25.6 C
Dar es Salaam
Friday, November 8, 2024

Contact us: [email protected]

TUHUMA MADIWANI KUNUNULIWA: NENO KWA NENO WALIVYOSHIRIKI MAZUNGUMZO YA RUSHWA

Eliya Mbonea, Arusha na Elizabeth Hombo, Dar


BAADA ya video zinazoonesha majadiliano ya siri ya kuwashawishi madiwani wa Chadema katika Halmashauri ya Meru mkoani Arusha, wahamie CCM, Gazeti la MTANZANIA limefanikiwa kuona picha hizo na kuandika majadiliano hayo.

Akizungumza kupitia video inayoonekana katika mitandao hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti, anaanza kwa kumshawishi mmoja wa madiwani hao ili ahame chama chake.

“Unajua mimi nilikuwa sijakutana na diwani huyu, diwani msomi, mimi nimewahi kukuona mara moja tu kwenye vikao na wale jamaa zako.

“Eheee, sasa tulizungumza kwa kifupi na DAS, alinipa feedback ya mazungumzo yenu mliyokuwa mmezungumza, lakini mimi nikataka tuzungumze wawili.

“Kwa bahati nzuri na yeye amekuwepo, hamna mbaya. Sisi tulikuwa tunakutegemea ingawa sijui mlizungumza nini. Lakini, nilikuwa na option mbili au tatu, kwanza wewe ni msomi sasa hivi ndio muda wa ajira zinatoka.

“Tumefanya mpango uingie kwenye system, kama ambavyo tumefanya kwa Bryson na Josephine, wale wao muda wowote wanaweza kuingia kazini.

“Emmanuel naye kazi yake ndiyo imetangazwa na tunataka aingie kule Arusha DC kwa kipindi ambacho wanasubiria ajira za Serikali wawe wanajitolea kule.

“Kuhusu wewe, niliambiwa unamaliza chuo mwezi wa sita, sijui umeshamaliza,” anaonekana Mnyeti katika majadiliano hayo akisema.

Katika majadiliano hayo, diwani aliyekuwa akizungumza ambaye bado hajajulikana majina yake, alisema tayari ameshamaliza masomo yake.

Baada ya diwani huyo kusema hayo, Mnyeti anaendelea kusema, kwamba sasa watapambana ili diwani huyo aingie kwenye ajira ingawa hajajua ni ajira gani watakayokubaliana.

“Ukibadilika ukarudi CCM, bado utashinda asubuhi kwa sababu watu bado wanakukubali. Unarudi ili kuongeza nguvu ya chama kwa usomi wako huo,” anaonekana Mnyeti akisema.

Hata hivyo, diwani huyo anaonesha wasiwasi na kusema. “Unajua, once unaambiwa kwamba ni ajira, ile inakuwa fumbo kwa sababu ajira hiyo ipo kwenye mamlaka nyingine japokuwa najua na nyinyi ni wawakilishi,” alisema.

Aidha, katika mazungumzo hayo yaliyokuwa na watu wengine pembeni, Mnyeti anasikika akimhakikishia diwani huyo, kwamba suala la Bryson ni tofauti kidogo na la kwake kwa sababu ameamua kufunga safari kwa sababu ya Bryson.

“Wizara ya Maliasili hata ajira walikuwa hawajatangaza wala walikuwa hawahitaji watu, lakini wakasema mwezi wa tisa, watamchukua tarehe moja, wakasema watakuwa na nafasi tatu za kitaaluma kama hiyo ya Brai, kwa hiyo, wakasema watamchukua.

“Lakini, kutofanya kazi kule yeye mwenyewe ndiye aliyeamua, lakini kuhusu ajira, tunaweza tukawa hatufanyi uamuzi, lakini tuna ‘influence’.

“Kwa mfano, sasa hivi imepelekwa CV ya Brai peke yake ndio tulikuwa hatujapeleka, Mzee Kinana mwenyewe alikuja kuyachukua haya majina hapa, kwa hiyo, na yeye kwa nafasi yake anakwenda kufanya anayoyajua yeye.

“Walinieleza issue zako, zipo zinazohitaji muda, zipo tunazoweza kuzifanya hata kuanzia wiki ijayo. Kwa mfano, wiki ijayo nina ziara nataka niongee ila yapo yanayohitaji muda lazima tukae tufanye mipango, tuweze kuyamaliza.

“Lakini, kwa kuwa Rais anakuja baada ya wiki tatu, hata kama tutaongea naye, tunataka tumwambie kuna vijana wamehama tunaomba uwasaidie.

“Inaleta maana, yupo hapa tarehe 23, mwezi huu kwa sababu atalala hapa, sisi tunataka tuzungumze naye kwenye ratiba atazungumza na wakurugenzi wote wawili, DAS na DSO.

