Mwandishi wetu-Mbeya
KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), Dk. Edwin Mhede, amewataka wazalishaji wanaotakiwa kutumia stempu za kodi za kielektroniki (Electronic Tax Stamp – ETS) kuendelea kuzitumia kama ilivyoelekezwa na sheria na taratibu za kodi kwa kuwa ina faida kwa wazalishaji wenyewe.
Dk. Mhede aliyasema hayo alipotembelea Kiwanda cha Bia mkoani Mbeya ili kujionea namna stempu za kodi za kieletroniki zinazofanya kazi katika kiwanda hicho.
Alisema ETS inasaidia kukusanya taarifa sahihi, si kwa matumizi ya kukadiria kodi pekee, bali inamsaidia pia mzalishaji kujua kiasi alichozalisha na kwa muda gani, lakini pia itamsaidia kuona kama kuna changamoto yoyote ili aifanyie kazi mapema.
“Ujumbe wangu kwa wazalishaji wengine ni kwamba waendelee kutumia stempu za kodi za kielektroniki kama ambavyo tumeelekezwa na sheria na taratibu za kodi, kwa kuwa inasaidia kuongeza ufanisi katika uzalishaji na kuweka taarifa sahihi za uzalishaji,” alisema Dk. Mhede.
Alisema katika matumizi ya mifumo, changamoto hazikosekani, lakini ni vema kutumia na kufahamu changamoto zilizopo na kuzifanyia kazi kwa kuwa si vibaya kuboresha mifumo pale ambapo umegundua changamoto katika matumizi ya mfumo huo.
Naye Meneja wa kiwanda hicho, Godwin Fabian, alisema kiwanda chao kinaamini ETS ni msaada kwa wazalishaji kwa kuwa inawezesha kugundua bidhaa zisizo halali na zinazoingia sokoni bila kufuata taratibu za uzalishaji na ulipaji kodi.
“Ujumbe wangu kwa wazalishaji wengine waone ni kitu kizuri na wasiogope kutumia stempu za kodi za kielektroniki kwa kuwa kama bidhaa zote zitawekwa stempu hizi, itasaidia kufahamu bidhaa zisizo halali zinazoingia sokoni na hivyo mfumo huu utasaidia kukabiliana nazo.
Matumizi ya stempu za kielektroniki za kodi kwa bidhaa zinazotozwa ushuru wa bidhaa, yalianzishwa kuchukua nafasi ya matumizi ya stempu za karatasi ambazo matumizi yake yalihusishwa na vitendo vya ukwepaji kodi pamoja na bidhaa bandia kwa kiasi kikubwa. Hii ni mojawapo ya hatua ya Serikali inayolenga kuboresha usimamizi wa kodi nchini.
Wanufaika wa mfumo huu ni Serikali, wazalishaji, waagizaji na watumiaji ambapo faida zake ni kulinda mapato ya Serikali kwa kuzuia bidhaa bandia, kumwezesha mtumiaji kutambua bidhaa yenye stempu halali kwa kutumia simu ya mkononi pamoja na kuongeza uhiari wa ulipaji kodi kwa kutengeneza wigo sawa wa ushindani kwa wafanyabiashara wote wanaozalisha na kuingiza bidhaa nchini.
Faida nyingine ni kuwezesha ufuatiliaji wa bidhaa kutoka viwandani, mipakani, bohari zilizoruhusiwa, majengo ya kutunzia bidhaa, sokoni hadi kwa mlaji na kuwezesha usimamizi wa bidhaa zinazotengenezwa au zinazoingizwa kutoka nje ya nchi.