Na Ramadhan Hassan, Dodoma
KATIKA Mwaka wa fedha 2023/2024 Tume ya Umwagiliaji imepanga kuendelea kutekeleza miradi itakayoongeza eneo la umwagiliaji lenye ukubwa wa hekta 256 ili kufikia hekta milioni 1.2 kama ilivyoelekezwa katika Ilani ya CCM.
Hayo yameelezwa Julai 28,2023 na Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Raymond Mndolwa wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji na mwelekeo ya tume hiyo kwa mwaka wa fedha 2923-2024 kwa Waandishi wa Habari jijini Dodoma.
Amesema hadi kufikia Juni 2023, tume imesaini mikataba 48 yenye thamani ya Sh bilioni 234.1 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa skimu na mabwawa ya umwagiliaji.
Amesema mikataba 22 yenye thamani ya Sh bilioni 25 kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.
Amesema mikataba mitatu yenye thamani ya Sh bilioni 23.9 kwa ajili ya ununuzi wa magari na mitambo.
Amesema hati ya Makubaliano (MoU) na Kampuni mbili kutoka nchi za Italia na Uispania kwa ajili ya kufanya mapitio ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa miradi ya Bonde la Mto Mara na mradi wa Kisegese uliopo katika Bonde la Kilombero.
Amesema tume imefanikiwa kununua mitambo 15 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa skimu za umwagiliaji.
Pia, tume imenunua magari 53 kwa ajili ya usimamizi wa miradi ya umwagiliaji. Tume pia imefanikiwa kupata fedha kutoka Benki ya Dunia kupitia mradi wa PFoR ambapo utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2023/2024.
amesema maeneo ya kipaumbele katika mwaka wa Fedha 2023/2024 ni kukamilisha ujenzi wa skimu mpya 25 zilizoanza kutekelezwa katika Mwaka 2022/2023.
Pia kukamilisha ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu 30 zilizoanza kutekelezwa katika Mwaka 2022/2023.
Vilevile, kukamilisha ujenzi wa mabwawa 14 yenye mita za ujazo 131,535,000 yaliyoanza kujengwa Mwaka 2022/2023.
Pia, kukamilisha usanifu wa mabonde 22 ya Umwagiliaji ulioanza Mwaka 2022/2023.
“Kuanza ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji kwenye mabonde 22 yenye jumla ya hekta 306,361, kuanza ujenzi wa skimu mpya 35 zenye jumla ya hekta 111,390,” amesema Mkurugenzi huyo.