“Kwa hiyo, huo usiku tunataka tumwambie bwana hebu ondoka na hawa watu ili hata wengine wapate moyo wa kuendelea kutoka kwa sababu hawa wametoka kwa ajili yako na inaweza kuleta chachu zaidi,” anasikika Mnyeti katika majadiliano hayo.

Hata hivyo, wakati Mnyeti akisisitiza hivyo, diwani aliyejiuzulu kwa upande wake anasikika akisema;

“Unajua mimi sikuwapo huku muda, nilikuwa nategemea kama ‘pilot’ ambayo itanijengea mimi ‘trust’ ndio maana nilikuwa kidogo navutika,”anasikika diwani huyo.

Baadaye kidogo, Mnyeti anaingilia kati na kusema, ngoja nikuambie, katika hali ya kawaida, kama binadamu anakuwa na ‘doubt’, Brai ana doubt na ajira yake, lakini sisi tuko hapa ndiyo maana tunahangaika na hayo mambo ya Josephine ajira zake TRA.

“Emma amejishikiza pale wametangaza nafasi yuko pale sasa hivi na hata kama nikuongea na mkurugenzi huyu, lazima aajiriwe, hii ya ajira yake imeshaisha,”anasikika Mnyeti akisema.

Sauti nyingine pembeni inasikika ikisema, “mimi hapa juma ngapi ofisa utumishi anaondoka kwenda Dar es Salaam kufuatilia vibali vyetu.

Wakati sauri hiyo ikisikika, Mnyeti anaingilia kati na kusema ngoja nikuambie.

“Unasikia mkurugenzi, kwa mfano, huyu bwana tukikubaliana, nitakachokifanya kwa kipindi ambacho utakuwa hujapata ajira, nitakuwa nakulipa mshahara.

“Yaani nitakupa hela yako wewe mwenyewe utakuwa unajua unafanyaje ili sasa wakati huo sisi utakuwa ni mzigo wetu kuingia kwenye system na hiyo inayobaki, iwe inatunza familia yako,” anasema Mnyeti huku diwani huyo akionyesha kuridhika.

Wakati mazungumzo hayo yakiendelea, Mnyeti anasema.

“Ngoja nikwambie kitu, kwa mfano sasa hivi ukisema unahama na kusema nikakuchukulie hela mahali, ntakuchukulia ntakwambia hii miezi miwili au mitatu, familia itakaa hivi.

“Lakini, wakati huo sasa, sisi ni mzigo wetu kukufanya uingie kwenye system ili baada ya miezi miwili au mitatu, flow yako ianze kuflow ndani. Yaani tukikubaliana sasa hivi, sina matatizo” anasema Mnyeti.

Hata hivyo katika mazungumzo hayo, diwani aliyejiuzulu anasikika akisema;

“Kama itawezekana, lolote at any time, ninaweza pia nikaja kama ulivyosema two milioni kimsingi siwezi nikaiita penati, (mara kicheko kinasikika huku Mnyeti na mtu huyo wakigongesha mikono).

“Iam taking for granted kwa sababu unaji sacrifice manake by the way, pia huwezijua reaction baada ya hapo manake najua naenda kuanza upya,” anasema diwani aliyejiuzulu.

Hata hivyo, Mnyeti anaongeza; yaani wewe usiwe na wasiwasi, itakuwa sorted huku akiungwa mkono na diwani aliyejiuzulu.

Baadaye, Mnyeti anamjibu, wewe niambie tunamaliza hapa hapa tukiwa wote wewe sema tusaidiane, niambie.

Majadiliano hayo yanaendelea kwa diwani aliyejiuzulu kusema; manake kweli unajua hiyo two milioni hata ukiangalia, mpaka unaniogopesha kusema.

Kisha sauti nyingine pembeni inasikika ikisema, kwa sababu nashangaa hamna diwani aliyetoka hapa zaidi ya milioni mbili, lakini  diwani aliyejiuzuru anasema, huwezi jua, Brai ni jamaa yangu sana hata yeye alinificha.

Katika eneo hilo, Mnyeti anasikika akisema “hebu sikiliza nikuambie kwa watu wenye akili kama wewe, huwezi kukaa kwenye hicho chama,” alisema.

Majadiliano yanaendelea kwa diwani aliyejiuzulu kuuliza, naweza kuleta muhutasari?

Kabla hajajibiwa, sauti nyingine inasikika pembeni, huo muhutasari mimi nitauchukua huko huko kwenye kijiji huo hata siuhitaji huku, kwanza hii haina shida.

“Wewe unazidi kutuchelewesha, hebu maliza hiyo habari greda liende kule, halafu wewe jioni njoo tumalize,” anasikika Mnyeti.

Baadaye, diwani aliyejiuzulu anaonekana kuweka msisitizo katika eneo hilo akisema, nyinyi mkimaliza hiyo, hata mtu akijua kuna kitu fulani kimefanyika kijijini watajua huyu bwana alishaondoka.

