Na ABSALOM KIBANDA
TANZANIA, pamoja na uchanga wake ni taifa ambalo kihistoria limekuwa likisukwasukwa na matukio yanayogusa maisha ya watu wanaopotea, kutekwa, kuumizwa na pengine kuuawa na watu wasiojulikana.
Katika umri wake wa miaka 54 na ushee, Tanzania inayo orodha ya watu ambao majina yao kwa nyakati zao yamekuwa yakijulikana na kubeba umaarufu unaotofautiana, ambao ama walitoweka au kuumizwa na wakati mwingine kutekwa katika mazingira ambayo hadi leo hii yanaacha maswali mengi.
Kule Zanzibar kwa mfano, baada ya mapinduzi ya mwaka 1964 wako watu maarufu kama Kassim Hanga na Idrissa Abdallah Majura ambao walitoweka na hawajapata kuonekana tena hadharani.
Majura ambaye ni baba mzazi wa mwanahabari mkongwe Tanzania, Abdallah Majura, ameendelea ‘kutafutwa’ na wanawe hadi leo pasipo mafanikio.
Katika moja ya andiko la hivi karibuni katika makundi ya Whatsapp, mwanahabari huyo aliwaandikia wahariri wenzake wa vyombo mbalimbali vya habari akiwataka wafanye kila linalowezekana kumsaidia yeye kujua mahali alipo baba yake.
Katika andiko lake hilo, Majura alikwenda mbele na kuandika kwamba hata kama kuna mtu anajua mahali liliko kaburi la baba yake, iwapo atakuwa amefariki dunia, basi angependa japo tu kujua.
Hiki kimekuwa ni kilio kisichokoma kutoka kwa mwanahabari huyo tangu nilipofahamiana naye kikazi kwa zaidi ya miaka 20 sasa.
Nina hakika kwamba hicho ndicho kilio ambacho jamaa na ndugu wa Hanga wanaendelea kubakia nacho katika fikra na kumbukumbu zao.
Pengine fundisho kubwa katika kutoweka kwa Hanga, Majura na watu wengine miaka ya mwanzo ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuendelea kwa hali ya taharuki, si miongoni mwa wanafamilia wa ‘wahanga’ hao, bali kwa visiwa vyote viwili vya Pemba na Unguja vinavyounda nchi hiyo ambayo leo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa maneno mengine, matukio ya namna hii yameendelea kuacha alama za uchungu, machozi na zaidi majeraha yasiyokoma kisiasa ambayo hadi leo yanaitafuna Zanzibar pasipo kukoma.
Ali Sultani Issa katika kitabu chake kiitwacho ‘Race, Revolution and Struggle for Human Rights in Zanzibar – The Memoirs of Ali Sultani Issa and Seif Sharif Hamad’ anaeleza historia ya mikasa ya kisiasa ambayo pia inagusa kutoweka kwa watu mashuhuri wa aina ya Hanga.
Haishii hapo, Issa katika kitabu chake hicho kinachogusa maisha yake, anakwenda mbali na kurejea hadi tukio la kuuawa kwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar baada ya Mapinduzi ya mwaka 1964, Abeid Amani Karume lililotokea Aprili 7, 1972.
Pengine kwa muktadha wa makala ya leo, Issa katika simulizi yake inayotofautiana na historia ya mapokeo, analihusisha tukio hilo la Karume kuuawa na kisasi kilichofanywa na watu wakubwa wa nyakati hizo, na si yule tunayesimuliwa kwamba alifanya kulipiza kisasi cha kuuawa kwa baba yake.
Simulizi za Issa, mtu ambaye alikuwa na mamlaka makubwa kwa nyakati tofauti ndani ya Serikali ya Zanzibar baada ya Mapinduzi hata akafanya kazi ubalozini Uingereza, Pemba na Unguja si za kupuuzwa.
Huyu ni mtu ambaye katika kitabu chake hicho anawahusisha viongozi wazito ambao nachelea kuwataja majina katika andiko langu hili na kuwahusisha na vifo vya aliyepata kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza miaka ya baada ya Mapinduzi, Othman Sharif na mwanasiasa mwingine maarufu, Twala.
Andiko la Issa kama yalivyo mengi mengine yanapaswa si kutukumbusha historia, bali kutufunda na kutufundisha kwamba madoa ya kihistoria yana tabia ya kuzaa hasira zisizokoma kizazi hadi kizazi.
Iwapo kweli akina Hanga, Twala, Majura, Othman Sharif na hata Mzee Abeid Karume walitoweshwa na kuuawa kiharamia, wako wapi leo waliowaua?
Zanzibar ya leo imebakiza watu wachache sana wa aina ya Mzee Ramadhani Haji Faki na Hassan Nassor Moyo, ambao pengine wangali wanajua na bado wana kumbukumbu ya ni nini hasa kiliwafika wenzao hao ambao kutoweka kwao au vifo vyao bado vinaacha maswali.
