MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imepata tuzo ya Ufunguo wa Dhahabu kwa mwaka 2016 baada ya utafiti wa upatikanaji wa taarifa kwenye ofisi za umma uliofanywa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) katika nchi 11 wanachama wa Shirika la Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alisema mamlaka imepata tuzo hiyo kutokana na ukusanyaji wake wa kazi kwa uwazi kwa umma.
Kayombo alisema kila mwaka umekuwa ukifanyika utafiti wa haki ya kupata taarifa na uliasisiwa Septemba 28, mwaka 2002 mjini Sofia, Bulgaria kwa lengo la kuona jinsi wanachi wanavyoweza kupata taarifa za maendeleo yao ama nchi kuwawezesha kufanya uamuzi sahihi na stahiki juu ya maisha yao na taifa kwa ujumla.
“Utafiti huu pia hutumika kama chombo cha kuwakumbusha walio katika madaraja na ofisi mbalimbali za umma juu ya wajibu wao wa kutumikia umma kwa uwazi na ukweli ili kuleta maendeleo stahiki nchini,” alisema Kayombo.
Alisema taasisi nyingine za umma zilizowahi kuongoza katika utafiti za nyuma tangu kuanza kwa mchakato huo ni Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Wizara ya Sheria na Katiba , Wizara ya Fedha, Uchumi na Mipango, Wizara ya Nishati na Madini na TRA.
Katika hatua nyingine, TRA kupitia Mkoa wa Kodi Ilala mwishoni mwa wiki iliyopita ilitoa elimu ya kodi kwa viongozi wa Serikali ya Mtaa wa wilaya hiyo kuwawezesha viongozi hao kuuipeleka kwa wananchi wake.
Akizungumza baada ya mafunzo hayo, Ofisa Huduma na Elimu wa Mkoa wa Kodi Ilala, Zakeo Kowelo alisema wamejipanga kuhakikisha elimu ya kodi inamfikia kila mwananchi na kwamba wanaamini kuwa viongozi hao wa mtaa wataifikisha kwa wananchi.
“Pamaoja na mafunzo lakini pia tunatarajia kuwa tunatembelea ofisi za watendaji wa mitaa kubadilishana uzoefu ikiwa ni pamoja na kutengeneza mazingira ya kuweza kukusanya kodi kwa urahisi kutoka kwa wafanyabiashara wa Kariakoo ambao wapo chini yao,” alisema Kowelo.