KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amesema iwapo chama chake kitapata ridhaa ya kushika dola, watahakikisha wanafuta sheria zote ambazo ni kandamizi kwa wananchi ili kuleta mabadiliko ya kweli.
Kinana alitoa agizo hilo wakati akizungumza na baadhi ya wanachama na viongozi katika Jimbo la Vunjo wilayani Moshi jana.
Alisema kumekuwa na sheria nyingi ambazo ni kandamizi kwa wananchi jambo ambalo si zuri.
Alisema sheria kandamizi kwa wananchi hazina maana na zimekuwa zikileta migogoro baina ya Serikali na wananchi.
“Sheria zimekuwa hazilengi kuwasaidai watu, ni vema zikaondolewa kwa lengo la kuwarahisishia wananchi maisha, maeneo mengi sheria hizi zimekuwa zikiwakandamiza na kusababisha wananchi kuichukia Serikali, CCM ikipata ridhaa ya kushika dola
tutazifuta sheria hizo,” alisema Kinana.
Alisema watu wanaoleta sheria hizo wana lengo la kuzitumia kwa ajili ya kujinufaisha binafsi.
“Wanaoleta sheria hizi ni watendaji ambao zinawanufaisha wenyewe na kuwakandamiza wananchi, nataka wagombea wote kuwa mstari wa mbele kuzikataa, tukipewa ridhaa tutaondoa sheria hizi,” alisema.
Katika hatua nyingine aliwataka wagombea wa nafasi za ubunge watakaobahatika kuwa katika Bunge lijalo kupinga kila kitu ambacho kitawasilishwa na Serikali.
Kwa upande wake mgombea ubunge wa Jimbo la Vunjo, Inocent Shirima, alisema iwapo atapewa ridhaa ya kuongoza jimbo hilo, atahakikisha mapato yanayotokana na Mlima Kilimanjaro yanawanufaisha wananchi.