Tungekuwa ni wanafunzi wazuri wa historia kama taifa, matukio hayo ya kihistoria kule Zanzibar yalitosha kuwa fundisho ambalo lingesaidia kuepuka mengine ya namna hiyo hiyo ambayo yameendelea kutugusa kwa namna na njia tofauti leo.
Katika nchi jirani tu hapo Kenya, matukio ya watu maarufu kutekwa au kutoweka na baadaye miili yao ikakutwa wakiwa wameuawa, yana historia ndefu tangu zama za Rais wa kwanza wa taifa hilo, mzee Jomo Kenyatta.
Kuuawa kwa wanasiasa wenye majina kama akina Tom Mboya mwaka 1969 na Josiah Mwangi Kairuki 1975 ni mifano mibaya ya awali iliyopata kuikumba Kenya ambayo kwa bahati mbaya haijapata kukoma hadi leo.
Wakati Mboya alikuwa kiongozi maarufu wa Chama cha Wafanyakazi, Kairuki alikuwa mwanasiasa mwenye nguvu, ambaye alipata kuwa msaidizi wa karibu wa Kenyatta kabla hajawa mbunge na jina lake lilitajwa sana katika urais kutokana na kuwa na msimamo mkali katika masuala kadhaa.
Matukio hayo ya Kenya hayajapata kuliacha salama taifa hilo kwa namna ile ile ilivyo Zanzibar ambako kila mara moshi hufuka na wakati mwingine moto kulipuka kabisa.
Ni jambo la bahati mbaya kwamba kama taifa tunaonekana kutojifunza. Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinaonekana ama kutoyapa uzito kwa maana ya kuyapuuza au kufumbia macho matukio ya namna hii.
Mwaka jana, taifa lilishuhudia moja ya matukio mabaya katika historia ya nchi hii. Mbunge maarufu wa upinzani, Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana na akaponea chupuchupu kuuawa.
Lissu alinusurika tofauti na ilivyokuwa kwa mzee Karume kule Zanzibar au kwa Tom Mboya na Kairuki kule nchini Kenya.
Wakati Lissu akinusurika, Watanzania wenzetu wengine, mwanasiasa kijana machachari, Ben Saanane na mwandishi wa habari Azori Gwandu ni miongoni mwa majina ya watu ambao kutoweka kwake kumeendelea kuacha maswali hadi leo.
Kama kuna hisia ambazo zinayaunganisha matukio yale ya kihistoria ya kiharamia ya Zanzibar, Kenya na haya ya karibuni ya Tanzania Bara, ni kunyoshewa vidole kwa mamlaka za dola na pengine viongozi wa kisiasa.
Sina hakika iwapo viongozi wa kisiasa wa taifa hili, hasa wale wa Zanzibar wanatambua kwamba hisia kali zisizokoma ambazo zimekuwa ni desturi ya kudumu visiwani, msingi wake ni matukio ya namna hii.
Ninawaasa viongozi wa taifa hili kutambua na kuchukua hatua za kuponya majeraha ya watoto, ndugu na jamaa za Majura, Hanga, Othman Sharif na Twala ambao bado wanaugulia maumivu ya watu wao kupokonywa haki yao ya kuishi. Wanapaswa kufanya kila linalowezekana kuzuia kuendelea kushamiri vitendo vya namna hii.
Tutakuwa tunajidanganya sana iwapo tutakaa kimya na kuyadharau na kuyakejeli masaibu kama yale ya Lissu, Saanane au Azori kwa propaganda za kisiasa, tukiamini kwa kujidanganya kwamba tunao uwezo wa kufunika kombe ili mwanaharamu apite.
Miaka 54 baada ya Mapinduzi ya Zanzibar vilio havijakoma. Bado wachambuzi na wadadisi wa mambo kule Kenya wanaendelea kufukua mafaili na kuibua kila kukicha taarifa mpya juu ya vifo vya akina Mboya na Kairuki.
Ni jambo la kusikitisha kwamba kule Kenya nako hulka zile zile za kuwapoteza watu na kuwaua kwa namna ile ile ilivyokuwa kwa Mboya na Kairuki hazijakoma.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Ofisa wa Tume ya Uchaguzi, Chris Msando alitoweka kabla mwili wake haujakutwa akiwa ameuawa kwa sababu zinazohusishwa na siasa.
Majeraha haya mapya ya Kenya kama yalivyo ya akina Lissu, Saanane na Azori hapa nyumbani yanapanda mbegu ambazo huko TUENDAKO yatazaa vidonda ndugu, na kama si kizazi chetu basi kijacho kitasoma na kusikia majina ya wakubwa kadha wa kadha wa leo wakitajwa na kuhusishwa na matukio haya, tena kwa ushahidi.
Sisi si wa kwanza. Tujifunze kwa makosa yetu, ya wenzetu na ya waliotangulia. Kuna kesho.