NA CHRISTOPHER MSEKENA
WIKI hii waandaaji wa tuzo za Vijana wa Kitanzania 50 Wenye Ushawishi (Most Influential Young Tanzanias) Avance Media wametoa orodha ya washiriki wake huku tuzo zenyewe zikitarajiwa kutolewa Januari 16, mwakani.
Vijana hao 50 wameweza kuvuka kiunzi cha kufanya kazi kwa ajili ya kuboresha maisha ya watu wengine kupitia kujituma, kufanya kazi kwa bidii, kujitolewa na kufanya maamuzi ya kijasiri kupitia sekta za biashara, burudani, sheria na utawala, habari, sayansi na teknolojia, michezo na uwajibikaji katika jamii.
Majina yaliyopenyeza kwenye kinyang’anyiro hicho ni pamoja na Wema Sepetu, Jokate Mwegelo, Ali Kiba, Diamond Platnumz, Joti, Riyama Ally na Vanessa Mdee wakitoka sekta ya burudani.
Watangazaji Babbie Kabae, Hamis Mandi ‘B Dozen’, Dina Marious, Millard Ayo, Idris Sultan na Salim Kikeke hawa wanachuana kwenye sekta ya habari.
Wengine ni Flaviana Matata, Jacqueline Mengi, Millen Magese, Miriam Odemba, Benjamin Fernandes na Osse Greca Sinare kwenye upande wa maisha na mitindo huku Hashim Thabit, Juma Kaseja, Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, Mrisho Ngassa na Shomari Kapombe wakiwania tuzo hiyo kwenye kipengele cha michezo.