26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Tume: Zawadi hakujifungua Mapacha

Na Derick Milton, Simiyu

Hatimaye sakata la mama mmoja anayefahamika kama, Zawadi Sayi Abdallah mkazi wa Kidinda Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu kudai kuwa alijifungua mapacha lakini akapewa mtoto mmoja limepatiwa majibu baada ya Tume iliyoundwa na Serikali kubaini kuwa mama huyo alijifungua mtoto mmoja na siyo mapacha.

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu Lupakisyo Kapange akipokea ripoti ya uchunguzi wa tukio la mama mmoja Zawadi Abdhallah mkazi wa Bariadi ambaye alidai kujifungua mapacha hospitali ya halmashauri ya mji Bariadi lakini akapewa mtoto mmoja.

Ripoti hiyo imekabidhiwa Alhamisi Agosti 19, kwa Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Lupakisyo Kapange.

Hata hivyo tume hiyo imeeleza kuwa katika uchunguzi wake, imebaini kuwa kilichosababisha mama huyo na familia yake kulalamika ni taarifa za uzushi zilizotolewa na watumishi wa Afya katika hospitali ya halmashauri hiyo (Somanda) alipojifungulia na kituo cha Afya Muungano.

Licha ya kubaini hivyo, Kamati hiyo imeeleza kuwa ilishindwa kuwabaini watumishi hao ambao walitoa taarifa za uzushi juu ya mama huyo kujifungua mapacha kutokana na malalamikaji kushindwa kuwatambua waliompatia taarifa hizo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye ni Kaimu Mkuu wa polisi Bariadi, (OCD) Pitter Mtinginya ameeleza kuwa kamati hiyo ilipitia nyaraka zote na kuwahoji watumishi, viongozi Idara ya Afya pamoja na walalamikaji.

“Kamati ilifanya kazi kwa weredi mkubwa, ilipitia nyaraka zote, ushahidi ulionekana kupitia jarada la mgonjwa, lakini kupitia vipimo na nyaraka za chumba cha upasuaji zote zilionyesha tarehe 23/05/2021 zawadi alijifungua mtoto mmoja wa kiume mwenye uzito wa kilo 3.3,” amesema Mtinginya.

Aidha, Mwenyekiti huyo amesema kuwa taarifa za mama huyo kuwa amejifungua mapacha, zilivumishwa na watumishi wa hospitali hiyo na kituo cha Afya Muungano na kwamba hazikuwa na ukweli bali zilileta taharuki.

Kutokana na hali hiyo Mkuu wa Wilaya hiyo Lupakisyo Kapange ambaye ndiye aliamua kuunda tume hiyo, amemwagiza Mganga mkuu wa halmashuari ndani ya wiki mbili kuhakikisha watumishi hao wanatafutwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Lupakisyo mbali na kuipongeza tume hiyo amesema kuwa watumishi hao lazima wapatikane kwani wao ndiyo wamesababisha taharuki hiyo bila ya kufuata maadili ya kazi yao ambapo ameeleza ikiwa uongozi utashindwa kuwapata atatumia vyombo vyake kuwasaka.

“Kamati hii imefanya kazi kubwa sana na jambo hili tunalifunga, ukweli Zawadi alijifungua mtoto mmoja na siyo mapacha, ndani ya wiki mbili Mganga Mkuu wa Halmashauri hao watumishi walisababisha haya watafutwe na kuchukuliwa hatua,” amesema Lupakisyo.

Tume hiyo uliundwa na vyombo vyote vya ulinzi na usalama, watumishi idara ya Afya pamoja na waandishi wa habari ambapo wamefanya kazi kwa muda wa wiki mbili.

Ikumbukwe kuwa Mama huyo (Zawadi) aliwalalamikia wahudumu wa afya katika hospitali ya halmashauri hiyo (Somanda) kumpatia mtoto mmoja badala ya watoto wawili (mapacha) baada ya kufika hapo na kujifungua.

Kwa mujibu wa Zawadi, licha ya kupewa mtoto mmoja baada ya kujifungua na kuondoka kurudi nyumbani akiwa ameridhika alishangaa kupata taarifa mpya kutoka kwa mhudumu mmoja ambaye alimweleza kuwa alijifungua watoto wawili.

“Wiki mbili baada ya kupita tangu nitoke hospitali, nilirudi hapo hospitalini kwa ajili ya kusafisha kidonda, ndipo huyo mhudumu akanipa hizo taarifa, nikaunganisha na zile ambazo mhudumu wa kwanza alinipatie wakati wa vipimo, nikaona kuna ukweli,” alisema Zawadi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles