Na Samwel Mwanga, Nzega
WANANCHI katika Wilaya ya Nzega mkoani Tabora wamehimizwa kutunza na kulinda miradi ya maji iliyoko kwenye maeneo yao ili iweze kuwahudumia kupata maji safi na salama.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP). Advera Bulimba katika kijiji cha Wita kilichoko Kata ya Ndala wilayani humo baada ya kuweka jiwe la msingi la ufunguzi wa mradi wa maji katika kijiji hicho.
Amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo katika wilaya hiyo wamekuwa wakitekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya maji hivyo ni jukumu la wananchi kulinda na kuitunza miradi hiyo kwa manufaa yao.
Dc Bulimba amesema mradi huo wa maji umejengwa kwa ushirikiano kati ya serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) wilaya ya Nzega pamoja na Shirika la World Vision Tanzania kupitia Mpango wa Maendeleo ya Jamii Ndala-AP wilayani humo.
Amesema wadau wakubwa na muhimu katika kulinda na kutunza mradi huo pamoja chanzo cha maji ni watumiaji maji pamoja na wananchi waishio katika maeneo jirani na chanzo hicho hivyo ni muhimu wakavilinda kwa uangalifu bila kuviharibu.
“Wadau wakubwa na ambao ni muhimu katika utunzaji wa vyanzo vya maji ni watumiaji maji na wananchi wanaoishi katika maeneo jirani na vilipo vyanzo hivyo ni muhimu kuelimishwa kuhusu kutumia maji kwa busara, uangalifu na tija bila kuharibu chanzo wala miundombinu ya maji,” amesema Bulimba.
Amesema utunzaji wa mradi huo na chanzo cha maji ambacho ni kisima kirefu kilichoko katika kijiji hicho ni suala mtambuka ambalo linawahusisha wadau mbalimbali na wananchi wakiwemo na kuhakikisha watu wote watakaohusika kuhujumu mradi huo wanachukuliwa hatua kali za kisheria.
Dc Bulimna ameendelea kueleza kuwa suala la kuhifadhi vyanzo vya maji limekuwa likitiliwa mkazo na serikali ya awamu hii ya sita ya inayoongozwa na Rais Samia Suluhu ili afikie adhima yake ya kumtua mama ndoo kichwani ifikapo mwaka 2025.
Aidha amelitaka jeshi la jadi la Sungusungu katika kijiji hicho kuhakikisha mradi huo unalindwa kwa nguvu zote na kuwadhibiti watu wote wenye nia ovu ya kuhujumu mradi huo muhimu kwa wananchi wa kijiji hicho.
Naye Mratibu wa Shirika la World Vision wa Mpango wa Maendeleo ya Jamii Ndala AP, Ngasa Michael amemweleza Mkuu huyo wa wilaya kuwa kwa kushirikiana na Ruwasa wameweza kuhakikisha mradi huo unakamilika na wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.
Amesema kuwa mradi huo wenye vituo vya kuchotea maji 12 unawahudumia jumla ya wananchi 3,401 katika kijiji hicho na umegharimu jumla ya Sh 464,557,269.55 huku Shirika hilo kupitia Mpango wa Maendeleo ya Jamii Ndala likitoa kiasi cha Sh 297,827,869.55 katika fedha hizo.
“Mpango wa Maendeleo ya Jamii Ndala kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 pamoja na mambo mengine ya utekelezaji wa miradi yetu moja ya shughuli kubwa tuliyofanya ni kuhakikisha tunashirikiana na Ruwasa kukamilisha mradi huu wa maji wa Wita,”amesema.
Awali, Kaimu Meneja wa Ruwasa wilaya ya Nzega, Mhandisi Faustine Makoka amesema kuwa kwa sasa mradi huo umekamilika na umeanza kutumika na changamoto iliyopo kwa sasa ni wananchi kushindwa kuunganisha maji majumbani kutokana na gharama kubwa za maunganisho.
“Huu mradi umekamilika ni mradi mkubwa na sasa wananchi walio wengi wanapata maji kupitia vituo vya kuchotea maji na changamoto ambayo tunayo ni wananchi kushindwa kuunganisha maji majumbani kutokana na gharama kubwa,”amesema.
Mhandisi Makoka amesema ili kumaliza changamoto hiyo ofisi ya Meneja wa Ruwasa wilaya ya Nzega itatoa mabomba pamoja na dira za maji kwa Jumuiya ya Kamawinu ambao ndiyo wanasimamia mradi huo ili iweze kuwaunganishia wananchi maji majumbani kwa bei nafuu ambapo gharama zitapungua kwa kiasi kikubwa sana.