26.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 12, 2024

Contact us: [email protected]

TUMEKUWA TAIFA LA MASHINDANO, AIBU SANA!

MWAKA 1999 wakati Baba wa Taifa, Mwalimu  Julius Kambarage Nyerere alipokuwa anaumwa, Taifa lote lilipata utulivu mkubwa na kila mmoja kwa nafsi yake alikuwa akimuombea.

 

Mwalimu Nyerere aliombewa kutokana na hadhi yake aliyonayo kwenye Taifa letu, lakini pia kutokana na ukweli kwamba tukio la mtu kama yeye kuugua lilikuwa kubwa sana na Watanzania pengine hatukuwa tayari kumpoteza.  Hata hivyo, Oktoba 14, 1999, alifariki na nchi yote ilikuwa na majonzi.

 

Mwalimu Nyerere alikuwa mwanachama wa CCM, lakini licha ya itikadi yake hiyo ya kisiasa, wananchi wote waliungana, wanasiasa wote waliungana na wote tulimlilia kwa sauti moja.  Katika kipindi hicho, Tanzania iliungana na kuwa na sauti moja ya kumlilia Baba yetu, kiasi cha wageni waliokuwa wametoka nchi zingine kushangazwa na umoja na mshikamano ule.

 

Siku ambayo mwili wa Mwalimu ulikuwa unasafirishwa kwenda Butiama kwa ajili ya mazishi, wanahabari wengi wa ndani na nje ya nchi walikuwa wamekusanyika uwanjani.  Wanahabari wa nje ya nchi walikuwa wameambatana na wale wa Tanzania na kilichotokea wakati ndege iliyobeba mwili wa Mwalimu kuanza kupaa angani, ni kwa kila mtu aliyekuwapo uwanjani hapo kuangua kilio, wakiwamo wanahabari wa Tanzania.  Wageni walitazama na kushangazwa sana.

 

Baada ya hapo, mwanahabari mmoja wa Afrika Kusini aligeuka na kumwambia rafiki yangu mmoja mwanahabari kwamba walidhani wao Waafrika Kusini wanapendana sana na kumpenda sana Baba wa Taifa lao, Mzee Nelson Mandela, lakini wamegundua kwamba Watanzania tunapendana zaidi.  Na kwa hilo, alisema, atarudi nyumbani kwao na kuwaeleza watu wake kupitia kalamu yake, namna Watanzania tunavyopendana.

 

Miaka 18 baada ya tukio hilo na ushuhuda wa mwanahabari yule wa Afrika Kusini, hali ya upendano na mshikamano baina yetu imebadilika kabisa na sidhani kama ataamini kwamba Tanzania ya mwaka 1999 ndiyo Tanzania ya sasa.  Sidhani kama ataamini kwamba nchi ile aliyoiona mwaka 1999 ndiyo yenyewe anayoiona sasa.  Sidhani.

 

Miaka minne iliyopita, niliamua kujikita zaidi katika jambo moja: uelewa wa mitandao ya jamii. Nilitaka kujua endapo matumizi ya mitandao ya jamii inasaidia Taifa kama letu na kama inachukua nafasi nzuri ya kuendeleza upendo na mshikamano baina yetu. Hata hivyo, jambo nililokuja kuligundua hadi hivi sasa ni kwamba ukianza kufuatilia kila kitu kilichomo kwenye hii mitandao ya jamii, utashikwa na hasira na kujiuliza ‘integrity’ ya watu imepotelea wapi.

 

Kipimo cha faida ama hasara za mitandao ya jamii na namna inavyochangia katika kuendeleza upendo na mshikamano baina yetu Watanzania, kinaendelea kujidhihirisha kadri siku zinavyozidi kusonga mbele.  Mfano mmoja wa karibuni sana ni haya yanayoendelea tangu kushambuliwa kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Mheshimiwa Tundu Lissu, takribani wiki mbili zilizopita.  Kupitia mitandao ya jamii, akili za kweli za baadhi ya watu zimeanza kuonekana na inasikitisha sana.

