25.5 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Trump, Putin, Erdogan wanapolazimika kushirikiana

recep-tayyip-erdogan-2-505x359
Erdogan

 

WAWILI kati yao wanaoongoza nchi zao kwa mkono wa chuma kwa misimamo isiyoeleweka inayobadilika kila mara kutokana na hulka na mazingira ya kisiasa kwenye nchi zao Rais Vladimir Putin wa Urusi anatikisana na mahasimu wake wa nchi za Magharibi akichekeana nao kinafiki, katika maeneo yanayorindima mapigano ikiwemo Syria anakomkingia kifua Rais Bashar al-Asaad ambaye anatishiwa kung’olewa madarakani na waasi wanaosaidiwa na Marekani.

Katikati ya mkanganyiko huo ni kundi la kigaidi la ISIS linalowindwa na Marekani lakini pia likimshambulia Asaad kutokana na msimamo wa kiimani lakini pia Putin anasigana na Ukraine aliyoipoka jimbo la Crimea.

Mwingine ni Rais Recip Tayyip Erdogan wa Uturuki aliyeahidiwa ‘mafao’ kwa kukinga wahamiaji haramu wasiingie Ulaya, akitumika pia kwa mashambulizi dhidi ya IS naye akiwadunda waasi wa PKK wa Kikurd waliopo Uturuki na Iraq, aliyezozana na Urusi alipoitungua ndege vita ya nchi hiyo iliyovuka kutokea Syria.

Urusi ilighadhibika na kuiwekea vikwazo Uturuki lakini jaribio la mapinduzi ya kijeshi alilonusurika Erdogan, anayemtuhumu hasimu wake Fethullah Gulen anayeishi ukimbizini nchini Marekani na kusuasua kutimizwa ahadi za Magharibi kwa nchi yake, kumemlazimisha atafute maelewano na Urusi na kuyakera mataifa ya Magharibi yanayohisi amewasaliti kwa kumkumbatia Putin.

Mtu wa tatu ni Donald Trump anayetafuta urais wa Marekani ambaye anafahamika kwa kauli zake tata naye anaingia katika jopo la watatu hao watatanishi katika siasa za kimataifa.

Trump aliwahi kutoa matamshi makali awali Urusi ilipomega jimbo la Crimea mnamo Machi 2014, akimshutumu Rais Barack Obama kuwa ni dhaifu ndiyo maana anashindwa kuikinga Ukraine akataka nchi za Magharibi zimchukulie hatua kali Rais Putin kwa kitendo chake lakini kadiri siku zinavyoenda amebadili msimamo na anafikiria kuiondolea Urusi vikwazo ilivyowekewa kwa kuivamia Crimea, ikiwa ataingia Ikulu na huenda akatambua kuwa Crimea ni sehemu halali ya Urusi.

GOP 2016 Debate
Trump

 

Haieleweki hasa kilichosababisha mabadiliko ya msimamo wa Trump kuhusiana na suala hilo lakini inasemekana kuwa, ushirikiano wake na watendaji wake wengi kwenye timu yake ya kampeni wanaoipendelea Urusi ndiyo sababu ya mabadiliko hayo, akiwamo Meneja wake wa kampeni, Paul Manafort ambaye awali alikuwa msaidizi wa Rais wa zamani wa Ukraine Viktor Yanukovych mwenye mlengo wa Urusi aliyepinduliwa na kuingia madarakani, Rais wa sasa Petro Poroshenko ambaye anaelemea upande wa Magharibi. Katika kutetea mabadiliko ya msimamo wake Trump ameibuka na hoja mbadala kwamba anadhani watu wa Crimea wanapendelea kuwa upande wa Urusi kuliko Ukraine.

Ameagusia kura ya maoni iliyofanyika mnamo mwaka 2014 ambapo asilimia 95.5 ya wakazi wote wa Crimea waliopiga kura, waliunga mkono jimbo hilo liwe chini ya uangalizi wa Urusi ingawa wengi walisusia upigaji kura huo ambao jumuiya ya Ulaya ilisema si halali kwamba ni uhuni wa kisiasa, lakini Trump anashadadia hoja yake mpya kwamba kuibinya Urusi ili ijiondoe Crimea kijeshi ni sawa na kutaka kuanzisha fukuto la vita kuu ya tatu ya dunia.

Kinachokanganya zaidi kuhusu utatu usioeleweka baina ya Trump, Putin na Erdogan ni ziara ya hivi karibuni ya Rais Erdogan nchini Urusi ambaye nchi yake na Urusi walikuwa mahasimu waliotupiana shutuma siku chache tu zilizopita, ambaye katika mazungumzo yake rasmi na mwenyeji wake Rais Putin waliitana kiswahiba ‘rafiki yangu mpendwa’ na sasa mahasimu hao wa zamani wanaelekea kuwa na msimamo mmoja kuhusu Syria, kwamba si lazima Rais Asaad aachie madaraka ili mazungumzo ya amani yafanyike kama nchi za Magharibi zinavyotaka, ukiwa ni msimamo mpya mbadala wa Uturuki.

Inavyoelekea kilichomsukumia Erdogan kwa Putin ni kutelekezwa na NATO hususan kuhusu jaribio la mapinduzi alilonusurika, pia msimamo wa Marekani kukataa kumkabidhi Gulen anayeshutumiwa kupanga mapinduzi hayo yaliyofeli.

Urusi iliyopewa karata turufu ya kujijenga dhidi ya nchi za Magharibi kwa Uturuki kuelemea upande wake, inasubiri turufu nyingine ikiwa Trump atafanikiwa kuingia madarakani kwani ameshatamka kuwa hana mpango wa kuibinya kuhusu Crimea. Ni mkanganyiko utakaojitanzua wenyewe kadiri siku zinavyopita!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles