Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Shirika la Maendeleo ya Petrol Tanzania (TPDC) linatarajia kufanya marekebisho ya visima vya kuzalisha gesi asilia kwenye kitalu cha Mnazi bay mkoani Mtwara lengo likiwa ni kuongeza ufanisi wa uzalishaji ambapo kwasasa asilimia 65 za uzalishaji wa umeme nchini unategemea gesi.
Akizungumza leo Julai 28, jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari Meneja Muendeshaji na Uzalishaji wa Gesi wa TPDC, Mhandisi Felix Nanguka amesema ukarabati wa visima ni kwa ajili ya kuendeleza gesi inayozalishwa nchini ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi.
“Tunatarajia kukarabati visima vilivyopo mnazi bay Mtwara ili kuhakikisha vinafanya kazi kwa ufanisi na kuongeza kiwango cha umeme kinachozalishwa nchini,” amesema Mhandisi Nanguka.
Amesema pamoja na ukarabati wa visima mnazi bay pia wanatarajia kuongeza uzalishaji wa kisima namba 1 kmd 1 ambacho kinatoa gesi kwa ajili ya umeme unaozalishwa mkoa wa Lindi na Mtwara na pia gesi inayoingia kwenye bomba kubwa linalopeleka gesi Dar es Salaam kwa ajilim ya matumizi ya grid na viwanda.
Amesema kwa sasa kisima hicho kinauwezo wa kuzalisha takribani futi za ujazo milioni 11 kwa siku ambapo baada ya marekebisho kisima hiko kitaongeza ujazo wa futi milioni 7 hivyo ufanisi wa kisma hiko utafikia asilimia 65.
“Kwa sasa uzalishaji wa umeme nchini zaidi ya asilimia 65 unategemea gesi inayozalishwa nchini hivyo zoezi hili ni muhimu kwani litasaidia ongezeko la mega watt 35 za umeme nchini,” amesema Nanguka.
Aidha, TPDC imeweka kwenye mipango yake kuongeza uzalishaji kwenye maeneo mengine ikiwa marekebisho ya visima vyote nchini pia uendelezaji wa gesi nambayo inatarajiwa kuanza kutumika 2025.