Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
MWANASIASA mkongwe nchini, Job Lusinde, amewataka Watanzania wote kufanya kazi kwa bidii kama njia pekee ya kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, ambaye jana taifa liliadhimisha kumbukumbu ya miaka 17 ya kifo chake.
Akizungumza katika kumbukumbu hiyo mjini hapa jana, Lusinde aliyewahi kufanya kazi kwa karibu na Mwalimu, alisema vijana wachape kazi kwa bidii kama namna bora zaidi ya kumkumbuka mwasisi huyo wa taifa. Lusinde amesisitiza pia uadilifu miongoni mwa vijana.
“Wakati wa Mwalimu watu walikuwa wakichapa kazi, hata kwenye ofisi habari za njoo kesho ilikuwa hakuna, wakati tunapata uhuru, ilikuwa uhuru na kazi, imani ya umoja ilikuwa ikiongozwa kwenye nembo, leo tunashukuru baada ya uhuru na kazi sasa ni hapa kazi tu,” alisema.
Balozi Lusinde alisema Mwalimu alikuwa akipenda kila mtu afanye kazi, alikuwa ni mtu mwenye upeo mkubwa, hakupenda makuu aliishi kama mtu wa kawaida na hakupenda ufahari.
“Kama ulitaka kumuudhi Mwalimu mwoneshe ufahari, alikuwa mtu ambaye hapendi makuu, tulijikuta tunafanya naye kazi vizuri kwa sababu tulimwelewa,” alisema.
Alisema alikuwa akipenda watu wanaofanya kazi kwa kuwapa uongozi ili wamsaidie katika kazi za kulijenga taifa.
“Mimi nilipata uwaziri nikiwa na miaka 30, katika baraza la kwanza la mawaziri, tulikuwa 12 akiwemo Mwalimu Nyerere, kati ya hao 12 tayari 10 wamefariki tumebaki mimi na Sir George Kahama.
“Tangu nimfahamu Mwalimu mwaka 1948, miaka mitatu baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, alikuwa akiamini katika umoja ndani ya nchi na kati ya mataifa mbalimbali, aliamini katika Umoja wa Afrika na shirikisho la Umoja wa Afrika,” alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Christine Mndeme, alisema huu si wakati wa kulala bali kila mmoja achape kazi kufuata nyayo za Baba wa Taifa aliyeanzisha dhana ya uhuru na kazi.
“Tumuenzi Baba wa Taifa kwa kujiepusha na mambo yasiyofaa, kama kuvuta bangi, wizi na ujambazi,” alisema. Pia aliwataka wananchi kutunza mazingira na akipatikana mtu anatupa taka ovyo au kujisaidia ovyo faini yake ni Sh 50,000 kwa kila kosa.