Na Safina- Sarwatt, Rombo
Viongozi wa Vyama Shiriki vya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Mkoa wa Kilimanjaro wameitaka serikali ifanye marekebisho ya Sheria za Mashirika ya Umma na Makapuni ili yaingize suala la ushirikishwaji katika vyombo vyake vya maamuzi.
Aidha, amesema TUCTA inaitaka serikali kubadilisha baadhi ya vifungu kandamizi kwa wafanyakazi, ikiwemo Sheria ya ajira na mahusiano kazini Na. 6 ya mwaka 2004 na kanuni zake za mwaka 2007, ambazo bado zimeonekana kuwa mwiba kwa wafanyakazi.
Hayo yamesemwa juzi Mei 1,2021 na Katibu wa Chama Cha Walimu Mkoa wa Kilimanjaro (CWT), Digna Nyaki, wakati akisoma risala ya Wafanyakazi kwa mgeni rasmi wakati wa Maadhimisho ya Sherehe za Wafanyakazi ambazo Kimkoa zilifanyika Wilayani Rombo.
“Tunaitaka serikali ione kuwa ipo haja ya kufanya marekebisho ya haraka kwa Sheria hii kandamizi, kwa mfano katika mahesabu ya kisheria ya kiinua mgongo, leo hii kwa mtu ambaye ajira yake inafikia ukomo hulipwa mshahara kwa siku Saba, tunaiomba serikali walau hesabu hiyo iwezekufika angalu mshahara kwa mwezi mara miaka aliyofanya kazi isiyozidi kumi na si kama ilivyo sasa,”alisisitiza Mwl Nyaki.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Mkoa, Mshikizi Onesmo Buswelu, amewataka wafanyakazi kuhakikisha kwamba wanaendelea kuisaidia serikali, kukusanya mapato kwa wingi ili kukuza uchumi wa nchi sanjari na kuweza kuongeza mishahara ya watumishi.
Buswelu amesema Serikali ipo kwenye jitihada za kuhakikisha maslahi bora kwa wafanyakazi yanapewa kipaumbelea licha ya kwamba yapo mambo muhimu yaliyoanza kufanyiwa kazi, ikiwemo ujenzi wa miundo mbinu ya Barabara, Afya, Elimu na Maji.
“Kila mfanyakazi anao wajibu wa kujituma kufanya kazi kwa bidii ili mishahara iweze kuwa juu hivyo ni lazima site kama Watanzani tushirikiane kuipa nguvu serikali katika kukusanya mapato yake ambaye anastahili kulipa kodi aweze kuilipa,”amesema.
Sherehe za Mei Mosi, huadhimishwa na wafanyakazi kote duniani Kila mwaka ikiwa Ni kumbukumbu ya kuwakumbuka wafanyakazi wenzao waliojitoa mhanga na kupoteza maisha yao kwa ajili ya kupigania Haki, Maslahi na Hali bora za Kazi.