 

Tukio lililotokea ni tukio la kwanza la ajabu zaidi kutokea nchini kwetu na ni tukio ambalo halikutakiwa kujali itikadi za kisiasa, bali kila mtu atambue kwamba kilichotokea kimeichafua Tanzania na kinatakiwa kulaaniwa kwa nguvu.  Hata hivyo, malumbano ya watu yaliyokuwa yakiendelea kupitia mitandao ya jamii kuhusiana na shambulio la Lissu, yalikuwa yanasikitisha na kuumiza.

 

Kwa tukio ambalo tulikuwa tukitarajia kila mtu atatoa pole kwa Lissu mwenyewe na kwa familia yake, wengine wameamua kujikita kutoa uchambuzi wao wenyewe, wakidai kwamba hiyo ni mipango ya mbunge mwenyewe kutaka kujizolea umaarufu.  Na anayetoa kauli hiyo, ni mtu ambaye unajua kabisa kwamba yupo upande wa pili wa ulingo wa siasa.

 

Imefikia hatua kumekuwa hata na malumbano juu ya nani aliyetoa ndege iliyombeba Lissu kwenda jijini Nairobi nchini Kenya, alimradi tu ijulikane kwamba ndege hiyo ilikodiwa na mtu kutoka chama kingine na hivyo chama chake kutaka kutafutia kauli ya kulisemea hilo, wakati aliyetoa ndege wala hata hakutoa kwa jina la chama chake na wala chama chake hakijasaidia hata tone moja ya mafuta.

 

Wengine pia hapo hapo ndio wameona pa kujitafutia mtaji wa biashara.  Kila tawi sasa limeamua kuanzisha mchango wa kukusanya pesa kwa ajili ya kusaidia matibabu, kana kwamba chama chenyewe hakiwezi kuwa na mwongozo mmoja na akaunti moja kwa ajili ya kulifanya hilo.  Unabaki kujiuliza, hivi kila tawi likianza makusanyo ya namna hiyo, pesa zinazokusanywa zitaratibiwa vipi na tutajuaje pia uhalali wa wakusanyaji utitiri waliojitokeza?

 

Matukio kama haya yanafanya nijiulize ni Taifa la namna gani ambalo Tanzania tumeamua kuwa?  Taifa la malumbano, mashindano na wanyang’anyi?  Taifa ambalo watu wanataka kutafutia umaarufu na sifa kwa mgongo wa matatizo ya wenzao?  Taifa ambalo furaha ya wengine ni kuwasema vibaya wapinzani wao, hata kama wana majeraha kadhaa ya risasi kwenye mwili wao?  Taifa ambalo watu wanatoa taarifa kwa vyombo vya habari ili tu kujitangaza kuwa wameshiriki kutoa msaada wakati hawajashiriki hata kidogo?  Taifa ambalo neno “michango” limekuwa wimbo wa kila siku ambao watu wameshachoka nao?

 

Natamani yule mwanahabari wa Afrika Kusini aliyekuja nchini mwaka 1999 wakati wa msiba wa Baba wa Taifa, aje leo.  Natamani kusikia atakachosema baada ya kusoma mitandao ya jamii na kuona Watanzania tunavyolumbana na kuchezea kamari uhai wa watu.  Natamani kusoma atakachokiandika kutokana na namna Watanzania tunavyosemana kupitia mitandao ya jamii. Natamani kupata maoni yake kuhusiana na mwenendo wa maisha ya Mtanzania mmoja dhidi ya mwingine.

 

Swali kuu ninalojiuliza ni hili:  Bado atasema kwamba sisi tunapendana kuliko watu wa taifa lingine lolote?  Bado ataweza kutoa ushuhuda juu yetu kwa familia yake?  Bado ataweza kuandika makala kuhusu mshikamano wetu kwa wasomaji wa nchi yake?  Bado ataiona Tanzania ya 2017 sawa na ile aliyoiacha mwaka 1999? Bado atatuona tunapendana?  Tujitafakari!

 

Mwisho….

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles