25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

SIRI MKATABA AIRTEL YAFICHUKA

  • Ni baada ya ripoti ya uchunguzi kutua kwa JPM

Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amewasilisha taarifa ya Kamati ya Uchunguzi kuhusu sakata la umiliki wa Kampuni ya simu ya Airtel kwa Rais Dk. John Magufuli.

Kukabidhiwa kwa ripoti hiyo, kumetokana na agizo la Rais Magufuli alilolitoa Desemba 20, mwaka jana, akimtaka Waziri wa Fedha na vyombo vingine vya usalama kufanya uchunguzi huo.

Akiwasilisha ripoti hiyo Ikulu Dar es Salaam jana kwa Rais Magufuli, Waziri Mpango, alisema kuwa Serikali imejiridhisha kuwa ubinafsishaji wa Shirika la Simu Tanzania (TTCL) kwenda Celtel, baadaye kuhamishiwa Zain na sasa Airtel ulifanyika kwa ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na taratibu.

Kutokana na hali hiyo, Dk. Mpango, alisema Serikali inayomiliki asilimia 40 ya hisa za Airtel, imeamua kufanya mazungumzo na kampuni hiyo inayomiliki asilimia 60 ya hisa ili nchi iweze kupata haki yake.

“Lakini niwaambie Watanzania yale ambayo tumeyaona ni machafu sana, ni mambo ya ovyo kabisa, nchi yetu kwa kifupi tuliingizwa mkenge, ni fedha nyingi zimepotea, kwahiyo sisi katika majadiliano haya lengo letu litakuwa ni kuhakikisha Watanzania wanapata haki yao,” alisema Dk. Mpango.

UCHUNGUZI AKAUNTI ZA AIRTEL

Desemba 30, mwaka jana, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), nayo ilijitosa kwenye uchunguzi wa akaunti zote za Airtel.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Benki wa benki hiyo, Kened Nyoni, baadhi ya benki zinazomiliki akaunti za fedha za Kampuni ya Airtel Tanzania, zimetii agizo la kuwasilisha taarifa za uendeshaji wa akaunti hizo.

Akizungumza pasipo kutaja idadi ya benki hizo, Nyoni, alisema agizo hilo limezingatiwa na kinachofanyika sasa ni kuchambua ili kujua idadi ya zisizotii.

Nyoni alisema benki zinazomiliki akaunti za Airtel Tanzania ni nyingi.

“Zipo benki nyingi na baadhi zimezingatia agizo letu tulilolitoa, kwahiyo ni vigumu kukutajia idadi kwa sasa ila jambo la msingi ni kwamba uchambuzi unaendelea ili kubaini benki ambazo hazijawasilisha taarifa tunazozihitaji,” alisema.

BoT iliziagiza benki zilizo na akaunti za fedha zinazomilikiwa na Airtel Tanzania, kuwasilisha taarifa za uendeshaji wake.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenda kwa taasisi hizo za fedha na kusainiwa na Nyoni, BoT inahitaji kupitia hesabu zote za uendeshaji wa akaunti za fedha zinazohusisha kampuni za simu za Celtel, Zain na Airtel ili iweze kufanya ukaguzi.

Pia taarifa hiyo ilisema BoT ilikuwa inahitaji taarifa za akaunti zote za kampuni hizo kwa mara moja kuanzia Januari mosi, 2000 hadi Desemba 27, mwaka jana (miaka 17) na zinatakiwa kuwasilishwa katika mifumo miwili tofauti ya nakala (hard copy na soft copy).

Nyoni, alikiri kwamba wameomba taarifa za akaunti zote za Airtel katika benki na taasisi nyingine za fedha.

Hatua ya BoT kufanya ukaguzi wa hesabu za Airtel, imekuja baada ya kauli ya Rais Magufuli, kumtaka Dk. Mpango, kufuatilia kwa karibu umiliki wa Airtel kabla ya mwaka huu kuisha kwa kuwa taarifa alizonazo ni kwamba kampuni hiyo ni mali ya TTCL.

BODI YA WAKURUGENZI YA TTCL

Siku moja baada ya Magufuli kutoa agizo hilo, Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL kupitia kwa Mwenyekiti wake, Omary Nundu, ilijitokeza na kuitaka Airtel kukabidhi mali za kampuni hiyo kwao kwa kuwa ndio wamiliki halali kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

Alisema Airtel ambayo ilisajiliwa Novemba 3, 1998 na uongozi wa TTCL kwa mtaji wa Sh bilioni 200 kwa jina la Celnet iliuzwa kijanja na waliokuwa viongozi wa Bodi ya TTCL.

Nundu alisema kupatikana kwa kampuni hiyo ambayo ilikuwa chini ya TTCL, kulitokana na kuvunjwa na kugawanywa kwa lililokuwa Shirika la Posta na Simu  Desemba 1993.

Alisema baada ya mgawanyiko huo, TTCL ikawa kampuni ya Serikali ikiwa na mtaji wa Sh bilioni 200.

“Julai 21,1999 baada ya miaka sita, thamani ya hisa za TTCL zikapanda kutoka bilioni 200 mpaka bilioni 600, baadae Februari 23, 2001 likaja wazo la kubinafsishwa TTCL, akajitokeza mtu anaitwa MSI Cellular Investment ,” alisema Nundu.

TAKUKURU

Kutokana na hali hiyo, nayo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ilitangaza kujitosa kwenye uchunguzi wa uuzwaji huo wa Airtel kutoka TTCL.

Msemaji wa Takukuru, Mussa Misalaba akinukuliwa na MTANZANIA, alisema taasisi hiyo imeishaanza uchunguzi na baadaye wahusika wote watafikishwa mahakamani.

“Tupo tunafuatilia, tumeanza kulifanyia kazi suala hili mara tu baada ya agizo la Rais Magufuli, lakini kwa sasa hatutasema tunawachunguza watu wangapi na wala hatutawataja majina kwa sababu tunahofia kuharibu uchunguzi wetu,” alisema.

Alisema baada ya uchunguzi huo, wahusika watafikishwa katika vyombo vya kisheria ili kujibu tuhuma husika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles