Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi nchini, imesema tayari imeanza kazi rasmi, hivyo kutoa wito kwa wananchi kutoa maoni ya kile wanachohotaji kifanyiwe maboresho katika mfumo wa ulipaji na ukusanyaji kodi.
Akizungumza leo Oktoba, 22 2024 Ikulu jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa tume hiyo, Balozi Ombeni Sefue amesema wapo tayari kushirikiana na kumsikiliza kila mdau iwe mmoja mmoja, kupitia vyama vya kitaalamu, jumuiya za biashara na nyingine ili kupata maoni yatakayowasilishwa kwa Rais Dk. Samia Suluhu.
Balozi Sefue amesema lengo ni kuhakikisha kunakuwa na mfumo bora wa kukusanya mapato na itafanya tathimini hiyo kwa kushirikisha wananchi.
“Mtakumbuka kuwa tarehe 4 Oktoba 2024, Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alizindua rasmi Tume ya Kutathmini na Kushauri kuhusu Maboresho ya Kodi.
Kama mjuavyo Tume hii imeundwa kufuatia malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji kuhusu kero mbalimbali zinazotokana na mfumo wa kodi nchini,” ameeleza Mwenyekiti huyo.
Amefafanua kuwa Tume hiyo imepewa miezi sita lakini machakato wa kutoa maoni utachukua kipindi kisichopungua miezi miwili kuanzia sasa, baada ya hapo watachukua mapendekezo hayo, kuyafanyia tathmini na kuyachanganua kabla ya kuwasilisha kwa Rais.
Ameeleza kuwa wameandaa namna bora ya kuratibu ushiriki wa wananchi, wafanyabiashara, wawekezaji na taasisi za umma na binafsi, asasi za kiraia, wadau wa maendeleo na wananchi wanaishi nje ya nchi ikiwamo kufanya mikutano katika maeneo mbalimbali.
“Tumeandaa mifumo rahisi, rafiki ya wazi ya ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wadau wa aina zote nchini ikiwemo dodoso la mtandaoni linalopatikana kupitia kiunganishi cha edodoso.gov.go.tz kwa kutumia namba ya dodoso 544978, barua pepe tume@taxreform.go.tz na maboresho. Kodi@taxreform.go.tz, namba za simu 0748 755 677, 0738 588 813,”
Balozi Sefue amesema lengo la Serikali imedhamiria kufikia kiwango cha asilimia 15 ya pato la Taifa ifikapo mwaka 2026/27 hatua itakayoongeza uwezo wa nchi kugharamia miradi ya maendeleo na kupunguza kiwango cha utegemezi wa mikopo na misaada.