NA VERONICA KAZIMOTO
Wafanyabiashara wenye malimbikizo ya madeni ya kodi, wametakiwa kutuma maombi ya msamaha maalumu wa riba na adhabu kwenye malimbikizo hayo mapema kabla ya Novemba 30, mwaka huu.
Baada ya hatua hiyo, wataweza kunufaika na msamaha huo ambao umetolewa kwa lengo la kutoa unafuu kwa kuwapa fursa ya kulipa kodi ya msingi ndani ya mwaka wa fedha wa 2018/19.
Wito huo umetolewa jana na Ofisa Elimu Mkuu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rose Mahendeka, wakati wa semina elekezi kwa wafanyabiashara, wadau na washauri wa wafanyabiashara kuhusu msamaha huo iliyofanyika mkoani Tabora.
“Nachukua fursa hii kutoa wito kwenu wafanyabiashara kutuma maombi ya msamaha wa riba na adhabu ya malimbikizo ya madeni ya kodi ambapo mwisho wa kutuma maombi ya msamaha huu ni tarehe 30 Novemba, mwaka huu.
“Mara nyingi wafanyabiashara huwa mnajitokeza mwishoni kabisa mwa tarehe zinazoonyesha mwisho wa kulipa, kuwasilisha au kutuma maombi fulani suala linalosababisha foleni na msongamano mkubwa katika kutoa huduma katika ofisi zetu.
“Kwa hiyo nawaomba msisubiri tarehe za mwisho kuleta barua za maombi ya msamaha huu wa riba na adhabu ya madeni ya kodi na naomba mjue kwamba, huu ndio muda mwafaka wa kila mwenye malimbikizo ya madeni kutuma maombi katika ofisi ya TRA katika mkoa wake kikodi,” alisema Mahendeka.
Naye, Ofisa Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka hiyo, Chama Siriwa, alisema mwombaji wa msamaha wa riba na adhabu ya malimbikizo ya kodi, anapaswa kutoa maelezo na vielelezo halisi, wakati wa uwasilishaji wa maombi yake.
“Kila mwombaji anatakiwa kutoa taarifa za ukweli wakati anaomba msamaha huu na endapo itabainika kuwa mwombaji ametoa taarifa za udanganyifu, kamishna mkuu anayo haki kisheria kubatilisha na hivyo kupelekea mwombaji kupoteza sifa za kufaidika na msamaha huu,” alifafanua Siriwa.