29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

TSHISHIMBI HATIHATI KUIVAA MBEYA CITY

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

KIUNGO wa Yanga, Pappy Tshishimbi, huenda asiichezee timu hiyo itakapoumana na Mbeya City, katika pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara litakalopigwa Jumapili hii  baada ya jana kuumia.

Tshishimbi aliumia kifundo cha mguu ‘enka’ akiwa kwenye mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Kiungo huyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), alishindwa kumaliza  mazoezi hayo licha ya awali kupatiwa huduma ya kwanza na daktari wa Yanga, Edward Bavu, kisha kurejea uwanjani.

Akizungumza na MTANZANIA baada ya mazoezi hayo kumalizika, Bavu alisema Tshishimbi hakupata majeraha makubwa, hivyo wanamtarajia leo ataendelea na mazoezi kama kawaida.

“Tshishimbi aliumia maeneo ya mguu, hali hiyo imetokana na kiatu alichovaa pamoja na uwanja ulivyo, hivyo alishindwa kuendelea na mazoezi nikaamua kumpumzisha, lakini kesho anaweza akaendelea na mazoezi,” alisema.

Endapo hali ya afya ya Tshishimbi itashindwa kutengemaa kwa wakati, kuna uwezekano kocha wa timu hiyo, George Lwandamina, akamtumia Said Makapu kucheza eneo la kiungo mkabaji.

Katika mazoezi hayo, Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, alitengeneza vikosi viwili; kimoja kikiundwa na wachezaji wakongwe huku kingine kikiwa na mchanganyiko wa wakongwe na vijana.

Kikosi cha kwanza kilikuwa na Ramadhani Kessy, Andrew Vincent, Nadir Haroub ‘Canavarro’, Juma Makapu/Matheo Antony, Pius Buswita, Raphael Daud, Pappy Tshishimbi/Juma Mahadhi,  Obrey Chirwa, Ibrahim Ajib, Maka Edward na Beno Kakolanya.

Kikosi cha pili kiliundwa na Pato Ngonyani, Juma Abdul, Abdallah Shaib ‘Ninja, Said Juma, Ramadhan Kabwili/Youthe Rostand na baadhi ya wachezaji wa kikosi cha vijana cha Yanga.

Baada ya kuunda vikosi hivyo, ilipigwa bonge la mechi ambapo Ajib, Buswita na Maka walipachika bao moja kila mmoja na kuupa upande wao ushindi wa mabao 3-0.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, akizungumzia mchezo wao na Mbeya Cuty, alisema wanafahamu wanakutana na timu yenye kocha mpya hivyo wana kila sababu ya kujiandaa kikamilifu ili wavune pointi tatu.

“Wachezaji wanaendelea vizuri isipokuwa Thaban Kamusoko na Donald Ngoma ambao ni majeruhi na Amiss Tambwe ambaye ameanza mazoezi, hawa  ndio wataukosa mchezo huu lakini  wengine wako fiti,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles