23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

TRUMP APITISHA KWA KAGAME SALAMU ZAKE KWA WAAFRIKA

DAVOS, USWISI

RAIS wa Marekani, Donald Trump, amemwomba Rais wa Rwanda, Paul Kagame ambaye kwa sasa ndiye atakayekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), kufikisha salamu zake kwa viongozi wengine wa mataifa wanachama wa umoja huo.

Viongozi hao wawili walikutana na kuzungumza jana mjini Davos, Uswisi pembezoni mwa Kongamano la Kiuchumi la Dunia (WEF) linalokutanisha viongozi na wafanyabiashara wakubwa duniani.

“Ningependa kukupongeza, Bwana Rais, unapochukua majukumu ya kuwa kiongozi mpya wa Umoja wa Afrika, ni heshima kubwa … najua unaenda kuhudhuria mkutano wa kwanza karibuni. Tafadhali, fikisha salamu zangu.”

Mkutano huo wa Kagame na Trump umekuja ikiwa ni wiki chache baada ya kiongozi huyo wa Marekani kudaiwa kuyaeleza mataifa ya Afrika kama “machafu” au mataifa ya “mabwege”.

Hatua hiyo ilimfanya Trump ashutumiwe vikali na viongozi wa AU na baadhi ya viongozi wa nchi za Afrika kama vile Botswana na Ghana.

Ingawa Trump alikanusha kwamba alitumia neno hilo kuyaelezea mataifa ya Afrika, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, aliunga mkono kauli hiyo na kummwagia sifa Trump kwa kuwa mkweli.

“Ninampenda Trump kwa sababu anasema ukweli mtupu, Waafrika wanatakiwa kusuluhisha matatizo yao wenyewe, Waafrika ni dhaifu sana,” alisema Museveni wiki hii wakati akifungua Bunge la Afrika Mashariki mjini Kampala.

Trump mwenyewe licha ya kukanusha kutamka maneno hayo, alikiri kutumia maneno makali kuyaelezea mataifa ya Afrika, Haiti na El Salvador, alipokuwa anazungumzia wahamiaji wanaoingia Marekani.

Waandishi wa habari walioko mjini Davos, wanasema hata hivyo katika mkutano wake na Kagame, Trump hakuonyesha dalili zozote za majuto kuhusu tamko lake la awali kuhusu Afrika.

Zaidi wanasema Trump alikataa kujibu maswali ya waandishi waliokuwa wakipaza sauti kutaka azungumzie kauli yake kwamba mataifa ya Afrika ni machafu.

Pamoja na kuonekana kukataa kuzungumzia jambo hilo, Trump alijikita zaidi kuelezea mkutano wake na Kagame kama “wa kufana sana”.

Pia alielezea uhusiano baina ya nchi hizo mbili akisema ni washirika wa kibiashara ambao wanajivunia ‘uhusiano mzuri sana’.

Kwa upande wake Rais Kagame alisema wameshauriana kuhusu ushirikiano wa nchi hizo mbili, ikiwa ni pamoja na usaidizi wa Marekani kwa Rwanda katika “operesheni zake kote duniani”, pamoja na masuala ya kiuchumi, biashara, uwekezaji na idadi ya watalii wa Marekani wanaozuru Rwanda ambayo inaongezeka.

Kagame amekutana na Trump katika wakati ambao mkutano wa viongozi wa nchi wanachama wa AU unatarajia kufanyika kesho na keshokutwa.

Kagame anakuwa kiongozi wa tatu kukutana na kufanya mazungumzo na Trump baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Viongozi wengine kutoka Afrika waliohudhuria kongamano hilo ambalo jana lilijikita kuzungumzia masuala ya biashara na uchumi duniani, ni Waziri Mkuu wa Somalia, Hassan Ali Khayre, Makamu wa Rais Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa na rais mpya wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles