23.7 C
Dar es Salaam
Saturday, September 23, 2023

Contact us: [email protected]

Madeni yasababisha Meatu kukosa Dawa

Na Derick Milton, Simiyu

Idara ya Afya Halmashauri ya Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu, imekiri uwepo wa changamoto kubwa ya uhaba wa dawa katika vituo vya kutolewa huduma za Afya unaosababishwa na madeni.

Kauli hiyo imekuja baada ya Madiwani wa halmashauri hiyo kulalamika wakati wa mkutano wa Baraza la Halmashauri uliofanyika leo Jumanne Agosti 24, mjini Mhanuzi, ambapo wamedai kuwa zahanati nyingi hazina hata dawa za msingi ambazo zinatakiwa kuwepo kila wakati.

Kaimu Mganga Mkuu wa halmashauri, Dk. Josephat Mponeja amedai kuwa changamoto hiyo imesababishwa na vituo vingi vya kutolea huduma kwenye halmashauri kuwa na madeni makubwa bohari ya dawa (MSD).

Amesema kuwa madeni hayo yamesababisha mzabuni ambaye ni (MSD) kushindwa kuleta dawa kwa muda mrefu, ambapo ameeleza jitihada zimekuwa zikifanyika kuhakikisha madeni hayo yanalipwa.

“Ni kweli tunalo tatizo la dawa kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma za Afya, tatizo ni madeni kwenye vituo hivi, lakini jitihada zimekuwa zikifanyika kadri tunavyopata pesa ndivyo tunavyolipa deni hilo,” amesema Dk. Mponeja.

Hata hivyo Kaimu Mganga Mkuu huyo hakutaja kiasi cha deni ambacho wanadaiwa MSD, na kueleza kuwa dawa ambazo wamekuwa wakipata ambazo ni kidogo wamekuwa wakigawa kulingana na mahitaji ya vituo.

“Tukipata pesa tunalipa kidogo na mgao wa dawa ukija ni mdogo sana hautoshelezi mahitaji, ndiyo maana maeneo mengi utakuta kuna uhaba mkubwa wa dawa, lakini tumeendelea kulifanyia kazi,” amesema Dk. Mponeja.

Awali, Madiwani hao walisema kuwa tatizo la dawa ni kubwa, huku wengi ambao wanateseka wakiwa wale wenye kadi za Bima ya Afya CHF pamoja na NHIF ambapo utakiwa kununua dawa kwenye maduka ya dawa.

“Wananchi tunawahamasisha wajiunge na Bima ya Afya, lakini hali ni mbaya kwenye zahati, vituo vya Afya na hata Hospitali ya Wilaya, hakuna dawa, changamoto ni kubwa, hata zile dawa za msingi hakuna,” alisema Emmanuel Chalya.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Anthony Philipo amemtaka Mkurugenzi wa halmashauri kufanyia kazi changamoto hiyo kwani wananchi wengi wanateseka vijijini kwa kukosa dawa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,699FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles