26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Trump atuma wanajeshi 5,200 kuzuia wahamiaji

                                       WASHINGTON, MAREKANI



SERIKALI ya Marekani imesema inawatuma wanajeshi 5,200 kusaidia kulinda mipaka kati yake na Mexico, baada ya maelfu ya wahamiaji kutoka mataifa ya Amerika ya Kati kujiunga na msafara wa wahamiaji wanaopania kufika Marekani.

Hilo linakuja huku Rais Donald Trump akidai anapanga kusaini amri ya kirais kuhitimisha haki ya uraia kwa watoto wanaozaliwa na wasio raia au wahamiaji nchini hapa.

“Sisi ni nchi pekee duniani ambako mtu anakuja na ana mtoto, na mtoto anakuwa raia wa Marekani. Huu ni upuuzi na unapaswa kukoma,” alisema Trump katika mahojiano yaliyotolewa jana.

Hata hivyo madai ya Trump kwamba Marekani ni nchi pekee duniani kutoa haki ya uraia wa kuzaliwa kwa watoto si ya kweli.

Wakati akiwa sahihi kuwa nchi za Ulaya zinahitaji kipindi cha ukazi kabla ya kutoa uraia kwa wale wanaozaliwa na wazazi wa kigeni, mataifa mengi ya Amerika kama vile Canada, Mexico, Brazil na Argentina yana mfumo sawa na Marekani wa haki ya uraia wa kuzaliwa.

Kauli hizo za Trump na suala la kutuma askari mpakani inaonwa kama sehemu ya kampeni ya kukibeba chama chake kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula utakaofanyika Novemba 6.

Idadi hiyo ya wanajeshi wanaotumwa kuulinda mpaka ni kubwa kuliko ilivyotarajiwa huku Trump akizidi kuwa na misimamo mikali kuhusu uhamiaji kuelekea chaguzi hizi.

Jenerali Terrrence O’ Shaughnessy, anayesimamia kambi ya wanajeshi walioko kaskazini mwa Marekani alisema wanajeshi 800 tayari wako njiani kueleka mpaka wa Texas na wengine wanaelekea katika mipaka ya California na Arizona.

O’Shaugnessy alisema Rais Trump ameweka wazi kuwa ulinzi wa mipaka ni jambo la usalama wa kitaifa.

Huku hayo yakijiri, mamia ya wahamiaji kutoka Honduras wamevuka mto kuingia Mexico, hilo likiwa kundi jipya la wahamiaji wanaoelekea Marekani.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN) zaidi ya wahamiaji 7,000 wako njiani kuelekea Marekani.

Katika kampeni za uchaguzi wa rais mwaka 2016, Trump alitumia suala la uhamiaji haramu kama moja ya ahadi atakazozipa kipaumbele akiingia madarakani.

Na sasa anatumia suala la msafara wa wahamiaji kutoka mataifa ya Amerika ya Kati kukipigia debe chama chake cha Republican katika uchaguzi wa katikati ya muhula.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles