25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

TSC Queens waibuka mabingwa Bonanza la Mei Mosi

Na Veronica Simba – TSC

Timu ya Mpira wa Pete kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC Queens), imetwaa ushindi wa kwanza katika bonanza maalum la michezo kwa Taasisi za Serikali, lililofanyika Aprili 24, mwaka huu, jijini Dodoma.

TSC Queens ilitwaa ushindi huo baada ya kuwabwaga washindani wao kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa waliochuana nao vikali katika ngazi ya fainali kwa magoli 25 kwa moja.

Wachezaji wa Timu ya Mpira wa Pete kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC Queens) wakiwa katika pozi la ushindi baada ya kuichakaza Timu kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa mabao 25 kwa 01, katika fainali za Bonanza la Michezo ya Mei Mosi lililoshirikisha Taasisi mbalimbali za Serikali, Mkoa wa Dodoma, Aprili 24, 2021.

Awali, Timu hiyo machachari ilipambana na Timu kutoka Wizara ya Fedha na kufanikiwa kuwachakaza mabao 29 kwa 05, hatua iliyowawezesha kufuzu kuingia ngazi ya fainali.

Akizungumzia siri ya ushindi huo wa kishindo, Mlezi wa TSC Queens ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimaliwatu, Shani Kamala alisema ni kutokana na kujituma katika kufanya mazoezi ya mara kwa mara.

“TSC tunathamini michezo kwani tunaamini ina mchango mkubwa katika kujenga afya za watumishi wetu. Ndiyo maana sisi kama viongozi tumeweka mikakati ya kuhakikisha watumishi wanafanya mazoezi mara kwa mara na kushiriki katika michezo mbalimbali,” alifafanua.

Wakati huohuo, Timu ya Mpira wa Miguu kutoka TSC (TSC Sports Club) waliibuka washindi wa tatu baada ya kuwachabanga mikwaju 5 ya Penalti wapinzani wao ngazi ya nusu fainali, Timu kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa ambao waliambulia mikwaju 2 tu.

Dafroza Luhwoga ambaye ni mchezaji wa Timu ya Mpira wa Pete kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC Queens), akifunga goli wakati wa mchezo wa fainali baina ya timu hiyo na wapinzani wao kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa. TSC Queens ilishinda kwa mabao 25 kwa 01. Mashindano hayo yalifanyika Aprili 24, wakati wa Bonanza la Michezo lililoshirikisha Taasisi mbalimbali za Serikali Mkoa wa Dodoma.

Kwa upande wake, Kapteni wa TSC Sports Club, Bitwalihat Magota amesema kikosi chake Kiko vizuri isipokuwa wanahitaji kuongeza zaidi mazoezi na mbinu za kimchezo.

Bonanza hilo liliandaliwa na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE), Mkoa wa Dodoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani maarufu kama Mei Mosi, ambayo huadhimishwa tarehe moja ya kila mwezi Mei.

Kikosi cha Mpira wa Miguu kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC Sports Club), kikiwa uwanjani muda mfupi kabla ya kuchuana na Timu kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa katika Bonanza la Michezo ya Mei Mosi lililoshirikisha Taasisi mbalimbali za Serikali Mkoa wa Dodoma, Aprili 24, 2021.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles