28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Tume ya Uchaguzi yawaonya wasimamizi

 RAMADHAN HASSAN -DODOMA 

WASIMAMIZI wa Uchaguzi Mkuu, wametakiwa kuzingatia weledi na kuepuka kufanya kazi kwa mazoea ili kupunguza au kuondoa malalamiko yanayoweza kujitokeza wakati wa uchaguzi. 

Akifungua mafunzo ya siku tatu jijini hapa, yaliyokutanisha washiriki 162, Kamishna wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Omari Ramadhani Mapuri, alisema kuwa wasimamizi hao wa uchaguzi katika kanda ya kati wanatakiwa kuzingatia maadili wanapofanya kazi hiyo. 

Alisema uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali zinazopaswa kufuatwa na kuzingatiwa akisisitiza kwamba hatua na taratibu hizo ndiyo msingi wa uchaguzi mzuri wenye ufanisi usio na malalamiko. 

Mapuri alisema wasimamizi hao, katika mkutano huo wa siku tatu wanatakiwa kubadilishana uzoefu, kujadili namna bora ya kufanikisha uchaguzi, lakini pia kujadili namna bora ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika hatua mbalimbali za uchaguzi. 

Aidha Mapuri, aliwataka wasimamizi hao kufanya kazi kwa kufuata maadili kwa kuzingatia Sheria, Kanuni pamoja na maagizo na maelekezo yanayotolewa na Tume ya Uchaguzi. 

“Mnatakiwa kutumia mkutano huu, kubadilisha uzoefu na kufanya kazi kwa kufuata maadili kwa kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo pamoja na maagizo ya Tume ya uchaguzi,” alisema. 

Mapuri alisema wasimamizi hao wameaminiwa na kuteuliwa na tume katika nafasi hizo za usimamizi wa uchaguzi kwa kuwa wana uwezo wa kufanya kazi hiyo hivyo wanatakiwa wajiamini na kujitambua. 

Alitoa wito kwa wasimamizi hao kuhakikisha kuwa wanayaelewa vema maeneo yao ya kazi kijiografia na kuhakikisha kwamba wanawatumia vizuri wasaidizi walio chini yao katika maeneo yao ili kutoa matokeo bora. 

Pia, aliwataka wasimamizi hao kujua miundombinu mbalimbali ya kufika kwenye vituo vya kupigia kura katika majimbo wanayosimamia uchaguzi. 

Mapuri aliwataka washirikishane na vyama vya siasa pamoja na wadau wengine wa uchaguzi katika mstakabali mzima wa uchaguzi ili kuongeza uwazi katika uchaguzi na hivyo kuleta ufanisi. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles