Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
TUME iliyoundwa na Mufti wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zubery, kuhakiki mali za waislamu nchini imewataka waumini wa dini hiyo kutoa taarifa za mali zilizouzwa kihalali au isivyo halali ili waweze kuzihakiki.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo, Sheikh Issa Othman Issa, alisema tume hiyo ni huru na ina wataalamu tofauti wakiwamo wa kutoka serikalini ambapo lengo lake ni kuhakikisha mali hizo zinapatikana na kurudishwa kwenye mikono ya Waislamu wenyewe.
Alisema ushirikiano wao utaisaidia tume hiyo kufanya kazi zake na kumaliza kwa wakati ili ziweze kuingizwa kwenye kumbukumbu.
Sheikh Issa alisema mpaka sasa tume hiyo imetimiza siku 30 tangu ilipoundwa na itazunguka nchi nzima ili kufuatilia mali za Waislamu ziweze kurudishwa.
“Tunawaomba waislamu kutoa ushirikiano kwa tume yetu pindi wanapopita kwenye maeneo yao ili tuweze kuingiza kwenye kumbukumbu zetu, jambo ambalo linaweza kurahisisha shughuli hii.
“Ndani ya kipindi cha mwezi mmoja, tume hiyo imeweza kupita katika maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kufuatilia jambo hilo, hali inayoonyesha wazi kuwa, kazi hiyo ni rahisi na kwamba inaweza kuisha katika kipindi cha muda uliopangwa wa siku 90,” alisema Issa.
Miongoni mwa mambo ambayo yanafuatiliwa na tume hiyo ni pamoja na mikataba ya uuzaji wa viwanja na mali nyingine ambazo zinamilikiwa na Baraza au taasisi zake.