WASHINGTON, MAREKANI
RAIS Donald Trump amewatupia lawama wakosoaji wake wa Chama cha Democratic kuwa wamesababisha kushindikana kwa makubaliano baina yake na Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong un.
Trump aliondoka kwenye mkutano huo nchini Vietnam bila ya kufikia makubaliano yoyote na Kim wiki iliyopita baada ya kutofautiana kuhusu masharti ya kuondoa vikwazo ilivyowekewa Korea Kaskazini.
Kupitia ujumbe aliouandika kwenye ukurasa wake wa Twitter Jumapili usiku, Trump aliwakosoa wana-Democrats kwa kuandaa kikao cha Bunge na wakili wake wa zamani, Michael Cohen wakati ambao alikuwa kwenye mazungumzo nyeti nje ya nchi.
Katika ujumbe huo, Trump aliandika kuwa wana-Democrats wameamua kumhoji mtuhumiwa mwongo na mdanganyifu wakati kuna mkutano muhimu wa nyuklia na Korea Kaskazini.
“Huu ni mtindo mpya dhaifu katika siasa za Marekani na pengine ndio chanzo kilichofanya mkutano huo kutofanikiwa,” alisema.