Baada ya maneno hayo, Mnyeti anasikika akimwambia diwani huyo, kwamba anaweza kuandika barua na hakuna mtu atakayeitangaza barua hiyo.

Baadaye inasikika sauti nyingine pembeni ikisema, wewe unajua Ngabobo aliandika barua lini lakini Mnyeti anasema imekaa wiki mbili hadi aliposema yeye.

Diwani aliyejiuzulu anasikika pia akisema kama ni hivyo, basi mimi niandike nije nayo kesho kama huyo nanihii ataongezea kidogo hapo.

Baada ya sauti hiyo, sauti ya pembeni, inasikika ikisema acha kuleta ‘verification’, sikiliza ukiandika tu kesho ukija nakuonyesha na shule hiyo hapo nenda ingia kafundishe.

Baadaye Mnyeti anasikika akisema, ninyi mnachelewesha, lakini kaba hajaendelea, mara diwani aliyejiuzuru anasema.

“Mimi hilo la ajira sina wasiwasi nalo kuna shule nyingi sikuziangalia sana, naangalia hiyo kitu. Kabla hajamailiza, Mnyeti anasikika akisema jamaa mjanja huyu!

Baadaye Mnyeti anasikika akisema anashauri mambo mengine yafanyike hata kama ni kuandika barua sasa hivi.

Mnyeti aruka ‘kimanga’

Viongozi wa wa Wilaya ya Arumeru waliotuhumiwa kuwashawishi madiwani wa Chadema ili kukihama chama hicho wameahirisha mkutano wao na waandishi wa habari uliopangwa kufanyika wilayani hapa.

Mkutano huo ambao uliitishwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Alexander Mnyeti ulipangwa kufanyika jana saa sita mchana ili kujibu tuhuma zilizoibuliwa na wabunge Joshua Nassari wa Arumeru Mashariki na Godbless Lema wa Arusha Mjini.

Pamoja na waandishi wa habari kufika katika ofisi za DC Mnyeti, wasaidizi wake walisema hawakuwa na taarifa za kuwepo kwa mkutano huo.

Hata hivyo taarifa zilizofikia MTANZANIA baadaye zilidai kuwa Mnyeti alikwenda uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro kumpokea Makamu wa Rais, Samia Suluhu alikuwa safarini kuelekea Wilaya ya Ngorongoro.

NASSARI TAKUKURU

Wakati huo huo, wabunge wa Chadema, Joshua Nassari na Godbless Lema wamewasilisha kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Valentino Mlowola, ushahidi kuhusu madiwani wa chama chao kununuliwa.

Wabunge hao waliokuwa wamesindikizwa na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, waliwasilisha ushahidi huo jana ofisi za makao makuu ya Takukuru zilizopo Upanga, jijini Dar es Salaam.

Wabunge hao walitumia takribani saa mbili kuanzia saa 8:39 mchana hadi saa 10:10 jioni walipotoka na kuzungumza na waandishi wa habari wakisema baada ya kukutana na Mlowola, aliwashauri pia kufungua jalada la malalamiko.

Walisema awali walikuwa na wasiwasi wa kutosikilizwa kwa vile ni wapinzani, lakini walitolewa hofu na Mlowola aliyewaeleza taasisi hiyo ni chombo huru.

Nassari alisema: “Tumekutana na Mkurugenzi wa Takukuru na timu yake pamoja na mkurugenzi wa investigation (uchunguzi).

“Tumekubaliana mambo fulani ya msingi, la kwanza  uchunguzi umeanza rasmi kuhusu ununuzi wa madiwani ambao sisi tuna ushahidi usiokuwa na shaka kwamba walikuwa hawajiuzulu kwa kuunga mkono Rais bali walikuwa wanaunga mkono rushwa.

“Ili jalada (la uchunguzi) lifunguliwe rasmi, itabidi mimi nije kesho (leo) au wakati ambao nitaona utafaa ili niweze kuandika malalamiko yangu rasmi. Vile vile na wale ambao nilishirikiana nao katika uchunguzi huu.

“Pia nimekabidhi ile flash niliyowapa waandishi wa habari, lakini nimemwongeza kidogo, nimemhakikishia nitakapofungua jalada nitamkabidhi ushahidi wote niliokuwa nao.

“Kwa hatua za awali tumepokewa vizuri, mkurugenzi katuhakikishia kwamba ile hofu ambayo tumekuwa nayo kwamba tunaweza tusitendewe haki, tuiondoe kwa sababu taasisi yao ni huru na watafanya kazi yao huru kabisa.

“Tutakapokuja kufungua jalada rasmi na kukabidhi ushahidi wote, nitazungumza na waandishi wa habari,”alisema Nassari.

Akizungumzia kuhusu video ambayo inamwonesha Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mashariki, Alexander Mnyeti huku tarehe ikisomeka 2008/01/08 alisema kwa kuwa yeye si mtaalamu wa IT hivyo alishindwa kubadilisha tarehe.

Mwisho.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles