26.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Trump alalamika kuhujumiwa

trump

Na Augustino Malinda, New York

JAPO ishara zilionyesha kushindwa kwa tofauti kubwa ya kura kwa mgombea urais wa Chama cha Republican, Donald Trump lakini matukio ya wanawake  zaidi ya saba kutokea hadharani na madai ya kudhalilishwa kijinsia yameharibu kabisa mweleko mzima wa kampeni za mgombea huyo.

Kuna vita nne zinazopiganwa kisiasa hadi sasa katika uchaguzi huu. Ni vita ya Trump dhidi ya Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, ambapo wamejitokeza wanawake wanaomtuhumu, viongozi wa chama chake na vyombo vya habari hali ambayo wataalamu wa siasa wanaona ni mwanzo wa mwisho wa kampeni za kuingia Ikulu na sasa yuko katika kampeni za kutetea umaarufu wake tu.

Kutokana na mfululizo wa matukio ya wanawake kujitokeza hadharani yaliyoanza Jumatano iliyopita pale alipodai atamshambulia Bill Clinton ambaye ni mume wa mgombea urais wa Chama cha Democratic, Hillary Clinton kwa tuhuma za udhalilishaji wa wanawake.

Licha ya kuonywa mara kwa mara na  wakongwe wa siasa za Marekani akiwemo aliyewahi kuwa Spika na mgombea wa urais wa chama cha Republican, Newt Gingrinch lakini Trump alisimamia azma yake ya kumbomoa Clinton.

Akihojiwa na Televisheni ya Fox News, Gingrinch, alisema haikuwa busara kumuingiza Bill Clinton katika kampeni hizo na kuwa anafunguwa mlango wa yeye naye kushambuliwa.

Gingrinch anamfahamu Clinton kwa kuwa ndiye aliyeitisha Bunge kumshitaki na kutaka kumvua urais wakati wa skendo ya Monica Lewinsky, lakini yaliyomkuta yamekuwa somo kubwa kwake kwa kuwa alishindwa kumuondoa ila yeye alipoteza uspika na kufumuliwa siri zake za kuchepuka nje ya ndoa.

Trump kwa majigambo alikataa ushauri huo na kudai ifikapo leo jumapili ambayo ni siku ya mdahalo atakuwa ameshammaliza Bill Clinton kwa kuwaleta washitaki wake.

Siku mbili baadaye mkanda wa video akizungumza maneno yasiyo mazuri kwa mke wa mtu na mwigizaji wa Tamthiliya ya ya Days of Our Lives, Arriane Zucker, ulianza kusambaa na kusababisha mwelekeo wa kampeni kubadilika rasmi. Sasa kampeni za Trump zimepoteza matumaini ya kuingia Ikulu.

Mwanamke mwingine aliyewahi kuwa katika kipindi chake cha Apprentice Summer Zervos naye amejitokeza akidai amedhalilishwa kijinsia na mgombea huyo  na tayari ameshapata wakili wa kumshitaki Trump ambaye ni mwanasheria maarufu anayewashitaki watu mashuhuri, Gloria Allred. Mwanadada huyo anadai alidhalilishwa na Trump katika hoteli kwa ahadi ya kupatiwa kazi nzuri.

Viongozi, wabunge na maseneta wa Republican wameanza kumkimbia Trump. Wiki iliyopita pekee Seneta Mark Kirk wa Jimbo la Illinois alitangaza kutompigia kura Trump na kuwataka wabunge na maseneta kujitokeza hadharani.

Wengine waliotangaza kutomuunga mkono ni Seneta John McCain, Gavana John Kasich (Seneta Portman wote wa Ohio), Kelly Ayotte (New Hampshire) na Crapo wa Idaho. Hadi sasa wabunge zaidi ya saba wametangaza kutomuunga mkono Trump.

Magazeti kadhaa yametaka ajitoe kugombea urais lakini katika hali iliyotarajiwa na wengi, Trump amedai hatajitoa na kwamba kushambuliwa kwake ni mbinu za Clinton na kampuni mbalimbali za kimataifa ili yaitawale vizuri Marekani kwa kuwa yeye ni mkombozi.

Katika kura za maoni ambazo zimetolewa  Ijumaa na Televisheni ya NBC na Fox News zinaonyesha Hillary anaongoza kwa kura za uwakilishi 287 akiwa amevuka idadi inayotakiwa ya kura 270 na Trump ana kura za uwakilishi 150.

Katika historia ya uchaguzi wa urais nchini  Marekani unaotarajiwa kufanyika Novemba 8 mwaka huu, hakuna mgombea ambaye yuko nyuma kwa kura za maoni kama Trump alivyo sasa akashinda, na viongozi mbalimbali wa Republican wameshaanza kujiandaa kupoteza urais na hivyo kujikita wakitetea viti vya ubunge na useneti.

Timu ya kampeni ya Trump  imesimamisha matangazo na kuondoa  wafanyakazi wake katika majimbo ya Virginia na South Carolina.

Katika vita yake na wanawake wanaomtuhumu, Trump amedai  kutowajua na kudai kuwa mataifa na kampuni ya nje yanawatumia ili asiwe rais wa marekani, katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika Charlotte, amedai ataleta ushahidi wa kuonyesha kuwa washitaki hao ni waongo, hata hivyo alimleta shahidi Mwingereza Anthony Gilberthorpe aliyedai kuwapo katika ndege  siku ya tukio miaka zaidi ya 25 iliyopita, hata hivyo shahidi huyo alibainika kuwa ni muongo na amekuwa na tabia ya kusingizia viongozi na wanasiasa maarufu nchini Uingereza, ikiwamo tukio la kusingizia  baadhi ya wanasiasa hukodisha wapenzi wa kiume wenye umri mdogo.

Trump pia ametishia kulipeleka mahakamani gazeti kubwa na maarufu nchini hapa la New York Times kama lisipokanusha habari ilizoandika kuhusu washitaki wa kike, tayari gazeti hilo limekataa na kumtaka afungue mashitaka likidai lina ushahidi wa kutosha kuwa ni kweli aliwadhalilisha wanawake hao.

Katika hotuba zake mbalimbali tangu matukio ya wanawake kumtuhumu, Trump amekuwa akishambulia vyombo vya habari na hivyo kuchochea washabiki wake kushambulia waandishi wa habari.

Tayari waandishi wameanza kuomba ulinzi wa polisi katika mikutano yake baada ya mwandishi mmoja kushambuliwa na kukutwa karatatsi kubwa lenye ujumbe alama ya Hitler na neno media.

Mchambuzi wa makala haya ni Mtanzania anayefanya shughuli zake nchini Marekani katika miji ya Washington DC na New York na amewahi kuwa mwandishi wa habari wa magazeti kadhaa hapa nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles