29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

Dk. Shein asema ufisadi ni kikwazo cha maendeleo nchini

shein

Na SAMWEL MWANGA-SIMIYU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema vitendo vya ufisadi na ubadhirifu vinavyofanywa na baadhi ya watumishi wa Serikali vinasababisha wananchi kukosa haki zao na maisha yao kuwa duni hivyo Serikali zote mbili haziwezi kuwavumilia.

Akizungumza jana wakati wa kilele cha maadhimisho ya mbio za Mwenge wa Uhuru kilichofanyika katika Uwanja wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi Mkoa wa Simiyu, Dk. Shein alisema wapo watumishi wa Serikali ambao wamekuwa wakiendekeza vitendo vya rushwa jambo ambalo ni kikwazo kwa maendeleo.

“Sote tunakumbuka msemo wa rushwa ni adui wa haki na kwamba sitapokea wala kutoa rushwa,” amewasisitiza juu ya umuhimu wa msemo huo kwa sababu kuna dalili kwamba rushwa ni kikwazo kikubwa katika utekelezaji wa majukumu ya maendeleo katika ngazi mbalimbali zikiwemo za halmashauri, Serikali kuu na taasisi mbalimbali za umma.

Rais huyo wa Zanzibar alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hazitawafumbia macho watumishi wa namna hiyo kwani kuna fedha nyingi zinapelekwa katika halmashauri za wilaya kwa ajili ya kuwapatia vijana lakini zimekuwa zikifikia mikononi mwa watumishi wachache ambao si waaminifu.

“Serikali zote mbili zinatoa fedha nyingi kwa ajili ya kuwawezesha vijana, lakini ukiangalia fedha hizo mahali pengine hazifiki kwa walengwa kwani huliwa na baadhi ya watumishi wachache ambao bila woga wanaendeleza vitendo vya ubadhirifu na ufisadi, hatuwezi kuwavumilia wakibainika watashughulikiwa tu watumishi wa namna hiyo ni lazima watumbuliwe,” alisema.

Awali kiongozi wa Mbio za Mwenge, George Mbijima, akisoma risala ya wakimbiza Mwenge mbele ya Dk. Shein, alisema tangu waanze shughuli hiyo ya kukimbiza Mwenge nchi nzima kwa siku 179 kwa kukagua, kuzindua na kufungua miradi mbalimbali lakini wamebaini baadhi ya miradi kuwa chini ya kiwango na fedha zinazotengwa kwa ajili ya vijana haziwafikii walengwa.

Alisema upotevu wa mapato na kushindwa kukusanya kodi, ubadhirifu, matumizi mabaya ya fedha na madaraka, ambapo utekelezaji wa baadhi ya miradi upo chini ya viwango huku kukiwepo na wizi, uzembe katika mamlaka za Serikali za Mitaa hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa fedha.

“Tumepitia miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu, lakini tulichokibaini ni kuwa miradi mingi iko chini ya kiwango, hailingani na kiasi cha fedha kilichotumika na maeneo mengine tumebaini ya kuwa fedha zinazotengwa na Serikali kuwaendeleza vijana haiwafikii walengwa inapelekwa kwa watu ambao si wahusika,” alisema.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu), Jenister Mhagama, alisema Serikali ya awamu ya tano imeelekeza nguvu zake katika kuwasaidia vijana nchi nzima kwani vijana wa Mkoa wa Simiyu wameonyesha jitihada zao kwa kujiletea maendeleo kwa kuanzisha  viwanda vidogo vya chaki katika Wilaya ya Maswa na kiwanda cha kusindika maziwa kilichoko katika Wilaya ya Meatu na kuwaonya watumishi wote watakaochezea fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya mikopo kwa vijana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles