MAOFISA wa kampeni wa mgombea urais wa Chama cha Republican nchini hapa, Donald Trump, wamekiri mgombea wao huyo yuko nyuma ya mpinzani wake kutoka Chama cha Democratic, zikiwa zimesalia chini ya wiki mbili kabla ya uchaguzi kufanyika.
“Tuko nyuma. Kuna baadhi ya mambo ambayo yanamfaa yeye (Hillary Clinton),” alisema meneja wa kampeni wa Trump, Kellyanne Conway.
Hata hivyo, aliongeza: “Hatukati tamaa. Tunajua kwamba tunaweza kushinda.”
Ijumaa iliyopita, Trump alionekana kukiri uwezekano wa kushindwa.
Alisema iwapo atashinda, ashindwe au atoshane nguvu na mpinzani wake, ataridhishwa na juhudi zake.
Siku moja baadaye, alitangaza hatua ambazo atazichukua siku 100 akiwa madarakani iwapo atashinda.
Miongoni mwa hizo ni kuweka masharti mapya kwenye mchakato wa kisiasa wa kutafuta uungwaji mkono kisiasa, mikataba ya kibiashara na mabadiliko ya tabia nchi.
Kura mpya za maoni zinaonyesha mpinzani wake, Hillary Clinton anaongoza kwa mbali kitaifa na katika majimbo mengi yanayoshindaniwa.
Maofisa wa kampeni wa Hillary wamebashiri kwamba huu utakuwa ‘uchaguzi mkubwa zaidi katika historia ya Marekani’.
Meneja wake wa kampeni Robbie Mook aliambia Fox News Jumapili: “Watu watajitokeza kupiga kura zaidi ya wakati wowote.”
Kura za maoni katika majimbo ambayo ni ngome ya Chama cha Republican kama vile Utah na Arizona, zinaonyesha huenda majimbo hayo kwa mara ya kwanza kipindi cha miongo mingi yakamuunga mkono mgombea wa Democratic.
Kura za maoni Arizona zinaweza zikawa si sahihi, lakini iwapo ni hivyo, basi jimbo hilo huenda likaanzisha mtindo wa kura utakaomnufaisha Hillary mwaka 2016 na hapo baadaye kuwa jimbo la kushindaniwa.
Hilo pia linachangiwa na kuongezeka wapigakura wa asili ya Kilatino.
Kwa chama cha Democratic, hizo zitakuwa habari njema na ambazo zitawasaidia katika uchaguzi, lakini kwa Republican, huenda ukawa mwanzo wa masaibu ya kisiasa.
Zikiwa zimesalia siku 16 kabla ya uchaguzi, macho ya wengi yanaelekezwa zaidi kwenye kashfa za udhalilishaji wanawake zinazomkabili Trump.
Jumapili, mtoto wake Eric Trump alisema baba yake atakubali matokeo ikiwa tu uchaguzi utakuwa huru na wa haki.