WASHINGTON, MAREKANI
RAIS Donald Trump, ameonekana kuguswa na tetesi kuwa muigizaji nguli wa Marekani, Oprah Winfrey anaweza kuwa mpinzani wake mwenye nguvu katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2020.
Rais Trump amesema itakuwa furaha kwake kutetea wadhifa wake dhidi ya Oprah, ambaye pia amepata kuwa mtangazaji maarufu wa televisheni nchini humo.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mkutano kujadili mabadiliko ya sheria za uhamiaji na maseneta wa Marekani, Rais Trump alisema ana uhakika wa kumshinda Oprah iwapo atajitokeza kupambana naye.
Opray ambaye alitoa hotuba wakati wa utoaji wa tuzo za Golden Globe iliyoegemea zaidi katika umuhimu wa kukabiliana na ukosefu wa usawa wa kijinsia, hotuba yake hiyo ilisifiwa na na Wamarekani wengi kutoka pande mbalimbali za nchi hiyo.
Ivanka Trump, ambaye ni mtoto wa kike wa Trump naye alisifia hotuba ya Oprah wakati wa utoaji wa tuzo za Golden Globe.
Hata hivyo, watu wa karibu na Oprah wamesema muigizaji huyo hana mpango wa kutangaza kuwania urais mwaka 2020.
Katika mkutano wake wa juzi na waandishi wa habari, Trump alisema kuwa kukutana na Opray katika kampeni za kuwania urais litakuwa jambo la kufurahisha sana.
“Nilishiriki baadhi ya vipindi vyake vya mwisho. Nampenda Oprah lakini sidhani kwamba atawania urais, akiogombea, ndio nitamshinda Oprah,” alisema Trump.
Akihojiwa na mtangazaji wa CNN, Larry King wa mwaka 1999, Trump alisema iwapo angewania urais angemchagua Opray kuwa mgombea mwenza.
“Oprah ninampenda, atakuwa chaguo langu la kwanza. Iwapo atawania itakuwa vyema. Ni mtu maarufu, ni mtu mwenye kipaji na mwanamke mzuri sana,” alikaririwa akisema.
Trump alirejea tena kauli hiyo mwaka 2015, wiki moja kabla ya kutangaza kuwa atawania urais alipoeleza kuwa angependelea kumchagua Oprah kuwa makamu wake wa urais.