Kuondolewa kwenye ajira kwa wafanyakazi hewa na wale wa darasa la saba imesababisha Chama cha wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (Tughe) kupoteza zaidi ya wanachama 9,000.
Hatua hiyo imesababisha kupungua kwa mitaji na wanachama hali inayowalazimu kuangalia namna ya kupata wanachama wapya hususani wale wanaoanza kuajiriwa serikalini.
Katibu Mtendaji wa Tughe, Eliabert Mkunda amesema hayo wakati akizungumza katika mkutano wa Baraza Kuu Tughe Taifa kilichofanyika mjini Morogoro jana.
Mkunda amesema baada ya kuathiriwa na zoezi hilo chama hicho sasa kinafanya kinafanya jitihada nyingine za kupata wanachama wapya hasa ambao wanaajiriwa kwa sasa na serikali ili kuongeza wanachama.
Awali akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa chama hicho, Hashim Mntambo amesema pamoja na mambo mengine wanaidai Serikali Sh milioni 480 ambapo fedha hizo zimeshahakikiwa kuwa deni halali lakini bado serikali haijawalipa.
“Kucheleweshwa kwa fedha hizo kunachangia kuyumbisha uendeshaji wa chama na kushindwa kufikia malengo yake kwa muda muafaka kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa za chama,” amesema.