25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Tumbaku ya mamilioni yakamatwa ikisafirishwa nje

Na MURUGWA THOMAS 

-TABORA

ILI zao la tumbaku liweze kuwanufaisha wakulima na waondokane na madeni, Serikali ya Mkoa wa Tabora inaendesha msako mkali kipindi hiki cha msimu wa soko kupambana na walanguzi.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa huo, Aggrey Mwanri, alipokutana na waandishi wa habari kuwaonyesha shehena ya tumbaku iliyokamatwa ikisafirishwa kuelekea nchi jirani.

Mwanri ameliagiza Jeshi la Polisi kushirikiana na bodi ya tumbaku nchini kuwakamata wote watakaobainika kujihusisha na biashara hiyo haramu ambayo inahujumu uchumi wa mkoa na Taifa kwa ujumla.

Alisema watu wawili waliokuwa wakitumia gari aina ya Fuso lenye namba za usajili T 290 DGV, walikamatwa juzi usiku wilayani Kaliua wakisafirisha tumbaku kinyume cha sheria.

Alisema thamani halisi ya tumbaku hiyo iliyokamatwa bado haijafahamika na kwamba gari hilo lipo kituo kikuu cha polisi mjini Tabora.

Licha ya kukamatwa kwa gari hilo ameliagiza Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama kulisaka gari jingine ambalo pia lilikuwa na shehena ya tumbaku inayodaiwa kutoroshwa baada ya kubaini wanafuatiliwa. 

 Mwanri alisema mkoa kupitia vikao vyake ulijiwekea utaratibu wa kusafirisha mazao kuwa ni mchana tu na si vinginevyo ili kuwadhibiti walanguzi na wana ushirika wachache wasiofuata taratibu za vyama vya msingi.

Alitoa wito kwa wananchi wote kushiriki katika vita hiyo na kuwaonya watumishi wa Serikali kutojihusisha na vitendo hivyo vya uhujumu uchumi.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa, Emanuel Nley, amethibitisha kukamatwa kwa watu wawili wakitumia gari aina ya fuso kusafirisha zao hilo la tumbaku kutokea Wilaya ya Kaliua usiku wa kuamkia jana.

Kamanda Nley alisema watashirikiana na vyombo vingine kuhakikisha mazao yote yanauzwa na kusafirishwa kwa kufuata sheria na taratibu zake.

Akizungumzia tukio hilo Kaimu Mkurugenzi uendeshaji wa zao hilo kutoka Bodi ya Tumbaku, Stanely Mnozya, alisema mtu yeyote haruhusiwi kununua na kusafirisha zao hilo bila kupata leseni na kibali kutoka bodi.

Mnozya alibainisha kuwa bodi ya tumbaku nchini itashirikiana na vyombo vya dola kuhakikisha zao hilo halitoroshwi kwa kuweka wasimamizi wake kwenye vizuizi mbalimbali barabarani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles