Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Shirika la Petroli Tanzania (TPDC) limefafanua changamoto ya hivi karibuni iliyosababisha msongamano wa magari kwenye vituo vya kujazia gesi, hususan Kituo cha Airport jijini Dar es Salaam. Tatizo hilo limesababishwa na hitilafu ya umeme, hali iliyosababisha foleni kubwa ya magari yaliyokuwa yakisubiri huduma ya gesi.
Kaimu Mkurugenzi wa Biashara ya Mafuta na Gesi wa TPDC, Mhandisi Emmanuel Gilbert, akizungumza Oktoba 3, 2024, alisema tatizo hilo liliathiri uendeshaji wa kituo hicho cha Airport hadi pale umeme uliporejea na huduma kuendelea. “Chanzo cha tatizo hili ni kukosekana kwa umeme, hivyo kituo kilishindwa kuendelea na huduma ya kujaza gesi kwenye magari hadi hitilafu hiyo ilipopatiwa ufumbuzi,” alisema.
Gilbert pia alieleza kuwa TPDC imefungua milango kwa sekta binafsi kuwekeza kwenye ujenzi wa vituo vya gesi, lakini mwitikio umekuwa mdogo. Hadi sasa, zaidi ya kampuni 40 zimepewa idhini ya kuwekeza kwenye sekta hii, lakini utekelezaji bado umesuasua.
“Kufikia sasa, magari yanayotumia gesi ni takriban 4,800, huku vituo vilivyopo vikiwa na uwezo wa kuhudumia magari 1,200 hadi 1,500 pekee, hali inayochangia msongamano,” aliongeza Mhandisi Gilbert.
Shirika la TPDC linatarajia sekta binafsi kuchukua jukumu kubwa zaidi katika kuboresha huduma na kuongeza vituo vya gesi ili kupunguza changamoto zinazojitokeza.