27.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 5, 2023

Contact us: [email protected]

Magufuli anajichelewesha mwenyewe

Rais John Magufuli
Rais John Magufuli

NA PETER MITOLE,

WIKI iliyopita niliandika makala ambayo baadhi ya watu walidhani ililenga kumtetea Rais John Magufuli kutokana na tuhuma kuwa anaiendesha nchi kidikteta. Sikuwa na maana wala dhamira hiyo.

Nilicholenga kuonyesha ni kuwa tunaweza kuwa na tatizo na badala ya kuangalia mzizi wa tatizo, sisi tunakimbilia kuangalia pembeni. Na kwa namna hiyo, hatuwezi kamwe kutatua kwa uhakika tatizo hilo. Tunaweza kulipatia ufumbuzi wa muda au wa juu juu tu.

Ni kweli Rais Magufuli anaweza kuwa na udikteta ndani yake, lakini ni ukweli pia anayo nafasi ya kikatiba kuutekeleza udikteta huo, kama kweli anautekeleza.

Nilichomaanisha katika makala ile ni kuwa iwapo hatutauangalia mfumo wa utawala nchini, itakuwa vigumu sana kuwanasa watu ambao watautumia vibaya na hilo lilithibitishwa zamani na kauli ya Mwalimu Nyerere kuwa katiba yetu inaweza kumfanya rais awe dikteta kwa kutekeleza yale yaliyomo kwenye katiba hiyo.

Leo naandika nikimgeukia Rais Magufuli na kumwomba aichanganue ile kauli yake kuwa hataki kucheleweshwa kwenye safari yake ya kuwaletea Watanzania maendeleo.

Ameitoa kauli hii ili kuhalalisha agizo lake la kukataza kazi za kisiasa akieleza kuwa harakati za wanasiasa, hasa wa upinzani, ambao wanapenda kufanya maandamano na mikutano, zitachelewesha kasi yake ya kuleta maendeleo kwa sababu watu watapoteza muda mwingi huko kwenye maandamano na mikutano.

Kwa jinsi anavyoitoa kauli hii, Rais Magufuli anaonyesha kuwa mikutano ya kisiasa na maandamano si vitu muhimu wakati huu. Kinachoshangaza ni kuwa kwanza anatoa kauli hii kwenye mikutano. Hapa anathibitisha kuwa kama si hiyo mikutano, angelazimika kutumia njia nyingine kuifikia hadhira yake.

Lakini kwa upande mwingine, wakati yeye anaona vyama vya upinzani vinachelewesha safari yake ya maendeleo, lakini ukweli ni kuwa wapinzani  hao ndio wanaweza kuiharakisha safari hiyo. Mawazo mbadala yanayotolewa na wapinzani wanapoikosoa Serikali, yanaweza kutumika kuboresha mipango ya Serikali na kuleta kasi zaidi ya utekelezaji.

Kwa jinsi anavyofanya, inaonyesha kuwa Rais Magufuli anaamini kuwa yeye na Serikali yake wana kila jibu la matatizo yanayowakabili Watanzania. Haya si mawazo sahihi sana.

Cha kukumbuka hapa ni kuwa vyama vya upinzani vilianzishwa kisheria na moja kati ya dhima yake kubwa ni kutoa changamoto kwa chama na Serikali iliyopo madarakani.

Kwa maana hiyo, mtawala mzuri anaweza kuwatumia wapinzani kama chanzo cha mawazo ya jinsi ya kuboresha utendaji na mipango ya Serikali.

Tukumbuke kuwa kila mara, wapinzani wamekuwa wakiifanya kazi hii. Kwa msikilizaji mzuri atapata mchango mkubwa sana kutoka kwa wapinzani.

Ni hatari sana kuamini kuwa kile unachokifahamu wewe tu ndicho sahihi na hakihitaji kukosolewa au kupatiwa nyongeza na wengine, hasa linapokuja suala la kuongoza nchi.

Wapinzani ni kati ya watu ambao Rais Magufuli anapaswa kuwaongoza na ni jambo jema kwa kiongozi kusikiliza anaowaongoza wana mawazo gani hata kama mawazo hayo ni ya kipuuzi.

Lakini kwa upande mwingine wapinzani hawa wapo kisheria na wana wajibu na haki. Wajibu wao ni kuikosoa Serikali. Ili watekeleze wajibu huu wanapaswa kupatiwa nafasi na fursa ya kufanya hivyo na mikutano ya hadhara ni moja kati ya nafasi hizo.

Kuwazuia wapinzani wasitoe maoni mbadala kupitia mikutano ya hadhara ni sawasawa na kujizuia wewe mwenyewe usipate mawazo mbadala. Kwa hiyo amri ya Rais Magufuli ya kupiga marufuku shughuli za kisiasa kwa wapinzani ni sawa na yeye kujichelewesha mwenyewe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles