kupunguza mawazo aliyonayo kwa sasa. “Nimekuwa nikitumia dawa za cocaine kwa kuwa nachoshwa na maisha ya sasa na ni bora nifanye hivyo ili niwe na amani,” alisema Fury.
Kutokana na hali hiyo, bodi ya ngumi inatarajia kukutana wiki ijayo kwa ajili ya kujadili suala la Fury, hivyo kwa mujibu wa Mtendaji wa British Boxing Board of Control (BBBofC), Robert Smith, amedai kuwa kuna uwezekano mkubwa bondia huyo atapokonywa leseni yake.
“Bodi inatarajia kukutana wiki ijayo Oktoba 12, ninaamini kila kitu kitakuwa sawa kutokana na maamuzi ambayo yatafikiwa siku hiyo, kikubwa ni kusubiri siku ifike na mjadala ukamilike.
“Mkutano huo hautokuwa unamjadili Tyson Fury peke yake, kuna mengi ambayo yatajadiliwa, lakini suala la Mr Fury litakuwa la kwanza, kwa kuwa ni jambo ambalo linasambaa kila kona kwa sasa, siyo tu kuhusu kutumia dawa, lakini kuna mambo mengi ambayo atakuwa anajadiliwa,” alisema Smith.
Hata hivyo, Fury ameonekana kuwa mtu ambaye hana wasiwasi kwa kuwa amedai kuwa anasubiri matokeo baada ya kikao hicho, lakini tayari amefanya mambo mengi katika maisha yake, hasa kutokana na ngumi.
“Naweza kusema kuwa nimefanya mambo mengi sana katika maisha yangu kutokana na ngumi, unadhani kwa nini nimetumia cocaine? Haya ni maisha yangu, naweza kufanya chochote ninachokitaka, nimetumia cocaine na kuna watu wanaendelea kutumia pia.
“Sijafanya mazoezi ya Gym mwezi sasa, lakini katika kipindi hiki nimekuwa na matatizo mengi, hivyo ukweli ni kwamba nimechoka kuishi na nikisema hivyo nadhani ninaeleweka, nimechoka. Nipo katika wakati mgumu kwa sasa na sijui kama nitamaliza mwaka huu,” alisema Fury.